Wizara ya Kilimo Kuwapa Kipaumbele Wabunifu wa Zana za Kilimo
Dar es Salaam – Wizara ya Kilimo imesema inawatambua na kuwapa kipaumbele wabunifu wa zana za kilimo nchini huku ikisema lengo ni kurahisisha shughuli hiyo muhimu ya kiuchumi.
Wabunifu hao wanaotengeneza zana kama matrekta, mashine za umwagiliaji, mashine za kuvunia mazao, mashine za kupandia, mashine za kuongeza thamani, majembe ya kukokotwa na ng’ombe wametakiwa kutengeneza zana hizo wakizingatia ubora.
Kauli hiyo imetolewa Alhamisi, Februari 5, 2026 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Athumani Kilundumya wakati akifunga mkutano wa Kwanza wa Kikanda wa Afrika kuhusu Matumizi Endelevu ya Zana za Kilimo jijini Dar es Salaam.
Kilundumya amesema katika kutambua mchango wao, Wizara imeandaa shindano la ubunifu litakalofanyika sikukuu ya wakulima maarufu Nanenane ambapo washindi watapata zawadi.
Kauli hiyo inakuja wakati Serikali kupitia Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ikizindua mpango wa taifa wa zana za kilimo awamu ya pili wa miaka kumi kuanzia 2025/26 hadi 2036.
"Kwanza tunaidadi ya watengenezaji wadogo tumeshawatambua na siku ya Nanenane tumeandaa eneo lao maalumu ili waweze kushindana," amesema Mhandisi Kilundumya.
Amesema lengo la Serikali ni kuanzisha vituo maalumu vya zana za kilimo vipatavyo 1,000 nchi nzima. Amesema yote hayo yanafanyika ili asiwepo Mtanzania anayelima ambaye atakuwa na kipato cha chini.
Mkutano huo umekusudiwa kuwa jukwaa la kubadilishana mbinu bora, kukuza ushirikiano wa kikanda, na kuhimiza matumizi endelevu ya zana za kilimo zinazochangia kuongeza tija na kipato kwa wakulima barani Afrika.