Nassoro Hamdani, Mjumbe Mstaafu wa CCM Taifa Afariki Dunia
Tabora – Mjumbe mstaafu wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa kutoka Mkoa wa Tabora, Nassoro Hamdani, amefariki dunia leo wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Mbali na nafasi yake ya kisiasa, Hamdani alikuwa ni mkurugenzi wa kampuni ya usafirishaji ya NBS Classic.
Mtoto mkubwa wa familia, Salum Hamdani, amesema baba yake amekuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu kwa muda mrefu, lakini kwa siku kumi zilizopita alizidiwa ghafla na wakamuwahisha katika Hospitali ya Mirambo, Tabora, baadaye akapelekwa Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Salum amesema akiwa Muhimbili alipata nafuu kwa siku chache lakini aliendelea kuugua, na ikizingatiwa ni mzee hivyo nguvu pia amekuwa hana. Kufikia leo asubuhi amefariki dunia akiwa anaendelea na matibabu Muhimbili.
Ameongeza kuwa mwili utasafirishwa kwa ndege binafsi kutoka jijini Dar es Salaam hadi Tabora ambako ndiko nyumbani kwake kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika kesho, licha ya kuwa muda kamili wa mazishi bado haujafahamika.
"Mzee wetu ametutoka, tunaumia sana lakini hii ni kadari ya Mwenyezi Mungu tunaipokea kwa mikono miwili. Tunamshukuru pia na tunamuomba atufariji na kututia nguvu tusitoke nje ya misingi ya dini," amesema Salum.
Msaada kwa Jamii
Nicholaus Kagusa, mkazi wa Tabora, ameeleza kuwa kifo cha mzee Hamdan ni pigo kubwa kwao kwani hakuwa mwanasiasa na mwekezaji tu bali alikuwa mlezi wa wanyonge na msaada mkubwa kwenye matatizo na hata furaha.
"Maumivu niliyo nayo siwezi kumsimulia hata mtu kwa sababu msiba huu ni mkubwa mno kwetu. Mzee huyu tumemzoea, ni mzee mwenye ushauri na hakuwahi kutudharau watu maskini, na kwanza ndio marafiki zake," amesema Kagusa.
Ashura Ramadhani amesema atamkumbuka kwa tabia ya kujitolea kwa wasiojiweza. Alikuwa kila Ijumaa anawapa chakula na fedha. Mwezi wa Ramadhani alikuwa anafuturisha bila kujali maskini wala tajiri mwezi mzima, na ikifika sikukuu ya Eid anatoa mchele, mafuta na vitu vingi ili kila mmoja afurahie nyumbani kwake.
"Mi nimeshalia mpaka nimechoka. Ebu fikiria, mwezi mtukufu ni keshokutwa tu halafu huyu mzee amefariki. Sasa sisi tutafuturu wapi? Hivi sikukuu sisi tutakulaje?" ameongea kwa huzuni Ashura.
Mfanyakazi Mzuri
Seif Seif ambaye ni konda katika kampuni ya NBS, amesema wameumizwa sana na msiba wa mzee huyo kwa sababu kampuni yake ni mojawapo ya kampuni nzuri kufanya kazi.
"Hii kampuni inatufanya tunalea familia zetu, lakini humu ndani hakuna masimango na ukiwa na changamoto unasaidiwa. Tunafanya kazi kwa amani sana," amesema Seif.
TNC inaendelea kufuatilia habari hii na itawaletea masasisho zaidi kuhusu mazishi ya marehemu Nassoro Hamdani.