Saturday, April 11, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Instagram
TNC
  • Home
  • Home
No Result
View All Result
TNC
No Result
View All Result

Mawazo kinzani mkakati ukianza kutekelezwa

by TNC
February 2, 2026
in Swahili
0
0
SHARES
2
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Mkakati Mpya wa KKK Waibua Mjadala kati ya Wataalamu wa Elimu

Dar es Salaam – Kutengenezwa kwa Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wa elimu ya awali na wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili umeibua mjadala miongoni mwa wataalamu wa elimu, wakiwamo wale wanaoonesha wasiwasi kuwa unaweza kuwa mkakati mwingine mzuri kwenye makaratasi bila kutatua changamoto halisi zilizopo shuleni.

Wadau wa elimu wameeleza kuwa tatizo si kukosekana kwa mikakati, bali ni utekelezaji wa mikakati iliyopo, wakishauri kuwa kabla ya kuanzisha mkakati mpya, Serikali ilipaswa kuimarisha utekelezaji wa sera na miongozo iliyopo, hususan katika kuongeza idadi ya walimu, kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuboresha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini.

Mkakati huo umeandaliwa baada ya kubainika kuwepo kwa idadi kubwa ya watoto wanaofika darasa la tatu wakiwa hawana stadi za msingi za kusoma, kuandika na kuhesabu, hali inayochangia kufanya vibaya kwao katika masomo mengine na hatimaye kuathiri ubora wa elimu kwa ujumla.

Matokeo ya Upimaji Yaonesha Changamoto Kubwa

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Profesa Said Mohamed, matokeo ya Upimaji wa Taifa wa KKK kwa darasa la pili mwaka 2023 yalionesha kuwa asilimia 78.92 ya wanafunzi waliofanya upimaji walifanya vizuri katika kusoma, asilimia 69.6 kuandika na asilimia 62.56 kuhesabu.

Takwimu hizo zinamaanisha kuwa asilimia 21.08 ya wanafunzi wa hatua hiyo ya awali ya elimu ya msingi hawajui kusoma, asilimia 30.4 hawajui kuandika na asilimia 37.44 hawajui kuhesabu.

Sababu za Kuandaliwa kwa Mkakati

Kwa mujibu wa waraka wa mkakati huo, sababu zilizochochea kuandaliwa kwake ni pamoja na umahiri mdogo wa walimu katika matumizi ya mbinu shirikishi za ufundishaji, tathmini endelevu na ufundishaji unaozingatia viwango halisi vya wanafunzi.

Aidha, matumizi hafifu ya zana na vifaa vya kufundishia yamebainika kuwa tatizo, licha ya kuwepo kwa miongozo na mazingira yanayoweza kutumika kuboresha ujifunzaji.

Sababu nyingine ni upungufu wa walimu wa darasa la awali, darasa la kwanza na la pili, msongamano mkubwa wa wanafunzi darasani, pamoja na mifumo ya tathmini inayojikita zaidi katika kuangalia uandikishaji na mahudhurio kuliko kupima umahiri halisi wa stadi za KKK.

Vilevile, mkakati umebainisha matumizi duni ya takwimu katika kupanga na kufanya maamuzi ya kielimu kuanzia ngazi ya shule hadi taifa.

Mbali na hayo, uratibu dhaifu wa utekelezaji wa afua za KKK kati ya ngazi ya Taifa, Mkoa, Halmashauri, Kata na Shule, pamoja na walimu kutokuwa na utaalamu wa kubainisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu ya ujifunzaji, umetajwa kuwa miongoni mwa changamoto sugu.

Maoni ya Wataalamu

Mtaalamu wa masuala ya elimu, Profesa George Kahangwa, amesema kuandaliwa kwa mkakati huo ni hatua muhimu na ya lazima kwa sasa kutokana na ukubwa wa tatizo la watoto wasiokuwa na stadi za KKK.

"Kuna kundi kubwa la watoto wasiokuwa na stadi za KKK. Kundi hili halijumuishi waliopo shuleni pekee, bali pia walioko nje ya mfumo wa elimu na hata wale waliokwisha hitimu, lakini hawakumudu stadi hizi za msingi," amesema Profesa Kahangwa.

Hata hivyo, pamoja na kuunga mkono uwepo wa mkakati huo, Profesa Kahangwa ametoa tahadhari kuwa bila usimamizi madhubuti na utekelezaji wenye kuleta matokeo, mkakati huo unaweza kuwa ni marudio ya juhudi nyingi zilizofanyika awali bila mafanikio ya kudumu.

"Suala la KKK si jipya. Zimekuwepo jitihada na miradi mingi ya kuimarisha stadi hizi, lakini mingi ilikosa uendelevu. Hofu yangu ni kwamba mkakati huu unaweza kuishia kwenye makaratasi. Tunahitaji kuuona ukitekelezwa na matokeo yake yaonekane," amesema.

Kwa mtazamo wake, changamoto kubwa ya miradi iliyopita ni kutegemea fedha za wafadhili, hali iliyosababisha utekelezaji wake kufanyika katika maeneo machache ya nchi na kushindwa kuendelea baada ya ufadhili kuisha.

"Tunapotaka kutekeleza mkakati huu, ni lazima tujifunze kutokana na makosa ya nyuma. Ni lazima tujiulize, ni vikwazo gani vilisababisha miradi iliyopita ishindwe?" amehoji.

Changamoto ya Mazingira ya Kujifunzia

Akizungumzia changamoto ya mazingira ya kujifunzia, Profesa Kahangwa amesema msongamano wa wanafunzi darasani na uhaba wa walimu ni kikwazo kikubwa katika kufundisha stadi za KKK, hususan kwa watoto wa awali hadi darasa la pili.

"Kumfundisha mtoto kusoma au kuandika kunahitaji mwalimu amfikie kwa ukaribu. Sasa kama ana wanafunzi zaidi ya 100 darasani, atawezaje kuwafikia? Ikumbukwe pia watoto wa umri huu wana uwezo wa kuzingatia somo kwa dakika zisizozidi 30. Ndani ya muda huo, mwalimu atawezaje kuwafikia wote?" amehoji Profesa Kahangwa.

Kwa upande wake, mhadhiri wa elimu, Dk Restituta Mushi, amesema uwepo wa mkakati huo ni muhimu, lakini akaonya kuwa haupaswi kuangaliwa kama suluhisho la haraka la changamoto za muda mrefu, akibainisha kuwa tatizo la KKK linaanzia kwenye maandalizi ya walimu kabla ya kuajiriwa.

"Walimu wengi wanaingia madarasani wakiwa hawajapata mafunzo ya kutosha ya kufundisha stadi za awali kwa vitendo. Kama mkakati huu haujaweka mkazo mkubwa kwenye kubadili mfumo wa mafunzo ya walimu vyuoni na vyuo vya ualimu, basi utakuwa unatibu dalili, si ugonjwa," amesema.

Ameongeza mkakati unapaswa kuambatana na marekebisho ya mitaala ya elimu ya ualimu ili kuhakikisha walimu wanahitimu wakiwa na ujuzi wa vitendo wa kufundisha kusoma, kuandika na kuhesabu, badala ya nadharia pekee.

Haja ya Uwajibikaji

Mchambuzi wa sera za elimu na masuala ya maendeleo ya watoto, Deus Mmanda, amesema mkakati wa KKK ni muhimu kwa sasa, lakini utekelezaji wake unaweza kukwamishwa na mifumo dhaifu ya uwajibikaji.

"Tumezoea kuwa na mikakati mizuri kitaifa, lakini changamoto inakuja kwenye ngazi ya halmashauri na shule. Nani atawajibika kama watoto bado wanafika darasa la tatu bila stadi za KKK? Je, kuna mifumo ya kuwawajibisha wakuu wa shule, walimu wakuu na maafisa elimu?" amehoji.

Amesisitiza bila kuwepo viashiria vya wazi vya kupima mafanikio ya mkakati na uwajibikaji kwa kila ngazi, kuna hatari ya mkakati huo kutekelezwa kwa mazoea bila kuleta matokeo yanayotarajiwa.

Mwelekeo wa Rais Samia

Hoja ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mkakati huo iliwekewa msisitizo na Rais Samia Suluhu Hassan wakati anauzindua, akitaka usiishie kwenye karatasi bali ubebe matokeo yatakayopimika na manufaa kwa walengwa na Taifa kwa ujumla.

Alielekeza kuwe na ufuatiliaji wa matokeo ya utekelezaji wa mkakati huo kuwa sehemu ya uwajibikaji katika ngazi zote, kuanzia mwalimu, mkuu wa shule, afisa elimu wa wilaya hadi mkoa.

"Kusiwe na ripoti za kuandika tu. Tunataka mabadiliko yaonekane kwa mtoto. Tunapotembelea sehemu, tukisimamisha mtoto wa darasa la pili akijiandaa kwenda darasa la tatu, tuhakikishe amesoma, ameandika na ameweza kuhesabu kwa jinsi ilivyopangwa," alisema Rais Samia.

Jukumu la Wazazi na Jamii

Mtafiti wa elimu ya awali na maendeleo ya mtoto, Anna Ishengoma, amesema mkakati wa KKK hauwezi kufanikiwa iwapo utajikita zaidi shuleni na kuwaacha wazazi na jamii pembeni.

"Stadi za kusoma na kuandika hazianzi darasani pekee. Mtoto anapoishi katika mazingira ambayo hakuna vitabu, hakuna mawasiliano ya lugha yenye kuchochea fikra, hata mwalimu akijitahidi sana matokeo yatakuwa hafifu," amesema.

Ameongeza kuwa mkakati unapaswa kuwa jumuishi zaidi kwa kuwekeza katika programu za uhamasishaji wa wazazi, hasa katika jamii zenye mwamko mdogo kuhusu umuhimu wa elimu ya awali.

Changamoto ya Lugha

Naye mtaalamu wa lugha na elimu, Mussa Kadeghe, amesema changamoto kubwa ya mkakati wa KKK ipo kwenye lugha ya kufundishia, akieleza kuwa watoto wengi wanakumbana na ugumu wa kujifunza stadi za awali kwa lugha wasiyoitumia nyumbani.

"Kama hatutaangalia kwa kina suala la lugha ya kufundishia katika madarasa ya awali, tutakuwa tunajirudia. Mtoto anahitaji kwanza kuelewa lugha, ndipo ajifunze kusoma na kuandika. Hili ni eneo nyeti ambalo mkakati unapaswa kulishughulikia kwa ujasiri," anasema.

Historia ya Tatizo la KKK

Mwaka 2012 ilibainika kuwa wanafunzi 5,200 waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huo, hawajui kusoma wala kuandika.

Wanafunzi hao walibainika kutojua kusoma wala kuandika baada ya kupewa majaribio ya kupima uwezo wao wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) baada ya kuripoti shuleni kama ilivyoagizwa na Serikali.

Desemba 14, mwaka 2011, wakati akitangaza matokeo ya Mitihani ya Darasa la Saba, aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, aliagiza wanafunzi wote watakaoingia kidato cha kwanza mwaka huo wapimwe kwanza uwezo wao wa kusoma na kuandika.

Ripoti ya taasisi ya Uwezo ya mwaka 2015 ilionesha kuwa asilimia 16 ya watoto wa darasa la saba mwaka 2014 walihitimu bila kuwa na uwezo wa kusoma mafungo ya hadithi rahisi ya Kiswahili ya darasa la pili.

Ripoti hiyo pia ilionesha kuwa asilimia 23 ya wanafunzi waliohitimu darasa la saba hawakuwa na uwezo wa kufanya hesabu rahisi za kiwango cha darasa la pili.

Machi 1, 2018, kulikuwa na taarifa kuhusu uwepo wa watoto waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wakiwa hawajui kusoma wala kuandika, huku Shule ya Msingi Kambala ikiwa miongoni mwa shule zilizolalamikiwa na wananchi kwa kufaulisha wanafunzi wasiojua kusoma wala kuandika.

Uchunguzi ulifanyika kwa mtoto mmoja kati ya waliotajwa kufaulu wakiwa hawamudu stadi za KKK na kukiri pasipo shaka kwamba hajui kuandika au kusoma, hata alipotakiwa kuandika majina yake au kusoma mahali palipoandikwa jina la kijiji anapoishi na wazazi wake (Kambala), alishindwa.

Tags: kinzaniKutekelezwamawazomkakatiukianza
TNC

TNC

Next Post

Private sector urged to boost Tanzania's global tourism

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Popular News

  • Zanzibar’s Leadership Advocates for Streamlined Tax System to Enhance Economic Growth

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanaohujumu miundombinu watachukuliwa hatua kali

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanaohujumu miundombinu watachukuliwa hatua kali

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wasiwasi juu ya Uchochezi wa Makada katika Jimbo la Katavi

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanawake Wanaonyonyesha Washauriwa Kula Milo Mitano Siku

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Category

  • English
  • Swahili

Socials

Instagram TikTok YouTube Facebook

About Us

TNC (Tanzania News Company) is the primary Source of News in English & Swahili in Tanzania

© 2025 TNC - Tanzania News Company

Welcome Back!

Login to your account below

Forgotten Password?

Retrieve your password

Please enter your username or email address to reset your password.

Log In
No Result
View All Result
  • Home

© 2025 TNC - Tanzania News Company