Wananchi Waendelea Kutafuta Ndugu Zao Vituo vya Polisi Bila Mafanikio
Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiwataka wanaotafuta ndugu zao kufika vituo vya polisi, baadhi ya Watanzania, wakiwamo wakazi wa jiji la Dar es Salaam, wameendelea kuzunguka vituo mbalimbali vya polisi wakitafuta ndugu na jamaa zao waliopotea tangu Oktoba 29, 2025, bila mafanikio.
Oktoba 29 mwaka huu, siku ya uchaguzi mkuu kuliibuka maandamano yaliyozua vurugu, kusababisha watu kupoteza maisha, uharibifu wa mali binafsi na miundombinu ya umma kuchomwa moto.
Jana, Novemba 23, 2025, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, aliwataka ndugu waliopoteza jamaa zao kwenda vituo vya polisi kutoa taarifa, kwani ndiyo mamlaka inayoshughulika na masuala hayo.
"Kwa hatua hii, sehemu sahihi ya kwenda ni Polisi, kwa sababu ndiyo watu wanaoweza kufanya jitihada za kuwatafuta waliopotea. Kwa sasa siwezi kutoa majibu kwa sababu matukio yalitokea wakati wa vurugu baada ya uchaguzi," alisema.
Hata hivyo, TNC imeshuhudia baadhi ya waliopotelewa na ndugu zao wakizunguka vituo kadhaa vya Polisi, vikiwemo Buguruni, Oysterbay na Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Baadhi ya waliozungumza na TNC wameeleza kwenda katika vituo hivyo bila mafanikio, na wamedai kujibiwa majibu yaleyale waliyojibiwa awali kwamba ndugu zao hawapo, na kuwataka kuzunguka vituo vingine.
Abdallah Said Amtafuta Ndugu Yake
Abdallah Said, mkazi wa Mabibo, ni miongoni mwa walioko katika jitihada za kumtafuta ndugu yake bila mafanikio. Anamtafuta Juma Said, aliyepotea tangu Oktoba 29 mwaka huu, baada ya kuondoka kazini eneo la Masaki, na alikuwa mfanyakazi katika moja ya hoteli.
Akieleza tukio hilo, Abdallah alisema siku hiyo wakati anaondoka nyumbani, mama yao alimshauri asitoke, lakini alisisitiza kwenda kazini akihofia kupoteza ajira yake endapo asingejitokeza.
Kwa kawaida, Juma alikuwa na tabia ya kurudi nyumbani siku inayofuata saa nne asubuhi, lakini safari hiyo hakurudi, na jitihada za kumtafuta hadi sasa hazijafanikiwa.
"Tulienda kuulizia kazini, wakasema alishaondoka. Tumezunguka vituo vya polisi na mochwari mbalimbali, lakini hadi sasa hatujampata," amesema Abdallah.
Amebainisha kuwa familia ilianza kukata tamaa, lakini ilipata matumaini mapya baada ya kauli ya Msigwa kuwataka wale ambao hawajawaona ndugu zao kwenda vituo vya polisi.
Hata hivyo, amesema kila kituo wanachopita wanajibiwa hayupo, ikiwemo Kituo cha Polisi Buguruni.
"Imekuwa kama utani. Kila kituo tunachokwenda tunaambiwa hakuna. Tunaomba Serikali itoe orodha kama kweli wapo watu ambao hawajajitokeza, ili tuweze kufuatilia kwa uhakika, badala ya kuzunguka bila majibu," amesema.
Hali Vituo vya Polisi
Katika upande mwingine, TNC ilifanikiwa kukutana na baadhi ya wananchi wengine waliofika Kituo cha Polisi Oysterbay kutafuta ndugu zao, lakini wengi wao walidai kujibiwa hawapo au bado hawajafanyiwa mahojiano.
Huku wengine wakikosa majina yao kwenye daftari la kituo, licha ya kudai kuonekana na ndugu zao wakiwa ndani, baada ya kuwasiliana kwa njia ya simu akiwa ameshikiliwa kituoni hapo.
Mama mmoja, aliyekataa kutajwa jina, amedai: "Nimekuja kumletea chai mdogo wangu. Nilivyoingia, nikaambiwa hayupo, ameenda kuhojiwa, lakini nilishawahi kuzungumza naye kwa simu na kuniambia yupo hapa."
Ameongeza kuwa mdogo wake alikamatwa nyumbani Mbezi siku 15 zilizopita kwa madai ya kuzungumza na mwanachama wa Chadema.
Mwananchi mmoja aliyekuwa ameshikiliwa kituoni hapo na kuachiwa wiki iliyopita alidai kuwa mahabusu zimefurika kupita kiasi.
"Nilipokuwa ndani, walikuwepo watu waliokuwa wanaingizwa wakiwa wamefungwa vitambaa vyeusi. Wakifunguliwa waliuliza, ‘Hapa ni wapi?’ wakaambiwa, ‘Hapa ni Oysterbay Polisi.’"
Amedai pia kuwa baadhi ya askari katika mapokezi wanawajibu vibaya wananchi wanaofika kuulizia ndugu zao.
TLS Yaitaka Serikali Kutoa Maelekezo ya Wazi
Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ikiwa miongoni mwa taasisi zinazowasaidia wananchi kutafuta ndugu na jamaa waliopotea, kimeitaka Serikali kutoa maelekezo ya wazi kuhusu vituo mahsusi vya kufuatilia taarifa hizo, badala ya kutoa kauli za jumla zisizotoa mwongozo thabiti.
Akizungumza na TNC, Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi, amesema kauli iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali, iliyowataka wananchi kwenda katika vituo vya polisi bila kubainisha ni vipi, imeendelea kuongeza mkanganyiko na kuwapa wananchi mzigo wa kuhangaika bila msaada wa uhakika.
"Wananchi wamezunguka vituo vya polisi kwa zaidi ya siku 20 wakitafuta wapendwa wao. Sasa, kwa kuwa amesema waende kituo cha polisi, basi awasaidie kwa kutaja ni kituo gani mahususi. Asitoe kauli ya jumla inayoendelea kuwatatiza wananchi," amesema.