Ukuaji wa Uchumi wa Dunia 2025: Sudan Kusini Yaongoza, Tanzania Nafasi ya 23
Dar es Salaam. Mwaka 2025 umeendelea kuwa kipindi muhimu katika historia ya uchumi wa dunia, ambapo mataifa mengi yameshuhudia ukuasi wa pato la taifa kutokana na mabadiliko ya kimkakati katika sera za kiuchumi, teknolojia, na biashara ya kimataifa.
Baada ya changamoto za miaka iliyopita kama vile misukosuko ya kiuchumi, mabadiliko ya tabianchi, na athari za majanga ya kiafya, nchi mbalimbali zimechukua hatua madhubuti kufufua na kuimarisha uchumi wao.
Uwekezaji katika sekta za uzalishaji, nishati mbadala, miundombinu na teknolojia ya kidijitali umechangia kuongeza ajira na kuboresha mapato ya serikali.
Aidha, ushirikiano wa kikanda na kimataifa umewezesha mataifa kunufaika na masoko mapya na kuongeza mauzo ya nje.
Haya yanashuhudiwa wakati ambao Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) linaeleza kuwa uchumi wa dunia ulikua kwa asilimia 3.2 katika mwaka 2025 ikiwa ni pungufu kutoka asilimia 3.3 mwaka uliotangulia na inatarajiwa kufikia asilimia 3.1 mwaka 2026.
Sudan Kusini Yaongoza Ukuaji wa Uchumi
Wakati hilo likishushudiwa IMF nchi ya Sudan Kusini ndiyo iliyoongoza kwa kushuhudia ukuaji mkubwa wa pato lake la taifa katika mwaka 2025 kuliko mataifa yote duniani ikiwa kwa asilimia 24.3.
Nchi hiyo ilifuatiwa na Libya iliyoshuhudia ukuaji wa asilimia 15.6, Guyana asilimia 10.3, Ireland asilimia 9.1, Kyrgystan asilimia 8.
Mataifa mengine yaliyoshuhudia ukuaji huo ni Tajikistan (asilimia 7.5), Georgia (asilimia 7.2), Ethiopia (asilimia 7.2), Rwanda (asilimia 7.1) na Benin asilimia 7. Wakati huo Tanzania uchumi wake ulikua kwa asilimia 6 huku ikishika nafasi ya 23 duniani ikiwa na ukuaji wa asilimia 6.
Ukuaji mkubwa wa uchumi wa Sudan Kusini ulitajwa kuchochewa na kurejea kwa biashara ya mafuta katika mwaka 2025 ikiwa ni baada ya kusimama kwa muda kutokana na migogoro iliyokuwapo ambayo pia ilichangia kuharibu kwa baadhi ya miundombinu ya kusafirisha mafuta.
Mafuta yanatajwa kuchangia asilimia 90 ya mapato ya serikali katika nchi hiyo wakati ambao wakiendelea na juhudi za kurejesha amani na kutengeneza mazingira ya kisiasa na kiuchumi yanayoweza kuvutia uwekezaji wa ndani na nje.
Hatua hizi ni pamoja na juhudi za kuboresha usimamizi wa mapato ya mafuta na juhudi za kurejesha hali ya kawaida ya biashara ambazo zimechangia kuongeza Imani kwa wawekezaji na sekta binafsi.
Hata hivyo kwa upande wa Ireland, ukuaji wake umetajwa kuchangiwa na uuzaji wa bidhaa za madawa katika masoko ya nje.
Maoni ya Wataalamu wa Uchumi
Akizungumzia suala hilo, Mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Lutengano Mwinuka anasema wakati mwingine viashiria vya ukuaji wa uchumi haumaanishi ukuaji wa maendeleo.
Amesema mara nyingi viashiria hivyo vya ukuaji wa uchumi huonekana zaidi kupitia sekta ambazo zimefanya vizuri kama ilivyo kwa Sudan Kusini kuuza mafuta mengi.
"Inaweza kuwa sekta moja imefanya vizuri zaidi, kama ambavyo Tanzania utalii unafanya vizuri, kadri inavyozidi kukua inaonekana zaidi," anasema.
Hatahivyo, ukuaji wa pato la Taifa haimaanishi moja kwa moja maisha bora kwa wananchi kwa sababu haioneshi usawa wa kipato, ajira zote au ubora wa huduma za kijamii zinazotolewa katika nchi husika.
Mtaalamu mwingine wa uchumi, Profesa Haji Semboje amesema Tanzania iko katika nafasi nzuri ya ukuaji ukilinganisha na Sudan Kusini kwani mara zote nchi zenye uchumi wa chini ukuaji wake huwa unaonekana kuwa mkubwa.
"Nchi zenye uchumi mkubwa ukuaji wake si wa kiwango kikubwa. Ni sawa na kulinganisha tairi ya gari ya IST na zile gari kubwa za migodini. Gari kubwa ya mgodini ni sawa na nchi ya uchumi mkubwa, likizunguka mara mbili linakuwa mbali tofauti na tairi la IST ambalo katika umbali sawa linaweza kuzunguka mara nne na lisifikie kiwango cha gari hilo," anasema.
Anasema namna Sudan kusini inavyotazazwa kwa sasa itakuwa ni tofauti na nchi nyingine ambapo hutumika vigezo mbalimbali ikiwemo kuangalia mfumuko wa bei, kiasi cha fedha kinachopatikana katika uuzaji wa bidhaa nje ya nchi na kiwango cha watu walioajiriwa.
Namna Tanzania Inavyoweza Kuongeza Ukuaji
Akizungumza namna Tanzania inavyoweza kuongeza ukuaji wake wa uchumi, Mtaalamu wa Uchumi Profesa Samwel Wangwe amesema kama nchi inaweza kuhakikisha imeboresha mnyororo wa thamani wa bidhaa inazozalisha na kukumbatia teknolojia.
Amesema nchi kama Ireland kufanya vizuri katika kuuza bidhaa za madawa inaonyesha kwa namna gani wametumia teknolojia kikamilifu na kuweza kufanya uzalishaji wa bidhaa.
"Hata sisi tunaweza kukumbatia teknolojia na kuhakikisha kuwa tunaongeza thamani katika bidhaa zetu, tuache kupeleka nje kahawa ghafi na badala yake tuiongeze thamani ili kupata fedha zaidi," anasema.
Amesema uwekezaji katika viwanda pia ni jambo linalopaswa kuangaliwa kwani kama nchi bado inaaingiza bidhaa nyingi ambazo inaweza kuzalisha ndani ya nchi na kuuza katika masoko ya nje.
"Gesi pia tunayo ya kutosha ni wakati wa kuangalia namna gani tunaifikisha kwenye viwanda vyetu ili itumike kikamilifu na iongezewe thamani kwa ajili ya masoko mengine," amesema.
Umuhimu wa Dira 2050
Katika eneo hili, Profesa Semboja anasema kama nchi inayo nafasi ya kukuza ukuaji wake wa uchumi kwa kiwango kikubwa kinachoweza kupunguza umasikini ikiwa itasimamia kikamilifu utekelezaji wa dira 2050.
"Tutengeneze mkakati wa utekelezaji Dira 2050 si tu kwa kauli zinazozungumzwa bali tufanye kwa vitendo vinavyofungamana," anasema.
Anasema mara zote serikali imekuwa ikianzisha sera nzuri za jumla na zile za kisekta lakini wanaozitekeleza hawapati nafasi ya kuzisoma na kuzielewa kikamilifu jambo litakalofanya waweze kuzizungumzia mbele za watu kwa namna nyepesi.
"Sasa kama dira hii tunataka kutekeleza vizuri kuwe na sauti moja kuanzia Rais hadi wasaidizi wake, kila anayeongea iwe dira 2050 na kila kinachosemwa kama ni kilimo, biashara, elimu iendane na malengo yaliyowekwa kwa miaka 25 ijayo," anasema.
Hilo litafanya watu wasitumie utashi wao wanapozungumzia mambo mbalimbali na kile wanachoona wao kinafaa (fikra) na badala yake kila kitu kilenge utekelezaji wa dira.
"Tofauti na kila kiongozi akiongea anachokitaka dira 2050 itakuwa ni ngumu kuona matokeo yake kama ilivyokusudiwa. Hii ianze na Rais Samia Suluhu Hassan wanaoandaa hotuba zake wahakikishe kila kitu ni utekelezaji dira, sera na mikakati iliyowekewa na serikali," anasema.
Hiyo itawafanya si viongozi tu bali watanzania kuwa na uelewa, kuitambua na kuikubali mipango iliyowekwa na kutambua nafasi yao.
Dira 2050 itakayoanza kutumika mwakani inalenga kutoa mwelekeo wa maendeleo ya taifa kwa karibu miongo mitatu ijayo ina shabaha ya kujenga Uchumi wa kati ngazi ya juu wenye pato la Taifa la dola trilioni moja huku pato la mtu mmoja mmoja likikatarajiwa kufikia dola 7,000 ifikapo 2050.
Sauti ya Wafanyabiashara
Wakati wataalamu wa uchumi wakiyasema hayo, Fredy Mwakyusa ambaye ni mfanyabiashara katika soko la Kariakoo alitaka bidhaa zenye masoko zaidi nje ya nchi kuwekwa wazi ili watanzania wenye uwezo wa kuyafikia masoko wayatumie ipasavyo.
"Tumeambiwa tunauza sana mazao ya kilimo, wananchi waambie mazao gani yana soko sana, watu wajue," alisema.
Matarajio ya 2026
Kwa mujibu wa IMF, katika mwaka 2026 uchumi wa nchi zilizoendelea unakadiriwa kukua kwa wastani wa asilimia 1.5 huku uchumi wa nchi zinazoibukia na zinazoendelea ukitarajiwa kukua kwa kiwango cha zaidi ya asilimia 4.
Wakati huo mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kupungua duniani kote, ingawa kwa viwango vinavyotofautiana kati ya nchi, ukiwa juu ya lengo nchini Marekani pamoja na hatari zinazoelekea kuongezeka na ukiwa wa chini katika nchi nyingine.
Katika upande wa udhaifu wa kifedha wa serikali IMF inaeleza kuwapo kwa uwezekano wa marekebisho makubwa katika masoko ya fedha ambao unaweza kusababisha kudhoofika kwa taasisi na kutishia uthabiti wa kiuchumi.
Kufuatia hali hiyo, IMF inawataka watunga sera kurejesha imani kupitia sera zinazoweza kuaminika, zilizo wazi na endelevu ambazo zitaambatana na diplomasia ya kibiashara.
Hayo yote yanaelezwa wakati ambao inashauriwa kulindwa kwa uhuru wa benki kuu sambamba na kuimarisha upya juhudi za kufanya mageuzi ya kimuundo.
"Katika hili hatua za awali za kuboresha mifumo ya sera zimezisaidia nchi kwa kiasi kikubwa hata hivyo, sera ya viwanda inaweza kuwa na nafasi lakini ni muhimu kuzingatia kikamilifu gharama mbadala na mizania ya faida na hasara inayohusiana na matumizi yake," imeeleza ripoti hiyo.