Tanzania Inaimarisha Nafasi yake kama Kitovu cha Biashara Barani Afrika
Tanzania kwa sasa inajikuta katika kipindi cha kipekee cha kihistoria, ikiwa ni nchi pekee mwanachama inayounganisha Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa ufanisi mkubwa.
Nafasi hii ya kijiografia si tu zawadi ya asili, bali ni karata muhimu ya kiuchumi ambayo ikitumiwa vyema inaweza kuifanya nchi kuwa kitovu kikuu cha biashara na uwekezaji barani Afrika. Uwepo wa Tanzania kama lango kuu la bahari kwa nchi nane zisizo na bandari, kumeifanya nchi hii kuwa mhimili wa usafirishaji na mawasiliano unaounganisha Kaskazini na Kusini mwa bara hili.
Nafasi ya Tanzania Katika EAC
Ndani ya Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), Tanzania imekuwa mchezaji muhimu katika soko lenye watu zaidi ya milioni 300. Kwa kupanuka kwa jumuia hii hadi kufika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Tanzania imekuwa kiunganishi cha biashara kati ya Bahari ya Hindi na Bahari ya Atlantic.
Uwekezaji mkubwa katika miradi ya miundombinu kama Reli ya Kisasa (SGR) na upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam ni hatua madhubuti zinazolenga kutoa huduma bora kwa majirani zetu wa EAC kwani inaongeza mzunguko wa fedha za kigeni na kutengeneza fursa za ajira kwa vijana wa Kitanzania kupitia sekta ya uchukuzi na huduma.
Ushirikiano wa SADC Unaimarisha Uchumi
Upande wa Kusini, katika jumuia ya SADC, Tanzania inatambulika kama nguzo ya utulivu na usalama, sifa ambazo ni msingi wa biashara. SADC inatoa fursa kwa Tanzania kufikia masoko makubwa kama Afrika Kusini, Angola, na Zimbabwe.
Kupitia soko hilo sekta ya kilimo inachukua nafasi ya mbele ambapo Tanzania ina fursa ya kuwa "ghala la chakula" kwa nchi za kusini ambazo mara kwa mara hukabiliwa na changamoto za tabianchi.
Kupitia itifaki za SADC za biashara, bidhaa za viwandani kutoka Tanzania sasa zinaweza kuingia katika masoko ya kusini bila vikwazo vikubwa, jambo linalochochea ukuaji wa viwanda vya ndani na kuongeza thamani ya mazao yetu.
Changamoto na Fursa Zinazosubiri
Hata hivyo, ili kunufaika kikamilifu na nafasi hii ya kimkakati, Tanzania inapaswa kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na kuondoa vikwazo visivyo vya kodi (NTBs).
Ushindani ndani ya EAC na SADC ni mkubwa hivyo ufanisi katika bandari zetu na kasi ya utoaji huduma mipakani ni mambo ambayo hayawezi kupuuzwa na ili kufanikisha hilo Serikali inapaswa kuhimiza sekta binafsi kuchangamkia fursa hizi kwa kuzalisha bidhaa zinazokidhi viwango vya kimataifa.
Pia diplomasia ya kiuchumi lazima iendelee kuwa kipaumbele, tukihakikisha kuwa mikataba ya kibiashara tunayoingia inalinda maslahi ya wazalishaji wa ndani huku ikivutia mitaji kutoka nje.
AfCFTA Inaimarisha Nafasi ya Tanzania
Vilevile, nafasi ya Tanzania katika Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika (AfCFTA) inaimarishwa zaidi na uanachama wake katika EAC na SADC. Kwa kuwa na mguu mmoja Kaskazini na mwingine Kusini, Tanzania inakuwa kama "daraja la dhahabu" la biashara.
Hii ina maana kuwa mwekezaji anayeweka kiwanda chake nchini Tanzania ana uhakika wa kufikia soko la nchi karibu 20 kwa urahisi zaidi kuliko nchi nyingine yoyote ile. Hii ni sifa ya kipekee inayopaswa kutumiwa kama chambo cha kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni (FDI) ambao utaleta teknolojia na ujuzi mpya.
Mustakabali Mkubwa Unasubiri
Kwa kuhitimisha, mustakabali wa uchumi wa Tanzania unategemea jinsi tutakavyoweza kuicheza karata yetu ya kijiografia ndani ya EAC na SADC. Tanzania si nchi ya pembezoni tena ni moyo wa biashara ya kikanda.
Tukijikita katika kuimarisha nishati ya uhakika, miundombinu ya kisasa na rasilimali watu yenye ujuzi, hakuna shaka kuwa Tanzania itakuwa injini kuu ya uchumi katika ukanda huu.
Wakati ni sasa kwa watanzania wote, kuanzia wakulima wadogo hadi wafanyabiashara wakubwa, kutambua kuwa soko letu si Tanzania pekee, bali ni bara zima la Afrika.