Umoja wa Mataifa Washitushwa na Hali Mbaya ya Kibinadamu El-Fasher, Kilo ya Mchele Sh243,700
Darfur – Umoja wa Mataifa imeshtushwa na hali kibinadamu iliyoshuhudia katika ziara yake iliyofanyika mji wa El-Fasher uliopo Darfur Magharibi nchini Sudan huku kilo moja ya mchele ikiuzwa Sh243,700 (Dola 100).
Ziara hiyo iliyofanyika jana Jumatano, Disemba 31, 2025 tangu mji huo uchukuliwe na kikosi cha kijeshi cha Rapid Support Forces mwezi Oktoba, imeonyesha maisha magumu yanayowakabili raia hao.
Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Denise Brown, amesema kuwa ujumbe huo uliodumu kwa saa kadhaa ulifanyika katika mazingira ya msongo mkubwa wa hofu.
"Ilikuwa ziara yenye taharuki kubwa, kwa sababu tumeingia katika eneo lisilojulikana, ambalo Umoja wa Mataifa umekuwa ukilielezea kama la uhalifu," amesema, akibainisha kuwa ziara hiyo ilifanyika muda mfupi baada ya kuuawa kwa walinda amani katika mji wa karibu wa Kadugli.
Brown amesema kuwa wakati wa ziara hiyo, waliona idadi ndogo ya raia, ingawa Umoja wa Mataifa unaamini kuwa wengine wengi bado wanashikiliwa au wamejeruhiwa na wanahitaji kuhamishwa haraka kwa ajili ya matibabu.
Vijiji vinavyozunguka El-Fasher vimeonekana kutelekezwa, huku wale waliobaki mjini wakiishi katika majengo yaliyoharibiwa au vibanda vya muda bila maji safi, vyoo au chakula cha kutosha.
Umoja wa Mataifa unasema mamia ya raia bado wapo katika eneo hilo, wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa dawa, elimu na mahitaji ya msingi. Bei ya chakula imepanda, ambapo kilo moja ya mchele inaripotiwa kuuzwa hadi Dola 100.
Brown ameonya kuwa hali hiyo inaakisi tabia inayoonekana kuzoeleka ya ukatili Darfur unaoendelea katika vita vya Sudan na kusisitiza kuwa tathmini zaidi za Umoja wa Mataifa pamoja na upatikanaji wa msaada wa kibinadamu unahitajika kwa dharura.