Vijana Sita Wahukumiwa Kifungo cha Miaka 30 kwa Unyang’anyi Morogoro
Morogoro – Mahakama ya Wilaya ya Morogoro imewahukumu vijana sita kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha, tukio lililotokea Machi 31, 2025 katika eneo la Chamwino.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, ametoa taarifa leo Januari 22, 2026 akieleza kuwa vijana hao walihusika na tukio la unyang’anyi lililotokea saa moja usiku wa Machi 31, 2025 katika eneo la Shule ya Msingi Chamwino, Manispaa ya Morogoro.
Kulingana na taarifa zilizotolewa, watuhumiwa hao walimvamia mfanyabiashara na mkazi wa Chamwino, Abubakar John, wakitumia silaha za jadi. Waliweza kumjeruhi kichwani kwa panga kabla ya kumpora simu aina ya iPhone pamoja na fedha taslimu shilingi 635,000.
Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wote na kuwafikisha mahakamani kwa hatua za kisheria.
Kamanda Mkama ameeleza kuwa baada ya usikilizwaji wa kesi chini ya Hakimu Theresia Kaniki wa Mahakama ya Wilaya ya Morogoro, mahakama iliwakuta na hatia Januari 19, 2026 na kuwahukumu kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja.
Waliokutwa na hatia ni Ramadhani Shabani Abdallah (24), Amos John Pagu (23), Said Shabani Aidan (20), Ally Hassan Ally (20), Joseph Raymond Haule (18) na Adrian Exavel Thomas (18), wote wakazi wa Chamwino.
Jeshi la Polisi limewataka vijana wote kuachana na vitendo vya uhalifu na badala yake kujikita katika shughuli halali za kujipatia kipato. Kamanda Mkama amesisitiza kuwa mkono wa sheria ni mrefu na hautamwacha mtu yeyote anayejihusisha na uhalifu.