Rais Dk Hussein Mwinyi Awasamehe Wafungwa 17 Katika Sherehe za Mapinduzi
Unguja – Katika maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, amewaachia huru wafungwa 17 waliokuwa wakitumikia adhabu zao mbalimbali gerezani.
Uamuzi huo umechukuliwa kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 59 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, ambacho kinampa Rais mamlaka ya kutoa msamaha kwa mtu yeyote aliyehukumiwa kwa kosa lolote.
Kati ya wafungwa 17 waliosamehewa, wafungwa 11 ni kutoka Unguja na sita ni kutoka Pemba.
Taarifa rasmi iliyotolewa Januari 11, 2026, na kusainiwa na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Raqey Mohamed, imeeleza kwamba hatua hii ni utaratibu wa kawaida ambao Rais hufanya wakati wa maadhimisho ya kitaifa.
Mapinduzi ya Zanzibar yalitokea tarehe 12 Januari 1964, na yalilenga kuondoa utawala wa kikoloni na kuweka mamlaka mikononi mwa Waafrika.