Othman Masoud: Utulivu wa Zanzibar Unatokana na Utii wa Wanachama wa ACT-Wazalendo
Unguja – Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman, ametoa tamko kuhusu hali ya utulivu uliopo nchini, akisema kuwa ni matokeo ya utii wa wanachama wa chama hicho kwa viongozi wao.
Katika ziara yake Kijiji cha Makangale, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Jumatano Desemba 17, 2024, Othman aliwatoa shukrani wazee na wananchi waliochangia mafanikio ya chama hicho katika uchaguzi uliopita.
Mwenyekiti huyo amedai kwamba busara ya viongozi wa chama hicho ya kuzungumza na wananchi imekuwa muhimu sana katika kudumisha amani baada ya uchaguzi uliochafuliwa.
"Viongozi wa chama hiki wamejitoa kuzungumza na wananchi kwa lengo la kuinusuru Zanzibar na machafuko kila ifikapo kipindi cha uchaguzi," alisema Othman.
Akiendelea, alisema: "Ni dhahiri kwa yaliyofanyika hayakuwa na nia njema kwa nchi na wananchi wake, bali nusura ya Mwenyezi Mungu kupitia dua zilizoombwa maeneo mbalimbali pamoja na wananchi kusikiliza kauli za viongozi ndio usalama huu."
Othman amewataka wananchi kuendelea kuwa na subira na mshikamano wakati mazungumzo ya kutafuta haki kwa njia za amani yakiendelea. Alitaja kijiji cha Makangale kama kielelezo cha maeneo yenye dhamira ya kweli ya mabadiliko visiwani Zanzibar.
Aliyekuwa mgombea ubunge wa Konde, Mohamed Said Issa, alimshukuru Othman kwa elimu ya kihistoria aliyoitoa kuhusu Zanzibar na kuahidi kuendelea kuwa balozi wa amani.
"Sisi tutaendelea kuwa mabalozi wazuri wa amani, subira, na mshikamano jimboni hapa," alisema Mohamed Said.
Kabla ya ziara hiyo, Othman alishiriki katika dua maalumu iliyoandaliwa na wananchi wa Makangale katika Msikiti wa Sheikh Ibrahim Omar, iliyoongozwa na Sheikh Hassan Masoud Hassan.