Msiba Moshi: Baba Anadaiwa Kumuua Mwanawe kwa Madai ya Pombe
Moshi – Tukio la kusikitisha limetokea Uru Shimbwe mkoani Kilimanjaro baada ya baba mmoja kudaiwa kumuua mwanawe mwenyewe kwa sababu ya ugomvi uliohusu pombe.
Laurian Teti, mkazi wa eneo hilo, anadaiwa kumuua kijana wake Mathias Teti (26) usiku wa Januari 21, 2026 nyumbani kwao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amethibitisha tukio hilo akisema wanamshikilia baba huyo kwa kosa la mauaji.
"Tukio hili limetokea Januari 21, 2026 saa 10 alfajiri katika Kijiji cha Shimbwe Chini, Kata ya Uru Shimbwe, Wilaya ya Moshi baada ya kutokea ugomvi kati yake na mtoto wake huyo," amesema Kamanda Maigwa.
Chanzo cha ugomvi uliozua kifo hicho ni baada ya kijana huyo kuanza kumdai baba yake ampe pombe iliyonunuliwa kwa ajili ya maandalizi ya kikao cha posa ya dada yake.
Kamanda Maigwa ameeleza kuwa taratibu za kiuchunguzi na upelelezi zinaendelea ili hatua zaidi za kisheria zifuate.