Chadema Wadai Kampeni ya ‘Bila Mabadiliko Hakuna Uchaguzi’ Imeimarisha Chama
Dar es Salaam – Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Zanzibar, Said Mzee, amesema kampeni ya ‘No Reforms, No Elections’ (bila mabadiliko hakuna uchaguzi) imekiimarisha chama hicho kwa kiasi kikubwa.
Mzee amesema kampeni hiyo imeimarisha imani ya wananchi kwa chama hicho katika kipindi ambacho viongozi wake wamekumbwa na vifungo na vikwazo vya kisiasa.
Kampeni ya No Reforms, No Election ni kauli mbiu ya Chadeama ambayo inalenga kusukuma mabadiliko kwenye mifumo ya uchaguzi, hasa katika Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC). Lengo la kampeni ni kuhakikisha mabadiliko yanatekelezwa kabla ya uchaguzi kufanyika.
Mzee ametoa kauli hiyo Januari 19, 2025 kupitia mkutano wa mtandaoni ulioandaliwa na Baraza la Wazee wa Chadema (Bazecha) ambao ulijikita kwenye historia ya Chadema upande wa Zanzibar katika kuadhimisha miaka 33 tangu kuanzishwa kwa chama hicho.
Kampeni Imekuwa ya Taifa
Kwa mujibu wa Mzee, kampeni hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa Chadema kuendelea kuwepo na kuwa imara licha ya mazingira magumu ya kisiasa iliyopitia.
"Moja ya sababu Chadema kinaendelea kuwepo licha ya kuwekwa kifungoni ni hii kampeni. Watanzania wametuamini pasipo shaka kuwa tunasemea shida na mateso yao, ndiyo maana wakaibeba ajenda hii," amesema Mzee.
Akizungumzia uanzishwaji wa kampeni hiyo, amesema viongozi wa chama walidhani wao ndio waliokuwa na uelewa mkubwa kuhusu changamoto za mfumo wa uchaguzi, lakini waligundua kuwa wananchi tayari walikuwa na uelewa mpana zaidi.
"Tulipoanza kampeni hii tulifahamu kuwa Watanzania walikuwa na uelewa mkubwa kuliko sisi. Matokeo yake ajenda hii ikahama kutoka kuwa ya Chadema na kuwa ya Watanzania wote," ameeleza.
Mabadiliko ya Katiba Yanahitaji Umoja
Akizungumzia suala la Katiba mpya, Makamu Mwenyekiti huyo amesema mabadiliko ya katiba yatafanikiwa kwa haraka endapo wazee na makundi ya kijamii yataungana bila kujali mgawanyo wao wa vyama vya siasa wala itikadi za kidini.
Kuhusu suala la maridhiano ya kisiasa, Mzee amesema hakuna dhamira ya kweli ya kufanikisha mchakato huo kwa sasa.
"Tumefungiwa kufanya siasa. Wanachama wawili wakikutana wanapewa kesi ya uhaini. Maridhiano hayawezekani katika hali hii," amesema.
Ameongeza kuwa Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu, ambaye angekuwa mstari wa mbele katika mazungumzo ya maridhiano, yupo gerezani, hali inayofanya mchakato huo kuwa mgumu zaidi kwa chama hicho.
Wasiwasi Kuhusu Tume ya Uchunguzi
Mzee pia amezungumzia Tume ya Uchunguzi iliyoundwa kuchunguza matukio ya siku na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, akisema mwenendo wa baadhi ya watu wanaojitokeza kwenye Tume hiyo kukihukumu Chadema haumtishi.
"Tume imeundwa kuchunguza yaliyotokea Oktoba 29, lakini kuna watu wanajitokeza kusema Chadema inahusika na hili au lile. Kwa nini wasiende kwenye Tume kutoa maoni yao badala ya kuita waandishi wa habari kuzungumza?" amehoji Mzee.