Mahakama Yaiamuru Lodhia Steel Industries Kulipa Fidia ya Sh270 Milioni
Arusha – Mahakama Kuu imetoa uamuzi wa kuilazimisha kampuni ya Lodhia Steel Industries Ltd pamoja na dereva wake, Abdalah Mbugu, kulipa fidia ya shilingi milioni 270 kwa kampuni ya Leopard Tours Limited kutokana na madhara ya ajali.
Kampuni ya Leopard Tours ilikuwa imefungua shauri la madai namba 28359 la mwaka 2023 katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, ikiomba kulipwa fidia maalum na fidia ya jumla ya zaidi ya shilingi bilioni 1.7 kutokana na athari za ajali hiyo.
Hukumu ya Mahakama
Katika hukumu yake aliyoitoa Januari 30, 2025, Jaji Frank Mahimbali alisema mwajiri anawajibika kisheria kwa matendo ya mwajiriwa yaliyofanywa wakati wa ajira, hivyo wote wawili wanawajibika kulipa fidia hiyo.
Leopard Tours Limited walifungua kesi hiyo dhidi ya kampuni ya Lodhia Steel Industries Limited kama mdaiwa wa kwanza, Mbugu au Abdalah Mohamed Kituru kama mdaiwa wa pili na mdaiwa wa tatu, kampuni ya Bima ya Meticulous General.
Maelezo ya Ajali
Kulingana na hati ya madai, Juni 16, 2023 eneo la Kambi ya Mkaa, Kikatiti katika barabara Kuu ya Moshi-Arusha, gari la Lodhia Steel Industries likiendeshwa kwa uzembe na mwajiriwa wao, liligongana uso kwa uso na gari la Leopard Tours.
Kutokana na ajali hiyo, kampuni ya Leopard Tours ikaiomba mahakama iwaamuru wadaiwa kuilipa fidia kutokana na madhara waliyoyapata wakati gari lao Toyota Landcruiser lilipogongana na lori Mitsubishi Fuso.
Kampuni ya Leopard Tours wakaomba walipwe fidia maalum na fidia ya jumla inayofikia shilingi bilioni 1.75, riba ya fedha hizo pamoja na gharama za kesi hiyo ambapo mdaiwa wa kwanza na wa pili walikataa kuwajibika kulipa fidia hiyo.
Hoja za Mahakama
Kwa makubaliano ya mdai na wadaiwa, walikubaliana hoja za kuamuliwa na mahakama ambazo ni pamoja na kama Mbugu alikuwa ni mzembe hadi kusababisha ajali na pili kama pia alikuwa ni dereva wa kampuni ya Lodhia.
Jaji alisema mashahidi wa upande wa wadaiwa katika shauri hilo walijaribu kushambulia uhusiano wa mwajiri na mwajiriwa hisia za hasara wakati mdai ana ushahidi thabiti wa uzembe, majeraha, na uharibifu wa kifedha wa haraka.
"Kwa kuangalia madai ya nafuu zinazoombwa inaonyesha kuwa mdai alipata hasara maalumu na hasara ya jumla zilizoorodheshwa katika hati yake ya madai. Kanuni zinazoongoza utoaji wa fidia ya uharibifu si ngeni," alisema Jaji.
Ushahidi wa Uzembe
Jaji Mahimbali alisema baada ya kuupitia kwa makini ushahidi na misingi ya kisheria kuhusu kama dereva Mbugu alikuwa mzembe, shahidi wa kwanza ambaye ni dereva wa gari la kampuni ya Leopard Tours alieleza kwa kina.
Dereva huyo alitoa ushuhuda wa kuona namna mdaiwa wa pili wakati akiendesha lori la mdaiwa wa kwanza, alipuuza alama za barabarani na kuendeshwa kwa uzembe na kusababisha lori alilokuwa akiendesha kugongana naye uso kwa uso.
"Mdaiwa wa pili aliyekuwa shahidi wa kwanza kwa mdaiwa alikana kuendesha kwa uzembe, akilaumu mafundi wanaotengeneza barabara lakini akakiri kutiwa hatiani katika kesi ya trafiki. Kukataa kwake kunapingana na kesi hiyo," alisema.
Mahusiano ya Mwajiri na Mwajiriwa
Kuhusu hoja ya mahusiano ya ajira kati ya mdaiwa wa pili (Mbugu) na mwajiri wake (kampuni ya Lodhia), shahidi wa pili wa mdai ambaye ni Ofisa Rasilimali Watu wa Leopard Tours alitoa vielelezo vinavyoonyesha mahusiano hayo.
Miongoni mwa nyaraka alizozitoa mahakamani kama kielelezo ni pamoja na michango ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na katika mahojiano ya dodoso, mdaiwa wa pili alikiri kuwa ni kweli ni mwajiriwa wa kampuni ya Lodhia.
"Kwa kuzingatia mizania ya ushahidi, ninaona mdaiwa wa pili alikuwa mwajiriwa wa mdaiwa wa kwanza na alikuwa akitenda kazi ndani ya wigo wa ajira yake. Hivyo, dhana ya wajibu wa mwajiri inafanya uwajibikaji uhamishiwe kwake," alisema Jaji.
Fidia ya Madhara ya Uharibifu
Kuhusu hoja ya uharibifu, Jaji Mahimbali alisema shahidi namba tatu wa mdai ambaye ni Meneja wa Fedha, alitoa vielelezo ambavyo ni bili za matibabu, ankara za hoteli, gharama za kuvua gari na makadirio ya gharama za kutengeneza gari.
"Nyaraka hizi zinaeleza kikamilifu jinsi mdai anavyothibitisha uharibifu au hasara, faida iliyopotea na biashara, pamoja na gharama za papo hapo," alisema Jaji.
"Hivyo ninaona ni kweli mdai alipata hasara lakini zile zinazoweza kuthibitishwa," alisema.
Mkataba wa Bima
Kuhusu iwapo kulikuwa na mkataba wa bima kati ya mdaiwa wa kwanza na mdaiwa wa tatu, Jaji alisema imethibitika ulikuwepo mkataba huo.
"Hivyo basi, bima inawajibika kufidia mdaiwa wa kwanza kwa majeraha ya mwili kwa abiria na uharibifu wa mali kwa gari la mdai katika shauri hili," alieleza Jaji.
Hata hivyo Jaji alisema, Sera hii haijumuishi hasara za pembeni kama vile kusitishwa kwa biashara na uharibifu wa sifa kwa hivyo, anaona kuwa bima inawajibika tu ndani ya wigo wa uharibifu wa kimwili na wa mali.
Uamuzi wa Kiasi cha Fidia
Jaji katika uamuzi wake, hukumu yake imetolewa kwa niaba ya mdai dhidi ya mdaiwa wa kwanza na wa pili kwa pamoja na kila mmoja peke yake hivyo mdai wanapewa tuzo ya kurejeshewa bili za matibabu zinazofikia shilingi milioni 2.
Pia anapewa tuzo ya kulipwa gharama za malazi shilingi milioni 1.68, tuzo ya kurejesha pesa kwa Kobo Safaris shilingi milioni 6.6, gharama za kuvuta gari shilingi 400,000, utengenezaji wa gari shilingi milioni 164 na gharama nyingine.
Mbali na tuzo hiyo, mahakama imewaamuru wadaiwa kulipa shilingi milioni 50 za uharibifu wa sifa na usumbufu, hasara iliyotokana na gari kusimama kwa miezi sita shilingi milioni 25, gharama za kesi na kampuni ya bima kulipa madhara ya kimwili.
Fidia yote hiyo inafikia shilingi milioni 270.4 bila kujumlisha gharama za kesi.