Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar: Miradi 107 Yazinduliwa
Unguja – Katika maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar, mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii yamejitokeza, yakiwa ni ushahidi wa maendeleo na haiba ya visiwa hivyo.
Katika maadhimisho ya mwaka huu, jumla ya miradi 107 katika sekta za elimu, afya, miundombinu ya barabara, masoko na nyumba za biashara, makazi na wafanyakazi imezinduliwa na kuwekwa mawe ya msingi Unguja na Pemba.
Shughuli hizo zilianza Desemba 22, 2025 na kuhitimishwa Januari 11, 2026, ambapo viongozi waliohudhuria ufunguzi wa miradi hiyo walielezwa historia ya Mapinduzi.
Umoja na Mshikamano Muhimu kwa Maendeleo
Akizungumza katika hafla ya kuzindua mradi wa shule ya Kizimkazi, Makamu wa Rais, Dk. Emanuel Nchimbi, alishauri kuwepo kwa umoja na mshikamano katika kujenga nguvu ya pamoja ili kuendeleza Mapinduzi.
"Wosia wangu mkubwa kwa watu wote, vijana na wazee kwanza umoja wetu uwe na nguvu zaidi tuijue serikali yetu, tuombee dua mambo yote yanayofanyika tufanikiwe na tuzidi kufanikiwa kama ilivyotokea Mapinduzi," alisema.
"Ukiangalia haya yote yanayofanyika ni kutimiza ndoto ya waasisi wa Mapinduzi Zanzibar ambayo lengo lake ilikuwa ni kuleta huduma bora kwa wananchi," aliongeza Dk. Nchimbi.
Mabadiliko Makubwa Katika Sekta ya Elimu
Alisema kabla ya Mapinduzi maisha ya Wazanzibari yalikuwa duni na fursa za masomo zilikuwa chache kwani shule zilikuwa 68 na waliopata nafasi za kusoma walikuwa 25,000 tena kwa ubaguzi mkubwa.
"Sasa ukiangalia katika miaka 62 yamefanyika mabadiliko makubwa kama walivyotarajia waasisi wetu, zimefikia shule 1,200 kutoka 68 zilizokuwapo awali," alisema.
Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kwa sasa kuna wanafunzi zaidi ya 600,000. Wakati wa Mapinduzi hakukuwa na chuo kikuu hata kimoja, lakini leo Zanzibar kuna vyuo vikuu vitano.
Uwekezaji na Ajira Zaidi ya 25,000
Kwa upande wa uwekezaji, kwa mujibu wa Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, zaidi ya miradi 558 imesajiliwa ikiwa na thamani ya Dola za Marekani 6.9 bilioni ambazo zitatoa ajira 25,000.
Serikali imeweka mikakati ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje, na kuunda mazingira rafiki ya biashara na kuifanya sekta ya utalii kuwa moja ya vivutio vikubwa vya utalii barani Afrika.
Uchumi na Utalii Wanaongezeka
Wataalamu wanazungumzia mabadiliko hayo wakisema Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika sekta ya utalii, huku idadi ya watalii ikiongezeka kwa asilimia 14, kutoka 568,312 Novemba 2023 hadi kufikia watalii zaidi ya 750,000.
Uchumi wa Zanzibar umeonyesha kukua ukifikia asilimia 7.5 mwaka 2024, ikilinganishwa na asilimia 5.1 mwaka 2021.
Sekta ya Uvuvi Inaendelea Vizuri
Katika sekta ya uvuvi na ufugaji wa mazao ya baharini, kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Hamad Bakar Hamad, uzalishaji wa samaki umeongezeka kwa asilimia 107.2, kutoka tani 38,107 mwaka 2020 hadi tani 78,943 mwaka 2024.
Bandari na biashara za usafiri wa majini pia ni miongoni mwa sekta ambazo zimeonesha kukua ambapo ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani na utanuzi wa bandari za Mkoani na Shumba unatarajiwa kuimarisha sekta ya usafiri wa majini.
Wananchi Wanashuhudia Mabadiliko
Mabadiliko haya yamewezekana kutokana na juhudi za Serikali ya Zanzibar katika kuboresha miundombinu, kukuza sekta ya utalii, na kuimarisha uchumi wa buluu.
Mchambuzi wa masuala ya kijamii Zanzibar, Khamis Ameir Ali, alisema kuna mabadiliko makubwa yanayoonekana kutokana na kujizatiti katika uimarishaji huduma.
"Katika historia inaelezwa wazi namna ambavyo maisha ya wananchi yalivyokuwa kabla ya Mapinduzi, ubaguzi na unyanyasaji wa kikabila na rangi, lakini leo hii tunaona hatua mbalimbali zinazopigwa katika sekta muhimu za huduma," alisema.
"Ukiangalia katika sekta za huduma kama elimu na afya, wakati ule zilikuwa shida na za kibaguzi, waliopata huduma hizo walikuwa wachache hususani wanaotoka katika upande wa watawala."
Hata hivyo, alisema licha ya hatua hizo bado zinahitajika jitihada za makusudi kuhakikisha hata zile changamoto ambazo bado zinaonekana, ziishe kabisa.
Zulima Haji Amour, mkazi wa Kiembesamaki Unguja, alisema hawakuwahi kufikiria kuona mabadiliko makubwa kwa namna wanavyoshuhudia sasa.
"Tunaona mabadiliko mengi ya kiuchumi na kijamii, Zanzibar ya miaka ile sio ya sasa, ikitokea mtu aliyeondoka kipindi hicho akija atapotea, nadhani haya ndio yalilengwa kufanyika kuwakomboa wananchi na kufurahia maisha ndani ya nchi yao," alisema.
Msamaha kwa Wafungwa
Rais Hussein Mwinyi alitoa msamaha kwa wafungwa 17 waliokuwa wakitumikia adhabu zao magerezani. Kati ya hao 11 wanatokea Unguja na sita ni wa Pemba.