Watu Sita Wakamatwa kwa Mauaji ya Waendesha Bodaboda Tabora
Tabora – Polisi mkoani Tabora wamekamatwa watu sita kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya waendesha bodaboda, ikiwemo kesi ya Hamisi Nchambi maarufu kwa jina la Ngosha ambaye mwili wake ulitelekeza juu ya kaburi.
Operesheni hiyo imefanywa na Jeshi la Polisi mkoani Tabora baada ya kuongezeka kwa matukio ya mauaji dhidi ya waendesha bodaboda.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Costantine Mbogambi, amethibitisha kuwa watuhumiwa wote sita wamekiri kuhusika na mauaji ya bodaboda katika mahojiano ya awali.
Mbogambi amesema mahojiano ya kina yanaendelea ili kubaini matukio mengine na kufikia mnyororo mzima wa uhalifu kabla ya kuwapeleka watuhumiwa mahakamani.
Operesheni Zaongoza Kukamatwa kwa Wahalifu Wengine
Katika operesheni iliyofanyika katika wilaya za Uyui, Nzega, Urambo na Kaliua, watuhumiwa wanne wamekamatwa wakiwa na vifaa vilivyoibiwa kutoka mradi wa Ziwa Victoria. Vifaa hivyo ni pamoja na mashine tatu, vikatia chuma viwili, nyaya mbili za grender na hydrolic lita 40.
Mbogambi amesema vifaa hivyo viliibwa na kufichwa katika vitongoji vya Ubalani na Majengo wilayani Urambo.
Katika tukio tofauti, polisi wamekamatwa watu watano kwa tuhuma za wizi wa pikipiki tisa zilizoportwa katika wilaya ya Nzega mkoani Tabora na Kahama mkoani Shinyanga. Watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani hivi karibuni.
Maandamano ya Waendesha Bodaboda
Kufuatia matukio haya, waendesha bodaboda mkoani Tabora wameandamana kwa amani hadi ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakitaka kufahamu ni lini mauaji hayo yatakomeshwa kabisa.
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, amethibitisha kuwa vyombo vya ulinzi vinaendelea na operesheni za kuhakikisha usalama wa wananchi wote.
"Sisi tupo kwa ajili ya kuhakikisha mnaishi salama mkiendelea na majukumu yenu. Ikitokea mtu anavunja sheria lazima tuchukue hatua kali kwa mujibu wa sheria," alisema Wella.
Kamanda Mbogambi ameahidi kuwa Jeshi la Polisi linafanya kazi usiku na mchana kukomesha vitendo vyote vya kihalifu mkoani Tabora na kuchukua hatua kali dhidi ya wahalifu.
"Haiwezekani watu wachache wasumbue watu hapa, waue wenzao na kuchukua pikipiki. Hatuwezi kuvumilia watu wa sampuli hii," alisema Mbogambi.