Unguja – Ujenzi wa maabara ya kisasa ya utafiti wa afya ya wanyama unatarajiwa kuongeza uwekezaji katika sekta ya mifugo nchini.
Imeelezwa kuwa wawekezaji wengi wanaotaka kuwekeza kwenye sekta ya mifugo wamekuwa wakiuliza uwapo wa huduma za matibabu ya mifugo kabla ya kufanya maamuzi ya uwekezaji.
Maabara hii imejengwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti ya Friedrich Loeffler Institute (FLI) ya Ujerumani kwa gharama ya shilingi bilioni 1.2.
Uzinduzi wa maabara ya afya ya wanyama ulifanyika Januari 7, 2026 katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo Zanzibar (Zaliri), Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya sherehe za kuadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kuongeza Uwekezaji wa Mifugo
Naibu Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Dk Salum Soud Hamed amesema hatua hii itaongeza kasi ya uwekezaji katika sekta ya mifugo.
"Mara nyingi wawekezaji walipokuwa wakitaka kuwekeza kwenye sekta ya mifugo, jambo la kwanza walikuwa wakiuliza kuhusu matibabu ya wanyama, kwa hiyo kujengwa maabara hii kutaongeza chachu ya uwekezaji katika sekta ya mifugo," amesema Dk Salum.
Mifugo ni moja ya sekta muhimu za kiuchumi kwa wananchi hasa wa vijijini na ni chanzo cha kipato na chakula.
Kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, sekta ya mifugo imekuwa ikichangia asilimia 12 ya jumla ya sekta ya kilimo (asilimia 24.3) ya pato la Taifa.
Teknolojia ya Kisasa
Serikali inalenga kuleta mageuzi katika sekta ya mifugo kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia za kuongeza uzalishaji na tija pamoja na kuimarisha miundombinu ya uzalishaji.
Maabara hii itawafaidia si wafugaji na wakulima tu, bali pia wadau wa sekta ya misitu hususani kwa upande wa wanyama pori, ambao nao afya zao pia huathirika na maradhi na watahitaji uchunguzi wa kina wa maabara.
Mkurugenzi wa FLI, Profess Dk Sascha Knauf amesema maabara yenye miundombinu ya kisasa ni kwa ajili ya binadamu na wanyama na itasaidia vizazi vya sasa na vijavyo.
Uwekezaji na Vifaa
Mkurugenzi Mkuu wa Zaliri, Abdallah Ibrahim Ali amesema kazi za utafiti zinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo upungufu wa vifaa na wataalamu kuwa katika hatari ya kupata magonjwa. Pia kuna changamoto ya wataalamu wachache katika maabara kisiwani.
Hata hivyo, wataalamu watatu wamepelekwa masomoni nchini Ujerumani na watakuja kuongeza nguvu za kazi.
Maabara hii ya aina yake ni ya mfumo wa makontena na ni ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki. Inategemewa kutoa huduma za kiuchunguzi kwa viwango vya kimataifa.
Maabara pia itakuwa na mifumo ya Tehama ambayo itawasiliana moja kwa moja na maabara kuu ya FLI ya Ujerumani.
Gharama za mradi huu ni shilingi bilioni 1.2, ambapo shilingi milioni 450 zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na shilingi milioni 750 zimetolewa na FLI ya Ujerumani.
Vifaa vya Kisasa
FLI imewasilisha vifaa vyote vya kisasa kwa ajili ya maabara ya utafiti wa afya ya wanyama, ikiwemo mfumo wa maabara wa makontena mawili, Bio-bank mbili kwa ajili ya kuhifadhia sampuli za wanyama kwa muda mrefu.
Vifaa vingine ni pamoja na jenereta mbili kila moja ikiwa na uwezo wa kilowati 15 na gari moja aina ya Double cabin kwa ajili ya kazi za kukusanya sampuli.
Serikali ya Mapinduzi pia imekamilisha ujenzi wa maabara ya microbiology na Parasitology, mabanda ya utafiti wa mbuzi wa nyama, ukumbi wa mkutano, ofisi kwa ajili ya watumishi wa maabara pamoja na vyoo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman amesema Taasisi imeanzishwa ikiwa na dira ya kuwa na ubora wa kimataifa katika utafiti unaotoa majibu kwa matatizo ya umasikini na uhaba wa chakula nchini.
Lengo kuu ni kuchangia katika kukuza uchumi kwa kuendeleza sekta ya kilimo, mifugo na rasilimali za misitu nchini, kwa njia ya utafiti na kubuni teknolojia za kisasa na kuzipeleka kwa wadau.