Benki ya Dunia Yaingia Mkataba na Chuo Kikuu cha Mzumbe kwa Mafunzo ya Ununuzi Endelevu
Dar es Salaam. Benki ya Dunia imesema utekelezaji wa miradi ya maendeleo hauwezi kufanikiwa bila mifumo madhubuti ya ununuzi inayozingatia ufanisi, uwazi na utekelezaji kwa wakati, ikisisitiza kuwa kuchelewa kwa maendeleo ni sawa na kuwanyima wananchi haki yao ya kunufaika na rasilimali za umma.
Kutokana na hilo, Benki ya Dunia imeingia mkataba na Chuo Kikuu cha Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, Januari 13, 2026, kwa lengo la kutoa mafunzo ya ununuzi endelevu kwa watendaji wa miradi inayofadhiliwa na benki hiyo, ili kuimarisha uwajibikaji, ufanisi na matokeo ya maendeleo katika sekta ya umma.
Akizungumza Februari 2, 2026, wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya wiki mbili ya kuwajengea uwezo wa ununuzi na usimamizi wa mikataba kwa Vitengo vya Utekelezaji wa Miradi (PIUs), Meneja wa Uendeshaji wa Benki ya Dunia kwa Tanzania, Zambia, Malawi na Zimbabwe, Milena Stefanova, amesema kuchelewesha maendeleo ni sawa na kuwanyima wananchi haki yao ya maendeleo.
Ununuzi Wenye Ufanisi Nguzo Muhimu Katika Kufanikisha Miradi
Stefanova amesema ununuzi wenye ufanisi na unaotekelezwa kwa wakati ni nguzo muhimu katika kufanikisha miradi, kwani unapotekelezwa ipasavyo huwezesha miundombinu kama barabara, vituo vya afya na shule kukamilika kwa wakati na jamii kuanza kunufaika mapema.
Amesema Benki ya Dunia imefadhili miradi mbalimbali katika sekta tofauti kwa thamani ya takribani dola bilioni 4 za Marekani, sawa na Sh trilioni 10, akisisitiza kuwa mifumo thabiti ya manunuzi ni msingi wa mafanikio ya miradi hiyo.
"Ununuzi unapofanya kazi vizuri, huduma muhimu zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa ubora unaotarajiwa. Ndiyo maana programu hii imelenga kusaidia timu za miradi kuhamia kutoka kufuata taratibu pekee hadi kupata matokeo halisi," amesema Stefanova.
Amesema mafunzo hayo yamelenga kuingiza mfumo wa ununuzi wa Benki ya Dunia, kanuni zake na zana za vitendo katika kazi za kila siku za utekelezaji wa miradi, ili kuhakikisha ununuzi mzuri unatafsiriwa kuwa utoaji wa huduma kwa wakati na kwa ubora.
Ushirikiano Imara Kati ya Benki ya Dunia na Chuo Kikuu cha Mzumbe
Stefanova amesema utekelezaji wa programu hiyo umetokana na ushirikiano imara kati ya Benki ya Dunia na chuo hicho, ambapo pande hizo mbili zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) ya kuendesha kwa pamoja mfululizo wa mafunzo ya muda mfupi na ya vitendo kuhusu ununuzi na usimamizi wa mikataba.
"Hatutaki kila mara wataalamu wa ununuzi kusafiri kutoka Washington, DC, kuja kutoa mafunzo. Tunataka chuo kiwe na uwezo wa kuendesha programu hizi chenyewe kwa uendelevu, huku sisi tukitoa msaada wa kiufundi, ushauri na uhakiki wa ubora," amesema.
Amesema mahitaji ya mafunzo hayo yamekuwa makubwa tangu yalipotangazwa, ambapo ndani ya wiki moja zaidi ya waombaji 100 waliwasilisha maombi, hali iliyosababisha kushindwa kuwapokea wote katika awamu ya kwanza ya mafunzo.
Chuo Kikuu cha Mzumbe Kinasisitiza Ununuzi Endelevu
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa William Mwegoha, amesema chuo hicho kinautazama ununuzi endelevu kama nyenzo ya kimkakati katika kuimarisha utawala bora, ufanisi wa kiuchumi, uhifadhi wa mazingira na ujumuishaji wa kijamii.
Amesema katika miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, ununuzi bora una mchango mkubwa katika kufanikisha matokeo yaliyokusudiwa ya miradi hiyo.
"Kupitia mafunzo haya ya vitendo, washiriki watawezeshwa kupata siyo tu uelewa wa kanuni na sheria, bali pia uwezo wa kufanya maamuzi makini, maadili ya kazi na ujuzi wa kimkakati katika ununuzi wa umma," amesema Profesa Mwegoha.
Amesema chuo kitaendelea kutumia programu hiyo kama fursa ya kuzalisha tafiti tumizi kuhusu mifumo ya ununuzi, usimamizi wa mikataba na changamoto za utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na wahisani, ili kuchangia mijadala ya sera, kuboresha mitaala ya elimu na kuongeza hazina ya maarifa ya kitaifa na kikanda.
Wizara ya Fedha Inasaidia Juhudi za Uimarishaji
Kamishna Msaidizi wa Manunuzi ya Umma, Wizara ya Fedha, Emma Komba amesema mafunzo hayo ni hatua muhimu katika kuhakikisha ufanisi, uwazi na uwajibikaji wa miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia na wahisani wengine.
"Mafunzo haya ni muhimu sana katika kusaidia serikali kutekeleza kwa ufanisi miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, kwa kuhakikisha taratibu za ununuzi zinazingatia thamani ya fedha na matumizi sahihi ya rasilimali za umma," amesema.
Washiriki Watoa Maoni Chanya
Mshiriki wa mafunzo hayo, ambaye ni Ofisa Ununuzi wa Mradi wa Bonde la Msimbazi, Sovela Elia, amesema miradi inayotekelezwa chini ya Mradi wa Msimbazi na DMDP ni mikubwa na yenye thamani ya takribani dola za Marekani milioni 1.6, hivyo ununuzi bora ni muhimu ili miradi hiyo ipate matokeo yanayotarajiwa.
"Programu hii itasaidia kuhakikisha miradi hiyo inafanikishwa kwa wakati na kwa kiwango kinacholengwa, ikilinda rasilimali za umma na kuhakikisha wananchi wananufaika mapema," amesema Elia.
Amesema kupitia mafunzo hayo, wataalamu wa manunuzi watapata ujuzi wa kiutendaji unaowawezesha kusimamia miradi mikubwa ya serikali na wahisani wengine, kufanya maamuzi sahihi, kusimamia mikataba na kutimiza malengo ya miradi kwa ufanisi zaidi.