Rais Mwinyi Afanya Mabadiliko ya Wenyeviti wa Bodi za Mashirika Zanzibar
Unguja – Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amefanya mabadiliko ya wenyeviti wa bodi wa mashirika mbalimbali ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Taarifa rasmi iliyotolewa leo Jumanne Desemba 30, 2025 na Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, imesema uteuzi huo unaanza kutekelezwa leo.
Kulingana na taarifa hiyo, Makame Hasnuu Makame ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO). Kabla ya uteuzi huu, Makame alikuwa akishika nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA).
Kwa upande wake, Sultan Said Suleiman ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA). Hapo awali, Sultan Said alikuwa akishika nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO).
Vilevile, Dk Mwinyi amemteua upya Dk Abdulhamid Yahya Mzee kuendelea kushika nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC).
Mabadiliko haya yamekuja baada ya siku tisa tu tangu Rais Mwinyi ateue wenyeviti wa bodi ya wakurugenzi tarehe Desemba 22, 2025.
Katika uteuzi wa Desemba 22, 2025, Dk Mwinyi aliteua wenyeviti watano ambao kati yao wawili wamefanyiwa mabadiliko haya mapya wakati watatu wamesalia kwenye nafasi zao.
Wenyeviti waliosalia kwenye nafasi zao ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Juma Burhani Mohamed, Dk Maudline Cyrus Castico na Dk Idrissa Muslim Hija.