TIA Yashauri Kuongeza Elimu ya Biashara Kampasi ya Mbeya
Mbeya – Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) kimeshauriwa kuongeza elimu ya nidhamu ya biashara na kutafuta mbia wa kifedha badala ya kuomba misaada ya kifedha kuwawezesha wahitimu kufikia malengo yao ikiwamo ajira binafsi kupitia ujasiriamali.
Akizungumza Desemba 12, 2025 katika mahafali ya 13 ya chuo hicho kampasi ya Mbeya, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa amewataka wahitimu kutumia elimu kwa uadilifu na nidhamu kuitumikia jamii na Taifa.
Amesema ili kuwawezesha wanafunzi kielimu, TIA ianzishe elimu ya nidhamu ya biashara ili mtu anapofanya ununuzi kwa kuuza au kununua ajue faida na hasara katika kipato chake, hali ambayo itasaidia vijana kutengeneza ajira binafsi kupitia ujasiriamali.
"Lakini Mkoa wa Mbeya unazo fursa nyingi za kiuchumi katika uwekezaji kama madini, kilimo, teknolojia na digitali, wahitimu tumieni nafasi hizi kutengeneza kipato," alisema Malisa.
"Pia, kuwepo na financial partners (mbia wa kifedha) badala ya financial support (msaada ya kifedha), kuna fursa ya Sh200 bilioni zilizotangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo leteni mawazo na ofisi zetu zitakuwa wazi," ameongeza.
Ongezeko la Udahili wa Wanafunzi
Akitoa taarifa ya chuo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Pallangyo amesema kwa sasa kampasi hiyo imeendelea kukua katika maeneo mbalimbali kitaaluma na miundombinu.
Profesa Pallangyo amesema kwa mwaka wa masomo 2025/26, chuo hicho kimeongeza udahili wa wanafunzi kufikia 1,808 ikilinganishwa na mwaka uliopita wa wanafunzi 1,416, ikiwa ni uelekeo thabiti wa maendeleo katika chuo hicho.
"Ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira, Taasisi imeanzisha kozi mpya tano ikiwa ya masomo ya juu tatu na mbili kwa ngazi ya shahada katika kampasi hii ya Mbeya, ambazo ni Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Uhasibu na Fedha na Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Ununuzi na Ugavi," alisema.
"Nyingine ni Shahada ya Uzamili ya Uongozi wa Biashara katika Usimamizi wa Miradi huku ikiwamo pia Shahada ya Usimamizi wa Biashara na Shahada ya Uongozi wa Rasirimali watu, kwa takwimu leo wahitimu ni 1,480 katika kozi mbalimbali," ameongeza Profesa huyo.
Uwekezaji wa Serikali
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo hicho, Profesa Johavness Aikael ameupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kuandaa wataalamu wenye uwezo wanaokidhi vigezo katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Amesema serikali imeendelea kuweka uwekezaji katika chuo hicho kwa kuboresha miundombinu ya kufundisha na kujifunzia na kuongeza ufanisi kitaaluma.
"Kukamilika kwa miundombinu ya mkataba, maabara, ukumbi wa mihadhara na madarasa yenye uwezo wa kubeba wanafunzi hadi 500 inachochea ongezeko la wanafunzi kufikia 3,349 kwa mwaka huu ikilinganishwa na idadi ya 2,888 kwa mwaka 2024/25," amesema Profesa Aikael.
Amesema kuwa kutokana na juhudi hizo za serikali kupitia sekta ya elimu, wahitimu wanapaswa kutumia taaluma zao kama nguzo ya mafanikio kufikia malengo yao akieleza kuwa wanafahamu changamoto ya ajira.
"Tunao vijana wenye ubunifu, waliofunguka kimawazo kuzifuata fursa na kuweka vyeti vyao chini kulitumikia Taifa, tunatarajia kupata wawekezaji kupitia wahitimu kutoka chuo cha TIA," amemaliza Profesa huyo.
Sauti ya Wanafunzi
Mmoja wa wanafunzi katika chuo hicho, Evance Kweka ameiomba serikali kuwasapoti vijana wenye ubunifu akiwaomba wahitimu kutotegemea vyeti badala yake kutumia ujuzi walionao kujikwamua kiuchumi.
Mwanafunzi huyo aliyebuni programu ya ‘Mafundi Popote’ amesema ili kuondokana na mgogoro wa ajira baina ya vijana na mamlaka, serikali iwaangalie wenye ubunifu na kuwawekea mazingira kuweza kutengeneza fursa binafsi.
"Kilio chetu zaidi ni kuajiriwa, lakini kama kijana ana ubunifu serikali inaweza kutengenezea mazingira wezeshi ili aungane na wengine kujiajiri, lakini wahitimu wasitegemee sana vyeti, watumie ujuzi na maarifa waliyopata," amesema Kweka.