Mlipuko Mbaya katika Baa ya Uswisi: Watu 40 Wahofiwa Kufariki, Wengine 100 Kujeruhiwa
Uswisi – Takriban watu 40 wanahofiwa kufariki dunia na wengine 100 wamejeruhiwa baada ya mlipuko kutokea katika baa maarufu ya watalii na mapumziko ya Constellation nchini Uswisi wakati wa sherehe za mkesha wa Mwaka Mpya.
Mashuhuda wa tukio hilo wameeleza kuwa moto huo ulisababishwa na mshumaa uliowekwa ndani ya chupa ya champagne katika sehemu ya chini ya ukumbi huo, uliopo katika mji wa milimani wa Crans-Montana.
Kwa mujibu wa maofisa usalama wa mji huo, wameeleza kuwa watu wengi waliokuwepo eneo hilo ni watalii wa kigeni.
Mlipuko huo uliotokea saa 1:30 asubuhi ambapo ni saa 3:30 asubuhi leo Alhamisi Januari 1, 2026 kwa saa za Afrika Mashariki, unatajwa kuleta simanzi katika nchi hiyo ikiwa ni siku ya kwanza ya mwaka mpya.
Picha zilizochapishwa zimeonyesha jengo hilo likiteketea, huku huduma za dharura zikiendelea kutolewa kwa majeruhi.
TNC imebaini kuwa daktari aliyekuwepo eneo la tukio amesema idadi ya vifo huenda ikawa ikaongezeka na hasara ni kubwa, hivyo takriban watu 40 wamefariki na 100 kujeruhiwa.
Shuhuda ambaye alikuwa ndani ya baa hiyo wakati mlipuko ulipotokea, alieleza kuwa moto ulianza baada ya watu kusherehekea kwa chupa za champagne zilizokuwa zimepambwa na mishumaa inayowaka.
"Baadhi ya chupa zilikuwa karibu na dari, ndipo moto ulipoanza. Dari lote lilishika moto na moto ukaenea kwa kasi. Ilitokea ndani ya sekunde chache. Tulikimbia nje tukipiga kelele na kulia," ameeleza shuhuda huyo.