Guinea: Jenerali Mamady Doumbouya Ashinda Uchaguzi wa Urais
Guinea. Jenerali Mamady Doumbouya amechaguliwa kuwa Rais wa Guinea baada ya kupata kura nyingi, kulingana na matokeo ya awali ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo, huku mitandao ya kijamii ikizimwa.
Kiongozi huyo sasa amechaguliwa rasmi katika uchaguzi uliowahusisha wananchi wa Taifa hilo, baada ya kuchukua madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi miaka minne iliyopita.
Hata hivyo, vikundi vya kiraia vinavyopigania kurejeshwa kwa utawala wa kiraia vimekemea uchaguzi huo na kuutaja kuwa ni maigizo baada ya wagombea wakuu kuzuiwa kushiriki. Aidha, wagombea wa upinzani walisema uchaguzi huo uligubikwa na dosari mbalimbali.
Siku ya Jumatatu, upatikanaji wa mitandao ya kijamii ya TikTok, YouTube na Facebook ulifungwa wakati raia wa Guinea wakisubiri matokeo ya uchaguzi.
Hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kuhusiana na kufungwa kwa mitandao na madhara yake kwa ukosoaji wa matokeo ya uchaguzi.
Matokeo ya awali yaliyotangazwa Jumanne Desemba 30, 2025 yalionyesha Jenerali Doumbouya amepata asilimia 86.72 ya kura zote katika uchaguzi uliofanyika Desemba 28, idadi inayompa ushindi na kuzidi kiwango kinachohitaji kufanyika kwa duru ya pili ya kura.
Ushindi huo unampa kiongozi huyo mamlaka ya kuongoza kwa kipindi cha miaka saba. Hata hivyo, iwapo matokeo hayo yatapingwa, Mahakama Kuu ya nchi hiyo itatoa siku nane ili kuyathibitisha madai yatakayowasilishwa.