Rais Mwinyi Awatakia Watanzania Heri ya Mwaka Mpya 2026
Unguja – Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, amewatakia Watanzania heri ya Mwaka mpya 2026, akiwataka kuendelea kudumisha amani, mshikamano na umoja wa kitaifa ili kuharakisha maendeleo ya nchi.
Katika salamu zake za Mwaka mpya, Rais Dk Mwinyi amesema mwaka 2025 umeacha alama ya mafanikio makubwa katika utekelezaji wa mipango na miradi ya maendeleo iliyoandaliwa na Serikali, hususan katika sekta za miundombinu, afya, elimu, utalii, nishati na uchumi wa buluu.
Dk Mwinyi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wananchi, pamoja na dhamira ya dhati ya uongozi katika kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa ufanisi na tija kwa manufaa ya wananchi.
Wito wa Kudumisha Amani na Umoja
Akizungumza katika hotuba ya kuukaribisha Mwaka mpya aliyoitoa saa 6:00 usiku, Januari mosi, 2026, Rais Mwinyi amewasihi wananchi kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano, akisisitiza kuwa misingi hiyo ni nguzo muhimu ya kuharakisha maendeleo ya nchi.
Amesema hadi kufikia mwisho wa mwaka 2025, Serikali ina kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa hatua kubwa za maendeleo zilizopatikana kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati katika sekta tofauti, zikiwemo utalii, ujenzi wa miundombinu, huduma za jamii kama elimu, afya, maji safi na salama, pamoja na michezo.
Malengo ya Mwaka 2026
Akieleza malengo ya Serikali kwa mwaka 2026, Dk Mwinyi amesema Serikali inalenga kuyaendeleza na kuyaboresha mafanikio yaliyopatikana kwa kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 7.1, kuongeza mapato ya Serikali na kuimarisha shughuli za kiuchumi, ikiwemo biashara, viwanda na uwekezaji.
Amebainisha kuwa sekta ya utalii itaendelea kupewa kipaumbele ili kuongeza mapato ya fedha za kigeni, sambamba na kuimarisha miundombinu ya barabara, bandari na viwanja vya ndege, kufungua masoko mapya na kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Katika sekta za elimu na afya, amesema Serikali itaongeza jitihada za kuboresha miundombinu kwa kujenga shule za ghorofa, mabweni na kuendelea na ujenzi wa hospitali za mikoa, Hospitali ya Mnazi Mmoja, hospitali za rufaa na kufundishia, pamoja na Kituo cha Tiba za Saratani Binguni.
Amewahimiza wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali katika utekelezaji wa mipango yote ya maendeleo kwa kushirikiana, kudumisha amani na mshikamano kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mafanikio ya Kiuchumi
Akizungumzia mafanikio ya kiuchumi, amesema juhudi za Serikali zimewezesha uchumi wa Zanzibar kukua kwa wastani wa asilimia 7.1, huku pato la Taifa kwa bei ya soko likiongezeka kutoka Sh4.78 trilioni mwaka 2021 hadi Sh6.57 trilioni mwaka 2024.
Aidha, ukusanyaji wa mapato umeongezeka kutoka Sh856 bilioni mwaka wa fedha 2020/21 hadi Sh2.104 trilioni mwaka 2024, huku mfumuko wa bei ukidhibitiwa na kubaki katika tarakimu moja ya asilimia tano.
Kwa upande wa uwekezaji, amesema hadi Desemba 2025, miradi 1,657 yenye mtaji wa Dola bilioni 20.206 za Marekani imesajiliwa na Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (Zipa), ikitarajiwa kutoa ajira zaidi ya 87,669 katika sekta za utalii, viwanda, nyumba za biashara na nyinginezo.
Ameongeza kuwa sekta ya utalii imeendelea kufanya vizuri, ambapo watalii 816,438 waliingia Zanzibar kati ya Januari na Novemba 2025, sawa na ongezeko la asilimia 27 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2024.
Maendeleo ya Miundombinu
Katika miundombinu ya barabara, amesema Serikali imekamilisha ujenzi wa kilometa 82.887 za barabara za mijini na kilometa 247 za barabara za vijijini kwa kiwango cha lami na zege, huku ujenzi wa madaraja ya juu na ya kawaida ukiendelea katika maeneo mbalimbali, hatua inayotarajiwa kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi.
Akigusia huduma za jamii, amesema uwekezaji mkubwa umefanywa katika sekta ya afya kwa kuongeza bajeti, kuajiri watumishi na kuboresha miundombinu, hali iliyoimarisha huduma za rufaa na ubora wa huduma katika hospitali zote za wilaya.
Katika elimu, bajeti imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 200, shule mpya za ghorofa zimejengwa, walimu wameajiriwa na mikopo ya elimu ya juu imeongezwa, hatua zilizoboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
Uwezeshaji wa Wananchi
Kwa lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi, amesema Serikali imetoa mikopo isiyo na riba yenye thamani ya zaidi ya Sh50 bilioni kwa wananchi zaidi ya 27,000, wakiwemo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Aidha, mafanikio yamepatikana katika sekta ya michezo kupitia ujenzi wa viwanja vya kisasa na kuendeleza vipaji vya vijana.
Dk Mwinyi amekumbusha kuwa mwaka 2026 ni wa maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, akiwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika shamrashamra zitakazoambatana na uzinduzi wa miradi ya maendeleo, matamasha na michezo kama ishara ya kuthamini Mapinduzi na mchango wake katika maendeleo ya Zanzibar na Taifa kwa ujumla.