Saturday, April 18, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Instagram
TNC
  • Home
  • Home
No Result
View All Result
TNC
No Result
View All Result

Ukamataji wa makandarasi waibua mjadala wa kisheria

by TNC
February 2, 2026
in Swahili
0
0
SHARES
5
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Viongozi wa Serikali Walalamikiwa Kutoa Amri za Kukamatwa kwa Makandarasi Kinyume na Sheria

Dar es Salaam. Baadhi ya viongozi wa Serikali wamekuwa wakitoa amri ya kukamatwa kwa makandarasi wanaodaiwa kuchelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ambapo imeelezwa hatua hiyo inakiuka misingi ya utawala wa sheria.

Katika matukio mbalimbali yaliyoripotiwa, viongozi kadhaa wameonekana hadharani wakitoa maelekezo ya kuwakamata makandarasi waliochelewesha ujenzi wa barabara, shule, vituo vya afya na miradi mingine ya umma, wakieleza kufanya hivyo ili kulinda maslahi ya wananchi na kuhakikisha thamani ya fedha za umma inalindwa.

Desemba 23, Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Reuben Kwagilwa alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, kumshikilia mkandarasi anayejenga barabara ya Msongola mpaka atakapotoa maelezo ya kutosha juu ya kukamilika kwa barabara hiyo kutokana na kuzorota kwa ujenzi wake.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas, Januari 6, 2026, aliagiza kukamatwa kwa mkandarasi kutoka Kampuni ya Bogeta Engineering Limited kwa tuhuma za kughushi nyaraka pamoja na kushindwa kukamilisha ujenzi wa mabweni mawili, matundu 10 ya vyoo na vyumba sita vya madarasa katika Shule ya Sekondari ya Jenista Mhagama, Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani humo.

Katika kisa kingine, Januari 8, 2026, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Jafar Seif, alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Juma Sweda, kuhakikisha mkandarasi Hamerkop International Limited anakamatwa na kuhojiwa endapo atashindwa kukamilisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) katika Hospitali ya Mji Njombe (Kibena) kabla ya Februari 8, 2026.

Alisema uamuzi huo umetokana na mkandarasi huyo kuongezewa muda mara mbili nje ya makubaliano ya awali ya mkataba, lakini bado kasi ya ujenzi ni ndogo licha ya Serikali kumlipa Sh794.2 milioni kati ya Sh863.3 milioni.

Januari 27, 2026, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, alimuagiza Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) kuwaweka ndani mkandarasi Edwin Rwezahula na mhandisi mshauri Emmanuel Kisimba wa mradi wa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Nguzo Nane hadi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kwa kupuuza maagizo ya Mkuu wa Mkoa, Mboni Mhita.

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, Desemba 16, 2025, katika ziara yake mkoani Ruvuma, alimuagiza Mkuu wa Mkoa kumsimamia mkandarasi anayejenga barabara ya Itai hadi Ruanda, ikiwezekana ikamatwe hati yake ya kusafiria hadi atakapokamilisha ujenzi.

"Mwite mkandarasi, mwambie alishapokea fedha ya awali ya ujenzi wa barabara hii na kwa utaratibu wa kiserikali ni lazima kazi aliyopewa fedha imalizike. Afanye kazi nyingine na atoe cheti kwamba kazi hii imeshafanyika ndipo apewe malipo mengine," alisema Dk Mwigulu.

Alisema kumekuwapo utaratibu wa makandarasi kupokea fedha za awali na kuzitumia katika shughuli nyingine.

Hatua Zinakiuka Sheria – Wanasheria

Akizungumza Februari 1, 2026, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi amesema ucheleweshaji wa mradi unaohusisha mkandarasi ni suala la kimkataba, siyo kosa la jinai, hivyo halipaswi kushughulikiwa kwa amri za kukamatwa kutoka kwa viongozi wa kisiasa.

"Ukandarasi ni suala la mkataba. Kama mkandarasi ameshindwa kutekeleza mradi kwa wakati, suluhisho lake lipo kwenye masharti ya mkataba husika, ikiwemo faini, kusitishwa kwa mkataba au kufunguliwa kesi ya madai. Huwezi kugeuza mkataba kuwa jinai," amesema Mwabukusi.

Amesema viongozi wowote, wakiwemo wakuu wa mikoa au wilaya, hawana mamlaka ya kisheria ya kuamuru kukamatwa kwa mkandarasi kwa sababu ya kuchelewesha mradi; kufanya hivyo ni kuvuka mipaka ya madaraka waliyopewa na sheria.

"Mkuu wa Mkoa hana mamlaka ya kukamata mtu kwa sababu ya mkataba. Akitoa amri ya kukamatwa kwa mkandarasi, anakuwa amekiuka sheria na mkandarasi ana haki ya kufungua kesi na kudai fidia," amesema.

Mwabukusi amesema hata kunapokuwa na tuhuma za rushwa, ubadhirifu au udanganyifu katika utekelezaji wa mradi, viongozi wa kisiasa hawapaswi kutoa amri za kukamatwa, bali wanapaswa kuziwasilisha tuhuma hizo kwa vyombo vyenye mamlaka ya uchunguzi kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na polisi.

"Kama kuna viashiria vya rushwa, kazi ya viongozi ni kuwasilisha taarifa Takukuru, ambayo ndiyo yenye uwezo wa kuchunguza rushwa, siyo kiongozi kuvaa mamlaka ya upelelezi au polisi," amesema.

Amesema kuendelea kwa mtindo wa viongozi kutoa amri za kukamatwa kwa makandarasi kunaweza kuleta hofu kwa wawekezaji na makandarasi, jambo litakaloathiri kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuvuruga mazingira ya biashara nchini.

"Utawala wa sheria unatenganisha mamlaka za kisiasa, kiutendaji na kisheria. Tukizichanganya, tunajenga taifa la hofu badala ya taifa la sheria," amesema.

Mwabukusi amesema njia sahihi ya kushughulikia ucheleweshaji wa miradi ni kufuata mikataba, kufanya tathmini za kitaalamu na kuchukua hatua za kisheria kupitia mahakama pale inapobidi.

Maelezo hayo yanaenda sambamba na kauli ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ambaye Februari 1, 2026, alitoa siku 28 kwa Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Kagera kukamilisha taratibu za kusitisha mkataba na kumfukuza kazi mkandarasi aliyeshindwa kutekeleza ujenzi wa barabara ya Kyerwa–Omurushaka yenye urefu wa kilomita 50 kwa kiwango cha lami.

Ulega alisema mkandarasi Shandong Luqiao Co. Ltd ameshindwa kutimiza wajibu wake baada ya kufikia asilimia 5.4 pekee ya ujenzi licha ya kulipwa Sh9.15 bilioni kama malipo ya awali kati ya thamani ya mradi ya Sh94.3 bilioni.

Makandarasi Waeleza Changamoto Wanazokumbana Nazo

Akizungumza na TNC kwa sharti la kutotajwa jina, mkandarasi mmoja amesema ucheleweshaji wa miradi haujitokezi kwa makusudi bali unasababishwa na changamoto mbalimbali zilizo nje ya uwezo wao.

"Kuna miradi tunachelewa si kwa uzembe wetu, bali kwa sababu ya kuchelewa kulipwa madai yetu (certificates). Unakuta umefanya kazi, mkaguzi amethibitisha, lakini malipo yanachelewa miezi sita au zaidi. Inakuwa vigumu kuendelea na kazi bila fedha," amesema.

Amesema mvua zisizotabirika ni miongoni mwa sababu zinazoathiri ratiba ya utekelezaji wa miradi.

"Unasaini mkataba leo, ukiwa katika safari ya ujenzi mvua ikinyesha inabidi kusubiri hadi itakapoacha ndipo uendelee na ujenzi, na hili hukumbukwa kuhesabiwa ndani ya mkataba," amesema.

Amesema ucheleweshaji mwingine hutokana na mzigo mkubwa wa kazi kwa washauri elekezi (consultants), ambao wana jukumu la kuhakiki kazi, madai ya malipo (claims) na kutoa vyeti.

Kwa ujumla, amesema ili miradi ya maendeleo ikamilike kwa wakati na kwa ubora, ni lazima kila mdau atekeleze wajibu wake kwa uwazi, uadilifu na kwa kuzingatia mipango iliyowekwa.

Amesema hatua za viongozi kutoa amri za kukamatwa kwa makandarasi zinawatia hofu na kuvuruga mazingira ya kazi, kwani mikataba ina vifungu vinavyoeleza hatua za kuchukua endapo kuna ucheleweshaji.

"Mkataba una adhabu zake, ikiwemo faini au kusitishwa, lakini kukamatwa ni kama umetenda kosa la jinai; jambo hilo ni udhalilishaji kwa sababu halipo kwenye mkataba," amesema.

Mmoja wa wafanyakazi wa mradi wa daraja la barabara ya Kawawa, eneo la Kigogo, Januari 29, 2026, alisema kuchelewa kukamilika kwa mradi kunachangiwa na malipo.

"Tulipo hatujalipwa, na ukimuuliza bosi naye anasema hajalipwa. Mbaya zaidi, hakuna mapumziko; kiuhalisia ni ngumu kufanya kazi kwa weledi na kumaliza kwa wakati," amesema.

Ikumbukwe, Julai 31, 2025, Chama cha Umoja wa Makandarasi na Watoa Huduma Shirikishi Tanzania (Tucasa), kupitia msemaji wake Haris Kapiga, kilipendekeza kuanzishwa kwa Sheria ya Malipo (Security of Payment Act).

Alisema ucheleweshaji wa malipo ni moja ya vikwazo vinavyozorotesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na sekta ya ujenzi kwa ujumla.

"Makandarasi wengi wanakumbwa na hali ngumu ya kifedha, kupoteza ajira, kushindwa kukamilisha miradi kwa wakati na wengine hata kukata tamaa na kuchukua hatua hatarishi," alisema.

Sababu za Ucheleweshaji wa Miradi

Mtaalamu wa mipango na uwekezaji, Peter Cornel, amesema ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini unasababishwa na mnyororo wa wadau ambao ni mteja, mkandarasi, mshauri elekezi pamoja na mifumo ya malipo serikalini.

Cornel amesema utekelezaji wa mradi unatakiwa kuendana na mpango uliopo, lakini tatizo hujitokeza katika mlolongo wa malipo hadi fedha kupatikana, hali inayosababisha miradi kusuasua au kusimama kabisa, kwani mkandarasi analipwa kwa mfumo wa vyeti (certificates) baada ya kazi kupimwa na kuthibitishwa.

Amesema kuchelewa kwa malipo humlazimu mkandarasi kutumia fedha zake binafsi au malipo ya awali (advance), jambo ambalo si makandarasi wote wana uwezo wa kuhimili. Pia amesema uzoefu, nidhamu ya matumizi ya fedha pamoja na mabadiliko ya michoro ya ujenzi huathiri ratiba ya kazi na malipo.

"Mchina akipata malipo ya awali, anayatumia moja kwa moja kwenye mradi husika. Lakini kwa baadhi ya makandarasi wetu, advance inaweza kutumika kwenye miradi mingine au shughuli nyingine, matokeo yake mradi wa awali unakwama," amesema.

Tags: kisheriamakandarasiMjadalaukamatajiwaibua
TNC

TNC

Next Post

Court allows teacher to file case challenging President

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Popular News

  • Zanzibar’s Leadership Advocates for Streamlined Tax System to Enhance Economic Growth

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanaohujumu miundombinu watachukuliwa hatua kali

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanaohujumu miundombinu watachukuliwa hatua kali

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wasiwasi juu ya Uchochezi wa Makada katika Jimbo la Katavi

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanawake Wanaonyonyesha Washauriwa Kula Milo Mitano Siku

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Category

  • English
  • Swahili

Socials

Instagram TikTok YouTube Facebook

About Us

TNC (Tanzania News Company) is the primary Source of News in English & Swahili in Tanzania

© 2025 TNC - Tanzania News Company

Welcome Back!

Login to your account below

Forgotten Password?

Retrieve your password

Please enter your username or email address to reset your password.

Log In
No Result
View All Result
  • Home

© 2025 TNC - Tanzania News Company