Mazishi ya Aliyekuwa Mbunge wa Peramiho Jenista Mhagama Yataendelea Desemba 16, 2025
Mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Peramiho (CCM), Jenista Mhagama unatarajiwa kuzikwa Jumanne ya Desemba 16, 2025 katika Kijiji cha Ruanda, Mbinga mkoani Ruvuma.
Jenista ambaye amekuwa mbunge wa Peramiho kuanzia mwaka 2005, amefariki dunia Alhamisi, Desemba 11, 2025 jijini Dodoma.
Ratiba ya mazishi yake iliyotolewa na uongozi wa Bunge, inaonesha Ijumaa, mwili wake utapelekwa nyumbani kwake Itega, jijini Dodoma.
Ratiba Kamili ya Mazishi
Jumamosi ya Desemba 13, 2025, mwili wa Jenista utapelekwa Kanisa Katoliki Kiwanja cha Ndege ambapo ibada itafanyika.
Viongozi mbalimbali watahudhuria kanisani wakiwemo Spika wa Bunge, Mussa Zungu, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba na Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi.
Baada ya shughuli ya kanisani, mwili wa Jenista utasafirishwa kwenda Songea, Mkoa wa Ruvuma.
Desemba 14, 2025, maombolezo yataendelea nyumbani kwa Jenista, eneo la Makambi, Songea Mjini. Siku hiyo mwili utapelekwa Kanisa Katoliki Matogoro, Songea Mjini ambapo ibada itafanyika na baadaye mwili kurudishwa nyumbani.
Desemba 15, 2025, mwili wa Jenista utapelekwa kwa wapiga kura wake Peramiho ambapo shughuli itafanyika Kanisa Katoliki la Peramiho. Viongozi mbalimbali wanatarajiwa kuwepo akiwemo Zungu, Dk Mwigulu na Dk Nchimbi.
Baadaye mwili utarudishwa nyumbani kwake Peramiho.
Desemba 16, 2025, mwili wa Jenista utapelekwa Kijiji cha Ruanda ambapo utahifadhiwa katika nyumba yake ya milele.