Dodoma. Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa ameeleza dakika za mwisho namna alivyopokea taarifa na jinsi madaktari walivyopambana kuokoa uhai wa marehemu Jenista Mhagama kabla ya kufariki dunia.
Mchengerwa ameahidi kuendeleza maono, dira na miradi yote aliyoyaasisi marehemu Jenista Mhagama, akisisitiza kuwa urithi aliouacha ndani ya Wizara ya Afya hautapotea bali utaendelezwa kwa nguvu zaidi.
Akizungumza Desemba 12, 2024, jijini Dodoma nyumbani kwa marehemu Itega, Waziri Mchengerwa ameeleza kuwa taarifa alizopokea kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya zilionesha jinsi madaktari walivyopambana usiku na mchana kuokoa maisha ya marehemu.
"Nichukue fursa hii kuwashukuru madaktari wote waliomhudumia pale Benjamin Mkapa walifanya kazi kubwa sana hadi dakika za mwisho. Katibu Mkuu aliniarifu kuwa hali yake ilikuwa mbaya sana, na licha ya jitihada zote, hatimaye Mungu alimchukua," amesema Mchengerwa.
Waziri Mchengerwa amewasihi madaktari wa Hospitali ya Benjamin Mkapa na wahudumu wote wa afya nchini kuendeleza moyo wa utoaji huduma bora, akisisitiza kuwa jitihada walizozionesha kwa Jenista Mhagama zinapaswa kuwa kielelezo cha taaluma yao kila siku.
Aidha, Mchengerwa aliwataka Watanzania kuungana katika kuendeleza kazi iliyofanywa na marehemu, ambaye alikuwa nguzo muhimu katika mageuzi ya sekta ya afya nchini.
Mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Peramiho (CCM), Jenista Mhagama unatarajiwa kuzikwa Jumanne ya Desemba 16, 2024 katika Kijiji cha Ruanda, Mbinga mkoani Ruvuma.