Serikali Yaagiza Ugawaji Sawa wa Maji Dar es Salaam
Dar es Salaam. Wananchi wakiendelea kulalamikia changamoto ya upatikanaji wa huduma majisafi na salama inayoathiri mfumo wa maisha ya baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam, Serikali imeagiza maji yaliyopo yagawanywe kwa usawa.
Vilevile, imeagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) kuweka wazi ratiba ya mgawo wa maji ili watu wajiandae na kuyahifadhi kwa siku ambazo hayatakuwepo.
Changamoto ya maji imebadilisha shughuli za kila siku, uchumi wa kaya na afya za baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam, wengine wakitumia muda mwingi kutafuta huduma hiyo muhimu.
Maeneo kama Tabata, Kariakoo, Segerea, Temeke na mengineyo, wakazi wake wamekuwa wakiamka alfajiri kusaka maji na wengine kusubiri kwenye visima ambavyo hutoa maji kwa muda usiotabirika.
Baadhi wanalazimika wananunua dumu la maji kwa Sh1,000 badala ya Sh200 za awali.
Akizungumza kwa simu Desemba 12, 2025 kwenye kikao cha wahariri na Dawasa, akiwa jijini Dodoma, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema ni haki ya wananchi kulalamika kutopata huduma.
"Kwa kipindi hiki ambacho tumekutana na changamoto hii tuwe wavumilivu na kuonyesha mshikamano kwani ni cha mpito tu," amesema.
Sababu za Upungufu wa Maji
Desemba 6, Dawasa katika taarifa kwa umma iliwataarifu wateja na wananchi wanaohudumiwa na mtambo wa kuzalisha maji Ruvu Chini (kuanzia Bagamoyo, Tegeta, Boko, Mbezi Beach, Mwenge, Kinondoni, Mwananyamala, Masaki hadi Ilala) kuwa kumekuwa na upungufu wa huduma ya maji katika maeneo mengi kutokana na uzalishaji kushuka zaidi ya kiwango cha kawaida.
Dawasa ilisema upungufu huo unatokana na sababu mbalimbali ikiwemo kushuka kwa kina cha Mto Ruvu iliyosababishwa na kuchelewa kwa mvua.
Kwa mtambo wa Ruvu Juu katika maeneo ya kuanzia Kibaha, Kibamba, Kimara, Tabata, Kinyerezi, Pugu hadi Kisarawe, Dawasa ilisema hali ya uzalishaji maji inaendelea vizuri na huduma inawafikia wananchi.
Ilieleza jitihada mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa kwa kushirikiana na Wizara ya Maji, ikiwemo kusitisha matumizi ya maji ya Mto Ruvu kwenye shughuli za kilimo na kuyaelekeza katika matumizi ya binadamu pekee na kuongeza matumizi ya visima ili kupunguza changamoto.
Waziri Aweso ametaka uwepo wa ushirikishwaji wa wadau na taasisi binafsi, wakiwamo wenye visima vikubwa ambao wanatoa huduma za maji kwa ajili ya kuwasaidia wananchi katika kipindi cha mpito cha changamoto ya upatikanaji wa maji.
Kiwango cha Uzalishaji
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Dawasa, Mkama Bwire, amesema kiwango cha maji katika mtambo wa Ruvu Chini kimepungua kutoka uzalishaji wa lita milioni 270 hadi lita milioni 50 ambacho hakijawahi kushuhudiwa kwa miaka ya karibuni.
Kwa upande wa mtambo wa Ruvu Juu, amesema una uwezo wa kuzalisha lita milioni 196 lakini kwa sasa uzalishaji ni lita milioni 151.4.
Bwire amesema maji kidogo yanayozalishwa yanasambazwa kwa uwiano sawa kati ya maeneo yote ili kupunguza athari kwa wananchi na imeongeza kasi ya kusimamia na kutatua mivujo haraka ili maji yasipotee hovyo.
"Nawaomba wananchi kwa kipindi hiki kuhifadhi maji, kutumia kwa uangalifu na kuwa wavumilivu wakati hatua za kudumu zikiendelea kutekelezwa," amesema.
Amesema wanaendelea kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha kila mwananchi anapata maji kwa uwiano sawa licha ya changamoto zilizopo.
Hatua za Muda Mfupi
Bwire ametaja hatua za muda mfupi zinazochukuliwa katika kipindi hiki cha changamoto ya maji kuwa ni kufufua visima katika maeneo mbalimbali ya huduma na kuunganisha maji yake moja kwa moja katika mtandao wa usambazaji ili kupunguza utegemezi mkubwa wa Mto Ruvu.
Baadhi ya visima hivyo amesema ni vya Mwananyamala, Tabata Matumbi, Segerea na Bonyokwa.
Pia, kazi ya kufunga pampu zenye uwezo mkubwa katika visima vya Kimbiji na Kigamboni inaendelea, hatua inayotarajiwa kuongeza uzalishaji wa maji kwa maelfu ya lita.
Hatua nyingine ili kuhakikisha maji yanatosha kwa matumizi ya binadamu, amesema ni kusitisha kwa muda vibali vya baadhi ya watumiaji wa maji, hususani sekta za kilimo na mifugo.
Vilevile kwa ushirikiano na Serikali ya Mkoa wa Pwani na Bodi ya Bonde la Wami–Ruvu, doria zinaendelea ili kuhakikisha hakuna matumizi ya ziada au yanayohatarisha chanzo cha maji.
Dawasa inaendelea kuhamasisha wananchi kutumia maji kwa uangalifu, kuyahifadhi na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima.