Sunday, March 15, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Instagram
TNC
  • Home
  • Home
No Result
View All Result
TNC
No Result
View All Result

RIPOTI MAALUMU: Hatari ya kiafya kukosekana vyoo mpakani Tunduma

by TNC
January 1, 2026
in Swahili
0
0
SHARES
2
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Mpaka wa Tunduma: Madereva Walalamika Kukosekana Vyoo vya Umma Licha ya Kutozwa Ushuru

Dar es Salaam. Ingawa kila lori hutozwa ushuru wa Sh15,000 kuvuka mpaka wa Tanzania na Zambia kwa ajili ya huduma za jamii, madereva wa malori hayo wanalalamikia kukosekana vyoo vya umma, hali inayowalazimu kuomba huduma hiyo katika nyumba za watu binafsi.

Kwa mujibu wa madereva hao, ushuru huo wa Sh15,000 hutozwa na uongozi wa Wilaya ya Momba, kupitia Halmashauri ya Mji wa Tunduma.

Hata hivyo, hawaelewi namna fedha hizo zinavyotumika, wakihoji kwa nini hata choo cha umma kinashindikana kujengwa.

Wakati madereva wakilalamika na kuhoji hayo, Serikali wilayani humo, inasema itaweka vibao kuonyesha vyoo vya masoko vilivyopo jirani na barabara, ili madereva wavitumie, badala ya kujenga choo kipya.

TNC imefika eneo hilo na kushuhudia vyoo vichache vilivyopo kwenye jengo la Kituo cha Huduma za Pamoja vinavyotumiwa na watumishi mpakani hapo.

Vilevile, si vyote vinavyotumika, viwili vimefungwa ikielezwa vimeharibika.

Madereva Walalamika Malipo bila Huduma

Kiongozi wa Chama cha Madereva Afrika kwa upande wa Tanzania, John Siaba amesema lori moja linapovuka mpakani hutozwa Sh15,000 kwa ajili ya usafi na miundombinu ya kijamii.

Licha ya malipo kufanyika, anasema katika eneo hilo hakuna vyoo vya umma kwa ajili ya madereva, hivyo hulazimika kwenda kwenye nyumba za watu binafsi kupata huduma.

"Tulizungumza kwenye kikao, halmashauri ilitwambia itafanya haraka kutujengea vyoo. Boda (mpaka) hii inavusha magari karibu 1,000 na kila moja inatozwa Sh15,000, fedha zote hizo inashindikana kujenga choo?" amehoji.

Ameeleza haoni sababu ya kutozwa ushuru huo kama madereva wanalazimika kuomba msaada wa huduma ya choo kwenye nyumba za watu binafsi ambako pia hutozwa kati ya Sh500 hadi Sh1,000.

"Madereva tunajisaidia kwenye vyoo vya watu binafsi, unakwenda unamuomba mtu anakusaidia, akikutoza fedha unampa, lakini hakuna choo cha umma. Tunaomba kijengwe choo cha angalau matundu sita na hata wakitoza fedha siyo shida," amesema.

Katika mpaka huo, kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), malori kati ya 1,100 hadi 1,400 yanavuka kutoka Tanzania kwenda nje ya nchi kwa siku.

Ripoti hiyo inaeleza kwa upande wa malori yanayotoka nje kuingia nchini kwa siku ni kati ya 400 hadi 600, kutegemea na nyakati husika.

Ukiacha malori yanayovuka, katika eneo hilo kuna pilika na shughuli nyingi za biashara.

Hassan Hassan, dereva mwingine wa lori, anasema zipo nyakati hasa msongamano unapokithiri, huwa wanalazimika kujisaidia haja ndogo barabarani, jambo ambalo si jema kwa afya.

"Unakuta umebanwa kupitiliza, huna pa kukimbilia zaidi ya kusimama pembeni ya gari unajisaidia. Msongamano wakati mwingine unakuwapo hadi usiku, huwezi kwenda kugonga nyumba ya mtu binafsi ameshalala muda huo," amesema.

Kwa upande wa vyoo vilivyopo jengo la huduma za pamoja, amesema vyote vinatumiwa na watumishi wa mpakani hapo na siyo madereva.

"Ni mtihani kwa ujumla, tunatozwa ushuru lakini hakuna vyoo. Kwa kuwa tunatumia muda mrefu kuwa ndani ya magari, kulipaswa kuwe na vyoo," amesema.

Wakazi Waeleza Changamoto za Usalama

Atuganile Kapyela, mkazi wa Mtaa wa Kilimanjaro ulio jirani na mpaka huo, anasema imekuwa kawaida kuombwa msaada wa huduma ya choo na madereva ambao huwasaidia bila kuwatoza chochote.

Ingawa anachukulia huduma hiyo kama msaada, kwa upande mwingine anasema hupata wasiwasi kuwaruhusu waingie chooni kwa kuwa wanalazimika kuingia ndani ya nyumba ndipo wafike kilipo choo.

"Fikiria unamruhusu mtu anaingia ndani mwako hujawahi kumwona, humjui, huna uhakika kama ni dereva kweli, ila unamruhusu tu kwa sababu ameomba msaada, inatia mashaka," amesema.

Ameeleza ipo historia ya wizi uliowahi kufanywa na mtu aliyeomba huduma ya choo, lakini akafanya vinginevyo, ndiyo sababu wenye nyumba wengi wanatoza fedha na wanamlinda kila anayeingia hadi anapotoka.

"Kuna mwenzetu amewahi kuibiwa. Mtu alijifanya dereva, akaomba akajisaidie, mwenye nyumba akamwamini, akaingia kujisaidia akaondoka na simu iliyokuwa sebuleni. Hii imefanya watu wawatoze na wawalinde," anasema.

Jambo muhimu zaidi, anasema ni Serikali kujenga vyoo kwa ajili ya madereva hao ili wasisumbue watu kuomba huduma kama inavyofanyika sasa.

Dalali Maneno, mwenye nyumba jirani na mpaka huo, anasema hamtozi yeyote fedha kupata huduma ya choo, lakini si kila anayeomba anamruhusu.

Anasema hilo linatokana na hofu ya wizi na uhalifu mwingine, hivyo ni wachache wanaopewa ruhusa kwenda kujisaidia.

"Hujui nani mwema na nani mbaya, utamruhusu kila mtu siku utafanyiwa ubaya. Pia, ukiwaruhusu wote choo kitajaa kabla ya wakati, kwa sababu madereva ni wengi na wakijua unaruhusu wanapeana taarifa," anasema.

Ameeleza karaha nyingine ya kuwaruhusu ni unadhifu wa nyumba husika, akifafanua wanapoingia baadhi hawasafishi vema vyoo na vinabaki na harufu, hivyo inahatarisha afya za wanafamilia.

"Suluhisho ni kujengewa vyoo vyao, ikiwezekana hata wachangishwe ilimradi wajengewe vyao. Nikiwa sipo nyumbani nimekataza watoto kuruhusu watu kujisaidia. Nikiwepo ndipo nawasaidia na najua inawapa changamoto," anasema.

Serikali Yaeleza Mpango wa Kutatua Tatizo

Akizungumzia hilo, Elias Mwandobo, Mkuu wa Wilaya ya Momba ulipo mpaka huo anasema mahitaji ya vyoo kwa ajili ya madereva ni miongoni mwa mambo yaliyozungumzwa wakati wa kikao cha viongozi, madereva, mawakala wa malori na wamiliki kilichofanyika mwanzoni mwa Desemba 2025.

Hata hivyo, amesema wametafakari na kuona hakuna haja ya kujenga choo kipya kwa ajili ya madereva wakati ambao Serikali inafanya maboresho mpakani hapo kuondoa msongamano.

Amesema kinachofanyika katika Barabara ya Sumbawanga yanakopanga foleni malori kuvuka mpaka, kuna masoko ya Chipaka na Majengo ambayo yote yana vyoo jirani na barabara, hivyo ndivyo vianze kutumiwa na madereva.

"Msongamano si jambo la kudumu, Serikali imeshatangaza mpango wa kutanua barabara kurahisisha malori kuvuka haraka. Upanuzi ukifanyika hiyo haja ya vyoo haitakuwapo kwa kuwa malori yatavuka moja kwa moja," amesema.

Mwandobo amesema halmashauri itaweka vibao kuonyesha vyoo vya umma vilipo ili madereva wachague kwa sababu haiwezekani kujenga choo barabarani kwa ajili ya madereva ilhali msongamano utakwisha.

Kuhusu tozo, amesema kila lori hutozwa ushuru wa maegesho na kuvuka kwa mujibu wa sheria ndogo za halmashauri husika na kwamba, fedha hizo zinatumika kwa ajili ya huduma za malori husika, zikiwamo za usafi wa barabara.

Wataalamu wa Afya Waeleza Hatari

Mtaalamu wa Afya ya Jamii, Dk Neema Msuya, anasema kukosekana kwa vyoo vya umma katika maeneo yenye mkusanyiko wa watu kama mpakani Tunduma, kunaongeza hatari ya milipuko ya magonjwa hasa ya kuambukiza.

"Watu wanapolazimika kujisaidia haja ndogo au kubwa nje ya vyoo rasmi, mazingira huchafuka haraka na vijidudu vya magonjwa kama kipindupindu, homa ya matumbo, kuhara damu na minyoo huenea kwa kasi.

"Mpaka ni eneo lenye watu kutoka maeneo tofauti, hivyo hatari ya kusambaza magonjwa kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine huwa kubwa zaidi," anasema.

Anabainisha kinyesi na mkojo vinapoachwa ovyo, huingia kwenye vumbi, maji ya mvua na mifereji, hali inayochangia kuenea kwa vijidudu kupitia mikono, viatu, vyombo vya chakula na hata maji ya matumizi ya kila siku.

"Hata mtu asiyejisaidia barabarani anaweza kuambukizwa kwa kugusa eneo lililochafuka au kula chakula kilichoandaliwa karibu na mazingira hayo. Vyoo si anasa, ni kinga ya msingi ya afya ya umma," anasema.

Mtaalamu wa Magonjwa ya Njia ya Mkojo, Dk Joseph Mrema, anasema kukosekana vyoo kunafanya madereva walazimike kuzuia haja kwa muda mrefu na hiyo ina madhara kwa afya.

"Madereva wengi wanapokosa vyoo hulazimika kuzuia haja ndogo au kubwa kwa saa nyingi, hali inayoongeza hatari ya maambukizi ya njia ya mkojo (UTI), matatizo ya figo, kuvimbiwa sugu na maumivu ya tumbo," anasema.

Vilevile, anasema kujisaidia sehemu zisizo salama huongeza uwezekano wa maambukizi ya ngozi na magonjwa ya tumbo, hasa pale kunapokosekana maji safi na sabuni ya kunawa mikono.

"Unapochanganya msongamano, uchovu wa safari ndefu, lishe isiyo bora na mazingira yasiyo na vyoo, unamweka dereva kwenye hatari ya matatizo ya kiafya yanayoweza kuathiri hata umakini wake barabarani na kusababisha ajali," anaeleza.

Tags: HatariKiafyakukosekanamaalumumpakaniRIPOTITundumavyoo
TNC

TNC

Next Post

Dk Shoo atoa wito wa imani, shukrani na kiroho mpya kuanza mwaka 2026

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Popular News

  • Zanzibar’s Leadership Advocates for Streamlined Tax System to Enhance Economic Growth

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanaohujumu miundombinu watachukuliwa hatua kali

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanaohujumu miundombinu watachukuliwa hatua kali

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wasiwasi juu ya Uchochezi wa Makada katika Jimbo la Katavi

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanawake Wanaonyonyesha Washauriwa Kula Milo Mitano Siku

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Category

  • English
  • Swahili

Socials

Instagram TikTok YouTube Facebook

About Us

TNC (Tanzania News Company) is the primary Source of News in English & Swahili in Tanzania

© 2025 TNC - Tanzania News Company

Welcome Back!

Login to your account below

Forgotten Password?

Retrieve your password

Please enter your username or email address to reset your password.

Log In
No Result
View All Result
  • Home

© 2025 TNC - Tanzania News Company