Ongezeko la Wagonjwa wa Kiharusi Tanzania: Vijana na Wazee Wako Hatarini
Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la idadi ya watu wanaopata kiharusi duniani, Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi zilizoathirika.
Wataalamu wa afya wanasema kiharusi ni ugonjwa wa ghafla unaotokana na ubongo kukosa hewa na virutubishi kutokana na kuziba au kupasuka kwa mishipa ya damu inayosambaza damu kwenye ubongo.
Shinikizo la juu la damu linaweza kusababisha kupasuka kwa mishipa hiyo, huku mafuta mengi yakiganda na kuziba mishipa mingine.
Wagonjwa wanaweza kupooza, kushindwa kuongea, kupoteza kumbukumbu, au hata kifo.
Kwa watu waliowahi kupata kiharusi, hatari ya kupata tena ni kubwa, na hatari ya kifo inategemea aina ya kiharusi.
Kiharusi kinachosababishwa na kuvuruga mishipa ya damu ni hatari zaidi kuliko kiharusi cha kuziba mishipa.
Takwimu za Kimataifa
Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha kuwa kila mwaka, watu milioni 15 hupata kiharusi. Kati yao, milioni tano hufa, na wengine milioni tano hubaki na ulemavu wa kudumu, jambo linalosababisha mzigo mkubwa kwa familia na jamii.
Nchini Tanzania, wagonjwa wa kiharusi wanaongezeka. Wataalamu wa afya wanatoa tahadhari kuwa hali hii inaweza kuathiri vijana na wazee endapo hatua za mapema hazitachukuliwa.
Taasisi za afya kama Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili, Hospitali ya Benjamin Mkapa, na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando zinashuhudia ongezeko hili.
Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili inaripoti kupokea wagonjwa watatu hadi sita kwa wiki waliopata kiharusi cha kupasuka kwa mshipa wa damu, wakati Hospitali ya Benjamin Mkapa inapokea wagonjwa wawili hadi watatu kwa siku.
Sababu na Hatari
Wataalamu wanasema sababu zinazosababisha kiharusi ni pamoja na shinikizo la juu la damu, uvutaji wa sigara, unywaji pombe kupita kiasi, ugonjwa wa moyo, ulaji usiofaa (ikihusisha mafuta mengi, chumvi, na sukari), msukumo wa juu wa damu, kisukari, na ukosefu wa mazoezi.
"Sababu kuu ya kiharusi ni kuziba kwa mishipa ya damu hasa ile iliyopo kwenye ubongo. Damu ikiwa haipiti vizuri kwenye mishipa hiyo, baadhi ya sehemu za mwili hazitafanya kazi ipasavyo. Shinikizo la damu linachangia kwa kiasi kikubwa, pamoja na urithi kutoka kwa wazazi," wataalamu wanaeleza.
Shirika la Afya Duniani linasisitiza kuwa kwa kila wagonjwa 10 wanaokufa kutokana na kiharusi, wengi wangeokolewa kama shinikizo la damu lingedhibitiwa mapema. Kwa watu wenye umri wa chini ya miaka 65, takriban wawili kati ya watano vifo vyao vinahusiana na uvutaji sigara.
Kiharusi Miongoni mwa Vijana
Wataalamu wanasema ingawa wengi huona kiharusi kama ugonjwa wa wazee, viwango vya kiharusi kwa vijana vinaongezeka.
Ripoti za kimataifa zinaonyesha ongezeko la asilimia nane kwa maambukizi ya jumla ya kiharusi, huku ongezeko kubwa zaidi likiwa kwa watu wa umri wa miaka 18 hadi 44 (asilimia 14.6) na miaka 45 hadi 64 (asilimia 15.7).
"Kuongezeka kwa unene uliopitiliza na hali nyingine za kiafya kama kisukari miongoni mwa vijana, kunasababisha magonjwa ya moyo kuanza mapema na kuongeza hatari ya kiharusi katika umri mdogo," wataalamu wanaeleza.
Ripoti za kimataifa zinatabiri ongezeko la asilimia 50 la wagonjwa wa kiharusi kufikia mwaka 2050, litakalosababisha vifo vya watu milioni 9.7 kila mwaka. Zaidi ya asilimia 90 ya vifo hivyo vitatokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati.
Wataalamu wanasisitiza: "Maangamizi yanayosababishwa na vifo na ulemavu kutokana na kiharusi si jambo lisiloepukika. Kiharusi kinaweza kuzuilika kwa kiwango kikubwa kwa kudhibiti sababu za hatari zinazojulikana kama shinikizo la damu, uvutaji sigara, ukosefu wa mazoezi, kisukari, kolesteroli ya juu, tumbaku na pombe. Hatari hizi zinachangia takriban asilimia 90 ya matukio yote ya kiharusi."
Dalili za Kiharusi
Dalili hujitokeza ghafla na hutofautiana kulingana na sehemu ya ubongo iliyoathirika. Miongoni mwa dalili hizo udhaifu au kupoteza ganzi upande mmoja wa mwili au uso, ugumu wa kuzungumza, kushindwa kumeza, kutofahamu kinachoendelea, kuchanganyikiwa, kushindwa kudhibiti misuli, shida ya kuona, na maumivu makali ya kichwa bila sababu.
Wataalamu wanashauri: "Njia za kupunguza uwezekano wa kiharusi ni kuepuka uvutaji wa sigara, kupunguza pombe, kula vyakula vyenye afya, epuka mafuta mengi, sukari na chumvi, fanya mazoezi ya mwili angalau dakika 30 kila siku, dhibiti uzito na shinikizo la damu, na chunguza afya yako mara kwa mara."
Kiharusi kwa Watoto Wenye Seli Mundu
Utafiti unaonesha kuwa kati ya watoto 196 wenye seli mundu, 47 walikuwa hatarini kupata kiharusi. Watoto waliopatikana hatarini walianzishiwa dawa ya ‘Hydroxyurea’, na utumiaji wa ultrasound ya Dopla ya kichwa ulionyesha kuwa kasi kubwa ya mtiririko wa damu kwenye mishipa mikuu ya ubongo inahusiana na hatari ya kiharusi.
Baada ya miezi 12 ya matibabu, asilimia 83 ya watoto waliopokea dawa walifikia utengamafu bila kiharusi au vifo vinavyohusiana na dawa. Watoto wenye bandama kubwa walihitaji dozi ndogo, ambayo iliboresha kiwango cha damu na fetal haemoglobin.
Uzoefu wa Wagonjwa
Joseph Atanas aliyewahi kupata kiharusi cha muda, anasema: "Nilianza kupoteza nguvu upande mmoja wa mwili, hivyo nikakimbia kwenda Hospitali ya Bugando. Madaktari walifanya vipimo vya shinikizo la damu, sukari, na mtiririko wa damu kwenye ubongo. Nikaambiwa nina kiharusi cha muda mfupi, nikaanza matibabu ya kuzuia damu kuganda na kudhibiti shinikizo la damu. Matibabu hayo yalisaidia kupunguza hatari ya kuwa na kiharusi kikubwa. Baada ya kutumia dawa hali yangu iliendelea vizuri; sijawahi kupata hali hiyo tena. Nazingatia maelekezo ya daktari, kufanya mazoezi, kula vizuri na niliacha kabisa kutumia kilevi."
Naye mkazi wa Buhembe mkoani Kagera, Adil Mutalemwa anasema alianza kuumwa sana kichwa, macho na moyo kwenda kwa kasi.
Alipokwenda hospitalini iligundulika ana shinikizo kubwa la damu na kuanza kutumia dawa kwa mwaka mmoja kisha akaacha.
"Baada ya kuona nimepata nafuu na presha kurudi kawaida niliacha dawa, miezi sita kupita tangu nilivyoacha dawa hali yangu ilibadilika. Nilikuwa siwezi kuinua mguu mmoja, mkono na mdomo pia ulianza kwenda upande. Ikabidi nirudishwe tena hospitali ambapo nilianzishiwa dawa upya na mazoezi tiba," anasema.
Anasema kwa sasa hali yake inaendelea vizuri, akieleza kuwa dawa na mazoezi vilimsaidia na hali inarudi taratibu japokuwa kwa sasa anatembea kwa usaidizi huku akiendelea kutumia dawa za presha ya juu.