Saturday, March 14, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Instagram
TNC
  • Home
  • Home
No Result
View All Result
TNC
No Result
View All Result

Makundi ya tembo yawatisha wananchi Lushoto, hatua za dharura zimeanzishwa kutatua tatizo

by TNC
January 20, 2026
in Swahili
0
0
SHARES
6
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Wananchi wa Lushoto Walalamikia Uharibifu wa Tembo, Waomba Serikali Ichukue Hatua

Lushoto – Wananchi wa kata ya Lunguza katika Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wamelalamikia uwepo wa makundi makubwa ya tembo ambayo yamekuwa yakiharibu mazao mashambani, kuharibu miundombinu ya maji na wakati mwingine kusababisha vifo vya watu, hali inayowafanya kuishi kwa hofu.

Wakizungumza na TNC Januari 20, 2026, wananchi hao waliiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kwa kuyafukuza makundi hayo ya tembo kutoka kwenye makazi yao na kuyarejesha kwenye hifadhi, ili waweze kuendelea na shughuli zao za kilimo na ufugaji bila vitisho.

Mkazi wa kijiji cha Kiwanja, kata ya Mnazi wilayani Lushoto, Kingazi Ally, amesema tembo wamekuwa wakifukia mabwawa waliyoyachimba kwa ajili ya maji ya kunywa na mifugo, hali inayosababisha adha kubwa kwa jamii ya wafugaji.

"Mpaka sasa tunafikiria kuchimba tena mabwawa, lakini haitasaidia kwa sababu mara tu baada ya kuchimba tembo wanahamia hapo na kuanza kufanya uharibifu. Mbali na mazao kuharibiwa, watu pia wanauawa. Ukisikia habari kutoka vijiji vya pembezoni, ni vifo na uharibifu wa mashamba," amesema Ally.

Ally ameongeza kuwa hivi karibuni katika kijiji cha Lunguza, mtu mmoja aliuawa na tembo, hali iliyosababisha hata watoto kushindwa kwenda shule kwa hofu ya kuvamiwa.

"Hata kwenda sokoni imekuwa shida. Tunaomba hawa tembo wafukuzwe warudishwe kwenye hifadhi. Kama wananchi tumeshindwa, tunamuomba Rais mwenyewe aingilie kati," amesema.

Kwa upande wake, Matachu Ligase amesema watoto wao wanapata shida kubwa kutokana na uwepo wa tembo, huku baadhi wakishindwa kuhudhuria masomo kwa hofu ya kukutana na makundi hayo.

Amesema hali hiyo inaweza kuathiri maendeleo ya kitaaluma ya watoto wao.

Ligase ameongeza kuwa kukaa kwa muda mrefu kwa tembo kwenye makazi ya watu kunawafanya wananchi washindwe kuendelea na shughuli zao za kiuchumi, hususan kilimo na ufugaji, ambazo ndizo tegemeo lao kuu la maisha.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kiwanja Omari Mwanfula amesema wananchi wa kijiji hicho wanakabiliwa na hatari ya njaa kutokana na tembo kuvamia mashamba na kuharibu mazao.

Ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuhakikisha wananchi waliopata madhara wanalipwa fidia kwa wakati ili kupunguza ugumu wa maisha yao.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wilaya ya Lushoto, Zakayo Ngioko, amesema tembo wamekuwa kikwazo kikubwa kwa jamii ya wafugaji na wakulima, hali inayosababisha mauaji na kuongeza hofu kwa wananchi.

"Hivi karibuni tulipata taarifa ya mzee mmoja wa Kimang’ati aitwaye Robert, mkazi wa kijiji cha Lunguza, aliyeshambuliwa na tembo na kisha kuuawa. Kwa kweli tembo wamezidi, hofu imeongezeka kwa wachungaji, wakulima na wanafunzi," amesema Ngioko.

Akizungumzia hatua zinazochukuliwa, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Zephania Sumaye, amesema jitihada zinaendelea kuhakikisha tembo wanaondolewa kwenye makazi ya watu na kurejeshwa kwenye hifadhi ili wananchi waendelee na shughuli zao kama kawaida.

"Tarafa ya Umba kwa ujumla ina changamoto ya tembo wanaotoka Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi. Hali ya ukame iliyozidi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Kenya, imesababisha tembo kutoka pori la Tsavo kuvuka mpaka na kuingia kwenye makazi ya watu," amesema Sumaye.

Sumaye ameipongeza Mamlaka ya Uhifadhi wa Wanyamapori (Tawa) kwa jitihada zao za kudhibiti tembo kwenye makazi ya watu, akisema wamefanya kazi kubwa lakini changamoto bado ipo.

Ameongeza kuwa eneo hilo lipo kwenye korido za wanyamapori, na tembo huwa hawasahau mapito yao ya asili. "Tumezungumza na wataalamu wa maliasili na tumefanikiwa kuwafunga kola tembo katika makundi makubwa matatu kwa Lushoto, Korogwe Mkinga, ili kuwafuatilia wanapotoka hifadhi na kuingia kwenye makazi ya watu," alisema.

Mkuu huyo wa wilaya amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua zote muhimu kuhakikisha wananchi wa maeneo yaliyoathiriwa wanaendelea na shughuli zao za kijamii na kiuchumi bila hofu, huku tembo wakidhibitiwa kwa njia endelevu.

Tags: DharurahatuaKutatuaLushotoMakundiTatizoTemboWananchiyawatishazimeanzishwa
TNC

TNC

Next Post

Army chief Muhoozi orders Bobi Wine to surrender within 48 hours

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Popular News

  • Zanzibar’s Leadership Advocates for Streamlined Tax System to Enhance Economic Growth

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanaohujumu miundombinu watachukuliwa hatua kali

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanaohujumu miundombinu watachukuliwa hatua kali

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wasiwasi juu ya Uchochezi wa Makada katika Jimbo la Katavi

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanawake Wanaonyonyesha Washauriwa Kula Milo Mitano Siku

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Category

  • English
  • Swahili

Socials

Instagram TikTok YouTube Facebook

About Us

TNC (Tanzania News Company) is the primary Source of News in English & Swahili in Tanzania

© 2025 TNC - Tanzania News Company

Welcome Back!

Login to your account below

Forgotten Password?

Retrieve your password

Please enter your username or email address to reset your password.

Log In
No Result
View All Result
  • Home

© 2025 TNC - Tanzania News Company