Mtoto Mzama Shimoni Afariki Tabora, Wengine Watatu Waokolewa
Tabora – Msiba umeikumba familia moja katika mtaa wa Kizigo, kata ya Ng’ambo, Manispaa ya Tabora baada ya mtoto wao mwenye umri wa miaka mitatu, Samir Adam, kufariki dunia baada ya kuzama kwenye shimo lililojaa maji. Tukio hilo limetokea wakati mkoa huo unakabiliwa na mvua kubwa iliyonyesha kwa zaidi ya saa nne, ikisababisha watu wengine watatu kusombwa na maji.
Akizungumza leo Desemba 25, 2024, baba mzazi wa mtoto huyo amesimuliya kuwa alipokuwa amelala, mama yake alimwita na kumpa taarifa kuwa mwanaye ametumbukia kwenye shimo. Baada ya kuharakisha kwenye eneo la tukio, alikuta mwanaye ameshazama kwenye maji.
"Nimerudi nyumbani nimechoka nikaamua kupumzika muda mfupi tu. Mama angu aliniita na kuniambia mtoto amezama kwenye shimo. Nimejitahidi kumuokoa mwanangu lakini amefariki tayari. Naumia sana," amesimuliya baba mzazi kwa uchungu.
Ester John, jirani wa familia hiyo, amesema alisikia jirani yake analia kwa sauti kubwa. Baada ya kuuliza, alipata taarifa ya kifo cha mtoto huyo.
"Nimeumia sana kwa sababu Samir ni kajukuu ketu hapa. Tunacheza nako kila wakati. Ni katoto kazuri, kana nidhamu na kachangamfu sana. Yaani mimi kama bibi nimepata maumivu mengi," amesema jirani.
Hatua Kali Dhidi ya Wanaoacha Mashimo Wazi
Mwenyekiti wa mtaa wa Kizigo, kata ya Ng’ambo, Grayson Samwel, ametangaza hatua kali dhidi ya wale wote wanaoacha mashimo hatarishi. Amesema angaliso lilishatolewa hapo awali, lakini baadhi ya watu wamekaidi na kuendelea kusababisha maafa.
"Hapa tumeshakaa vikao kabisa tukapeana maelekezo juu ya maeneo yote hatarishi. Kila mmoja achukue tahadhari kwenye eneo lake. Hili sitalifumbia macho kwa sababu mashimo kama haya yanagharimu maisha ya watu, akiwemo mtoto huyu leo amepoteza maisha kwa shimo la mtu aliyeacha hapa," amesema mwenyekiti.
Watu Watatu Waokolewa Baada ya Kusombwa na Maji
Katika matukio mengine yaliyotokana na mvua kubwa, watu watatu akiwemo mtoto mmoja wameokolewa baada ya kusombwa na maji ya mvua katika kata za Malolo na Mwinyi. Waliosombwa ni mwanamke mmoja, dereva wa pikipiki pamoja na gari lake la bodaboda, na mtoto mmoja aliyekuwa akivuka barabara maeneo ya Mwinyi na mtaa wa Kombomasai kata ya Malolo.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na wananchi wa maeneo hayo wamefanikisha operesheni ya uokoaji.
Kamanda wa Zimamoto Mkoa wa Tabora, Loshipay Laizer, amebainisha kuwa jeshi lake linaendelea na doria kuhakikisha wananchi wote wanaopata changamoto wanaokolewa kwa haraka. Ametoa wito kwa wananchi kuepuka kuacha mashimo wazi kwani ni kinyume cha sheria.
"Sisi tunahakikisha tunawaokoa wananchi wetu wanaopata changamoto. Pia tunawaomba watupe taarifa za matukio katika maeneo yao," amesema Kamanda Laizer.