Tanzania Yaendelea Kutumia Teknolojia ya Nyuklia Katika Maendeleo ya Kilimo na Afya
Arusha – Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki nchini (TAEC), Profesa Najat Kassim Mohammed, amethibitisha kuwa taasisi hiyo imeendelea kuendeleza matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika maendeleo ya sekta ya kilimo, afya na uhifadhi wa chakula nchini.
Akizungumza katika ofisi za taasisi hiyo jijini Arusha Februari 4, 2026 wakati wa ziara ya viongozi wa Shirika la Wakala wa Kimataifa la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA), Profesa Najat alisema TAEC inasimamia miradi mbalimbali ya kimkakati inayolenga kutatua changamoto na kuongeza tija katika jamii.
"Tunashirikiana na IAEA kwenye miradi ya kimkakati hapa nchini ambayo ipo chini ya TAEC na taasisi zingine. Tunao mradi wa kuzalisha mbegu bora ambao upo katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI)," alisema Profesa Najat.
Ametaja miradi mingine ikiwa ni pamoja na ujenzi wa maabara ya kisasa Zanzibar kwa ajili ya tafiti za wanyama, na ujenzi wa mashine ya Radiolojia kwa ajili ya kudhibiti vyakula visiharibike ambao upo katika hatua za ujenzi jijini Dar es Salaam.
Upanuzi wa Vituo vya Matibabu ya Saratani
Profesa Najat ameeleza kuwa Tanzania inaendelea na mradi mkubwa wa kuongeza vituo vya matibabu na uchunguzi wa saratani nchini.
"Kulikuwa na vituo vya serikali viwili tu ambavyo ni Ocean Road na Bugando, lakini sasa tunaongeza vituo kuwa sita ikiwemo KCMC, Benjamin Mkapa, kituo cha Mbeya na kituo cha Mnazi Mmoja Zanzibar," alisema.
Ameongeza kuwa ziara hiyo imekuja kuimarisha mahusiano na IAEA lakini pia kupitia miradi mbalimbali wanayoifadhili ambayo yanaletea manufaa makubwa kwa nchi.
Mpango wa Uzalishaji Umeme wa Nyuklia
Profesa Najat amebainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati imeanzisha mazungumzo ya Tanzania kuelekea kuzalisha umeme kwa njia ya nyuklia, hatua ambayo imepokea mkono wa rambirambi kutoka kwa IAEA.