Dodoma Yatangaza Kilimo Kipya cha Tufaa ili Kuongeza Kipato cha Wakazi
Dodoma – Mkoa wa Dodoma umetambulisha mpango mpya wa kilimo cha tufaa (apple) kama zao la kibiashara lenye lengo la kuongeza mapato ya familia mkoani. Kila kaya itatakiwa kupanda angalau miti miwili ya tufaa kwa ajili ya kujipatia kipato cha ziada.
Mti wa tufaa huanza kuzaa matunda baada ya miaka miwili, na mti mmoja uliotunzwa vizuri una uwezo wa kuzaa matunda 350 kwa wakati mmoja. Heka moja inaweza kupandwa miti 450, na kutokana na soko kubwa la matunda haya ndani na nje ya nchi, mkulima ana fursa ya kujikomboa kiuchumi.
Mkoa Utanunua Miche 6,000
Wakati wa kutiliana saini makubaliano ya ununuzi wa miche ya matunda hayo na kampuni ya Tamtam Tanzania Limited Ijumaa Disemba 11, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alisema zao hilo litakuwa ni la kimkakati kati ya mazao mengine yanayolimwa mkoani.
Mkoa umekubaliana kununua miche 6,000 yenye thamani ya shilingi milioni 72, ambayo itasambazwa katika halmashauri za wilaya zote. Kutakuwa na mashamba darasa ya zao hilo ili kuwawezesha wakulima na wadau wengine kujifunza kilimo hicho kupitia wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo.
Lengo la Kutunza Mazingira na Kuongeza Mapato
Senyamule alisema mpango wa kupendekeza kilimo cha tufaa ulifikwa pale walipotafuta zao jingine la kimkakati ambalo litatunza mazingira na pia kuwa chanzo cha mapato ya familia. Ameeleza kuwa tofauti na miti mingine inayopandwa bure na kudhoofika kwa ukosefu wa utunzaji, mti wa tufaa unauzwa kwa bei kubwa, hivyo watu watautunza vizuri.
"Mche mmoja wa matufaa unauzwa shilingi 12,000 kwa hiyo sidhani kama kuna mtu atakayekubali anunue miti kwa bei kubwa halafu auache ukauke. Soko la matunda haya ni kubwa ndani na nje ya nchi hivyo mbali na kutunza mazingira lakini inaongeza kipato cha familia," alisema Senyamule.
Kila Kaya Kupanda Miti Miwili
Mkuu wa Mkoa ameagiza kila kaya mkoani kupanda miti miwili ya matofaa ili kutunza mazingira na kujiongezea kipato pale itakapokuwa na kuanza kuzaa matunda, ambayo bei yake haipungui shilingi 1,000 kwa tunda moja.
Alisema zipo aina nyingi za matufaa lakini Mkoa wa Dodoma utapanda aina tatu ambazo zimefanyiwa utafiti na kubainiwa zinastahimili hali ya hewa ya mkoa huo. Tayari zimeshaonyesha mafanikio makubwa kwa wale waliopanda kwa majaribio.
Mbali na tufaa, Senyamule alisema kuna mazao mengine ya kimkakati yanayolimwa mkoani Dodoma ikiwa ni pamoja na alizeti, mtama na zabibu ambalo ni zao pekee linalolimwa mkoani humo.
Kampuni Kuhakikisha Soko
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dk Khatibu Kazungu, amethibitisha kuwa mkoa umenunua miche 6,000 ya mitofaa yenye thamani ya shilingi milioni 72 kwa lengo la kuongeza kipato cha wakazi.
Mwakilishi wa kampuni ya Tamtam, Gibson Kalyetekela, alisema kampuni yao inazalisha aina zote za miche ya mitofaa na itanunua matunda yote yatakayozalishwa nchini, hivyo kuondoa wasiwasi wa kukosa soko la zao hilo kwa wakulima watakapohamasishwa kulima kwa wingi.