Thursday, January 15, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Instagram
TNC
  • Home
  • Home
No Result
View All Result
TNC
No Result
View All Result

VIDEO: Maaskofu wakitoa ujumbe wa Krismasi

by TNC
December 26, 2025
in Swahili
0
0
SHARES
2
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Viongozi wa Dini Wasisitiza Unyenyekevu na Amani Katika Sikukuu ya Krismasi

Dar es Salaam/Mikoani. Sikukuu ya Krismasi imetamatika, huku viongozi wa kiroho wakitaka itumike kuwa chachu ya kuzika tofauti na kujenga utayari wa kuanza upya, wakisisitiza kukomeshwa kwa ufisadi, ukatili, ulafi, ibada za uongo, hasira na fitina.

Katika baadhi ya madhabahu, sikukuu hiyo na ile ya Mwaka mpya, viongozi wa makanisa wametaka ziwe mwanzo wa jamii kuthamini uhai na yeyote asifikirie kuutoa wa mwingine, kwa kuwa kufanya hivyo ni kuingilia mamlaka ya Mungu.

Mahubiri ya viongozi hao wa dini katika sikukuu hiyo ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo yalihusisha onyo kwa waliopata nafasi za uongozi, kuhakikisha wanakuwa wanyenyekevu na wazitumie nafasi hizo kuwahudumia waliowawezesha kuzipata.

Hayo yameelezwa leo, Alhamisi, Desemba 25, 2025, na viongozi mbalimbali wa dini ya Kikristo kwa nyakati tofauti, katika mahubiri yao wakati wa ibada ya Sikukuu ya Krismasi.

Ibada ya Kitaifa: Ujumbe wa Unyenyekevu

Katika Ibada ya kitaifa iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kiaskofu la Bikira Maria Mshindani, Kigoma, Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma, Joseph Mlola, amesema Mungu aliichagua Krismasi kuwa siku ya unyenyekevu dhidi ya kiburi, upendo dhidi ya chuki na huduma dhidi ya utawala.

Kuzaliwa kwa Yesu Kristo katika hali duni, amesema, kunawafundisha binadamu kwamba ukuu hupatikana katika unyenyekevu, huruma na kuwahudumia wengine.

"Tulipokee, tulielewe na tuliishi kwamba tunapotafuta nafasi mbalimbali kwenye jamii, tukumbuke huduma, Yesu amekuja kwetu kwa ajili ya kuhudumia na siyo kuhudumiwa," amesema.

Msisitizo wa Askofu Mlola ni kile alichoeleza kuwa ni muhimu kila mtu awe mnyenyekevu, awe na huruma na aweke kipaumbele kuwahudumia wale waliompa nafasi aliyonayo.

"Kazi ya mfalme ni kutawala na kuongoza. Kristo amekuja kutawala maisha yetu na kutuongoza kwa Mungu. Amekuja kuanzisha utawala wa Mungu duniani wa haki, amani, umoja na upendo," amesema.

Ameeleza ni vigumu binadamu kuishi kumfikia Yesu, lakini angalau somo la unyenyekevu wake linawaalika watu kufanya jambo fulani.

"Mara ngapi tukiwa katika hali zetu za kawaida tunakimbizana na majukumu katika maeneo yetu, kwa nini tunapopata nafasi fulani tunaanza kupandisha mabega, tunaanza kuona hata tuliokuwa nao pamoja kwamba hatuwafahamu tena?" amesema.

Ameeleza ni muhimu kujifunza unyenyekevu, vyeo na nafasi zisiwe sababu za kung’ang’ania kwa nguvu, bali kujishusha ili kuwafikia wale wanaopaswa kuhudumiwa.

"Si kuanza kudharau, kuona kwamba wale ni duni na wewe ulikuwa humo. Waswahili wanasema, mpanda ngazi hushuka," amesema Askofu Mlola.

Thamani ya Uhai

Askofu Mlola amesema Mungu anafundisha kutambua thamani ya uhai, hivyo yeyote asifikirie kuutoa uhai wa mwingine kwa kuwa kufanya hivyo ni kuingilia mamlaka yasiyo yake.

"Mtu yeyote asiote ndoto, iwe ya mchana au usiku, katika maisha yake au kufikiria tu kuutoa uhai wa mwenzake au hata uhai wake mwenyewe, ambao kimsingi si wake bali ni mali ya Mungu.

"Mwenye mamlaka ya uhai huo yupo, tusijitwalie jukumu lisilotuhusu, tuwe na hofu ya Mungu maishani mwetu. Uhai wa mtu unaanza tangu pale kutungwa mimba mpaka pale Mungu atakapoamua kuutoa."

Amesema kufikiri na kutenda kinyume na ukweli huo ni kukosa hekima inayotaka kuchagua yaliyo mema na kuacha mabaya ya uovu.

Kuzaliwa kwa Yesu, amesema, kutukumbushe wajibu wa kila mmoja kulinda uhai na haki ya kila mmoja kuishi.

Kuzika Tofauti na Kuanza Upya

Katika mahubiri yake hayo, Askofu Mlola amesema ni muhimu kuwa tayari kuanza upya katika maisha na daima tusikubali kubaki sehemu moja, kwani binadamu anapaswa kubadilika.

"Kama tulikuwa na mahusiano mabaya, hatuelewani, tuanze maisha mapya, kama tulikuwa na tabia mbaya, tuanze upya. Krismasi ni mwanzo mpya. Kuzaliwa kwake Yesu Kristo ni mwanzo mpya wa maisha," amesema.

Ametaka watu kuwa tayari kuzika tofauti kwa kuhakikisha visababishi vya kutofanana na Mungu vinang’olewa, ikiwemo ukatili, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada za uongo, uchawi, hasira, fitina, uzushi, husuda, ulevi na ulafi.

Ameitaka jamii kushikamana na masuala ya kiroho yatakayoipeleka katika uzima, upendo, haki, amani, uvumilivu, furaha, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi.

Ujumbe wa Amani

Ametumia madhabahu hiyo pia kueleza ujumbe wa amani unaoihusu dunia nzima na kwamba inampasa binadamu kueneza amani kuanzia katika nafsi yake, familia, Taifa na ulimwengu kwa ujumla.

"Lakini daima ianzie kwetu, mtu mmoja mmoja, na kila mmoja ajitahidi kuwa chombo cha amani ya Mungu. Yesu ni Mfalme wa amani, alikuja kuleta amani na haki pale ambapo haikuwepo, ni sisi tunapaswa kujitahidi iwepo," amesema.

KKKT: Amani Inatawale Tanzania

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa, amesema Kristo amewataka waumini waishi kwa kudumisha amani hata kama watu watabeza hilo, ndiyo hitaji na dai lake.

Amesema hata malaika na jeshi la mbinguni walitangaza kwa kupaza sauti: "Atukuzwe Mungu juu mbinguni na amani duniani kwa watu wote."

"Najua kama Taifa tumepitia katika kipindi kigumu, ambacho sina hakika kwa wale wanaonizidi umri kama wamewahi kupita kipindi kigumu kama hiki, hakuna hatujui kwa nini," amesema Askofu Malasusa.

Amesema watu wa kiroho wamekuwa wakijiuliza kwa nini Mungu ameruhusu mambo hayo kutokee, akisema tafsiri ni nyingi, lakini mojawapo ni Mungu kutaka kuonesha umuhimu na thamani ya amani.

"Ndugu zangu, ni vigumu sana kupata maneno yanayoweza kuelezea umuhimu wa amani, ni vigumu sana, lakini itoshe tu kuwa Mungu wa Krismasi na huyu Yesu anayezaliwa, yeye ambaye ni Mfalme wa amani, atawale kwanza katika mioyo yetu," amesema Askofu Malasusa.

Onyo kwa Viongozi Wanaong’ang’ania Madaraka

Mchungaji wa Kanisa Anglikana Mtakatifu Marko Sofu, mkoani Pwani, Rogers Mshuza, amewaonya viongozi wanaopenda kung’ang’ania madaraka kuacha tabia hiyo akisema inaleta chuki, migawanyiko na machafuko katika jamii na duniani kwa ujumla.

Amesema kila uongozi una ukomo wake na haupaswi kuchukuliwa kama wa milele, akiwataka kutambua madaraka ni dhamana ya muda iliyowekwa na Mungu, si mali binafsi ya mwanadamu.

Wazazi Watahadharishwa: Kumbukeni Wajibu wa Januari

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Godson Mollel, amewataka wazazi na walezi kutumia sikukuu za mwisho wa mwaka vizuri huku wakitambua kuwa Januari wana wajibu wa kupeleka watoto shule.

"Tunaomba Mungu leo iwe siku ya amani katika familia, kweli ikawe amani. Leo ni siku hata ya kubadilisha mlo, jamani tukale kwa furaha, leo siyo siku ya ujinga, ni siku ya kufurahi na familia. Na tunapokula, tukumbuke Januari shule, tule kwa akili tuwapeleke watoto shule," amesema.

Acheni Siasa za Udini

Askofu wa Kanisa Anglikana, Dayosisi ya Tabora, Elias Chakupewa, amesisitiza kuachwa tabia ya kufanya siasa za udini kwani zinachochea migogoro miongoni mwa madhehebu na jamii.

"Acheni kabisa mambo ya kuingiza udini kwenye siasa, kwani inachochea migogoro miongoni mwetu, hii sio asili ya Tanzania kuwa na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe kwani tumezoea amani, upendo na mshikamano," amesema.

Amesema sikukuu hii ikawe ni sababu ya kudumisha heshima ya madhehebu ya dini na kuacha kugeuza majukwaa ya dini kurushiana maneno yanayoshusha heshima ya dini nyingine au utu wa mtu, kwani sio desturi na mila za Watanzania.

Watanzania Hawashabikii Haki

Kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Askofu wa jimbo hilo, Juda Ruwa’ichi amesema Watanzania wengi hawashabikii haki wala sio wadau wa haki.

Amesema wengi wao kwa ujinga, kwa kurubuniwa au vinginevyo wamekuwa wadau wa amani akiweka msisitizo kuwa pasipo na haki hakuna amani.

"Sisi tunaoadhimisha Krismasi, kuzaliwa kwa mwokozi tunatakiwa kuwa watu wa haki, wewe mwana Dar es Salaam, Mtanzania je wewe ni mtu wa haki…? Wewe ni mdau wa haki? Naomba kuthubutu kusema kwamba Watanzania wengi hawashabikii haki sio wadau wa haki, Watanzania wengi kwa ujinga au kutokujua wanajiadai wadau wa amani," amesisitiza.

"Ewe Mtanzania kama utaka kujigamba kuwa mtu wa amani jitose kupigania haki, jitose kusema kweli, amani na yanayompendeza Mungu," amesema.

Kanisa Haliwezi Kunyamaza

Katika Parokia ya Mtakatifu Petro, Oysterbay, jijini Dar es Salaam, Paroko wa Parokia hiyo, Batholomew Mroso, amesema kudai haki na kukataa uovu si chaguo la kanisa bali ni kutimiza msingi wake wa kiimani.

Ameeleza kuzaliwa kwa Yesu Kristo ni tukio la kipekee lililodhihirisha upendo na ukombozi wa Mungu kwa mwanadamu.

"Nafasi yetu ndani ya Mungu ni kubwa, hivyo lazima tujiulize sisi ni kina nani na kusudi letu ni nini," amesema, akihimiza waumini wasiwe waoga bali wasimame imara kutetea haki na kukataa uovu.

Padri Mroso amesema Kanisa linapopinga adhabu ya kuua watu hata wenye makosa, linajikita katika misingi ya Kristo aliyezaliwa ili kuleta ukombozi na heshima kwa utu wa mwanadamu.

"Kanisa linapotetea haki kwa kukataa watu kunyongwa, hata kama wana makosa, ni katika misingi hiyo ya Kristo aliyezaliwa kama mwanadamu ili atuletee uhuru na haki," amesema.

Kuhusu mwaka 2025, amesema umekuwa na matukio mengi yasiyopendeza, hivyo 2026 unapaswa kupita na mambo yake yote mabaya yasahaulike na kuanza ukurasa mpya.

"Ninaamini kila mmoja anatamani huu mwaka upite upesi, ndiyo upite haraka na mambo yake yote," amesema.

Tags: KrismasiMaaskofuUjumbeVIDEOwakitoa
TNC

TNC

Next Post

Waliojeruhiwa katika ajali ya kanisa waeleza kilichotokea

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Popular News

  • Zanzibar’s Leadership Advocates for Streamlined Tax System to Enhance Economic Growth

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanaohujumu miundombinu watachukuliwa hatua kali

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanaohujumu miundombinu watachukuliwa hatua kali

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wasiwasi juu ya Uchochezi wa Makada katika Jimbo la Katavi

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanawake Wanaonyonyesha Washauriwa Kula Milo Mitano Siku

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Category

  • English
  • Swahili

Socials

Instagram TikTok YouTube Facebook

About Us

TNC (Tanzania News Company) is the primary Source of News in English & Swahili in Tanzania

© 2025 TNC - Tanzania News Company

Welcome Back!

Login to your account below

Forgotten Password?

Retrieve your password

Please enter your username or email address to reset your password.

Log In
No Result
View All Result
  • Home

© 2025 TNC - Tanzania News Company