Chama cha Mapinduzi (CCM) Yahamasisha Wanachama Kujiandikisha Kwenye Daftari la Mpiga Kura
CCM imewataka wanachama wake kujitokeza kwa wingi ili kuboreshwa taarifa zao kwenye daftari la mpiga kura, lengo lake kuhakikisha nafasi ya kushika dola.
Uboreshaji wa taarifa za mpiga kura, ambao utawezesha kila mtanzania kupata kibali cha kutumia haki yake ya kuchagua kiongozi, utaanza Machi 17 hadi 23 mwaka huu katika mkoa wa Dar es Salaam.
Katika mkutano wa ndani wa Wilaya ya Ubungo, Katibu wa NEC, Amos Makalla alisema kuwa ili kushika dola, wanachama lazima wajiandikishe kwanza kabla ya kuanza kuhamasisha wananchi wengine.
“Tuna wanachama 12 milioni nchi nzima, na Dar es Salaam tunaongoza kwa idadi ya wapiga kura. Viongozi wa Wilaya, Kata, Matawi na Mitaa wanahitajika kuhakikisha watu wao wanajiandikisha,” alisema Makalla.
Akizungumzia umuhimu wa uchaguzi, Makalla alisema kura nyingi ndizo zinazotoa ushindi, hivyo wananchi wasiache mchakato huo ikiwa wanataka kudhibiti nchi.
Makalla alishauri viongozi wa serikali za mitaa kufanya kazi kwa uadilifu ili wananchi wapate huduma bora, na kuhakikisha kuwa wanachama wanaendelea na jukumu la kuhamasisha wengine kujiandikisha.
“Tunahimiza wanachama wakutane na watu wao kuanzia Machi 17 hadi 23, 2025 na kuwahamasisha kujiandikisha ili tuhakikishe ushiriki mkubwa kwenye uchaguzi ujao,” alisema.