Watu Wanne Wafariki Kwa Kusombwa na Maji Mbeya, Jeshi la Zimamoto Latoa Onyo
Mbeya – Watu wanne wameripotiwa kufariki dunia baada ya kusombwa na maji jijini Mbeya, huku Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani humo likiwataka wananchi kuchukua tahadhari ya ziada kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Jeshi hilo limewasisitiza wananchi kuweka ulinzi maalum kwa watoto, wazee na wenye ulemavu wakati wa kipindi hiki cha mvua kubwa.
Aidha, Jeshi la Zimamoto limewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za majanga popote yanapotokea ili kuweza kuokoa maisha ya wananchi kwa wakati, huku likihakikisha kuwa liko tayari kutoa huduma wakati wowote.
Januari 2 mwaka huu, Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) ilitangaza uwepo wa mvua kubwa kwa siku 10 zitakazoambatana na ngurumo za radi, na Mbeya ikiwa miongoni mwa mikoa iliyotajwa.
Mrakibu Mwanadamizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mbeya, Malumbo Ngata, amesema hadi sasa watu wanne wamepoteza maisha kwa kusombwa na maji kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha.
Ngata amesema matukio ya kusombwa na maji yalianza Desemba 25 mwaka jana, huku wanaume watatu wakipoteza maisha, akiwemo mmoja aliyesombwa Januari 2 ambaye bado hajapatikana.
Ameeleza kuwa Jeshi la Zimamoto linaendelea na juhudi za kumtafuta mtu huyo katika mito mbalimbali, pamoja na mwanamke mmoja wa Mtaa wa Makunguru.
"Tunaendelea kumtafuta huyu aliyesombwa na maji, tangu Desemba 25 ni watu wanne waliosombwa kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha. Kuna aliyekutwa pale Mkulu inapojengwa barabara baada ya kudumbukia, mwingine alikuwa mwendesha pikipiki," amesema Ngata.
Kamanda huyo ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo, wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari wakati wote, na kufuatilia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa juu ya utabiri wa mvua.
Amesema tahadhari hizo ziendane sambamba na ulinzi kwa watoto, wazee na wenye ulemavu kuhakikisha wanakuwa salama, na kutoa taarifa kwa Jeshi la Zimamoto pale inapotokea tatizo kwani huduma zipo wakati wote.
"Tunavyo vifaa vya kisasa kutuwezesha kufika popote, wananchi watoe taarifa inapotokea majanga, lakini kwa kipindi hiki cha mvua wachukue tahadhari na kuwalinda watoto, wazee na wenye ulemavu," amesisitiza Kamanda huyo.
Benson Msuya mkazi wa Sokomatola amesema tukio la mwanamke kusombwa na maji limewashtua wengi, akiomba wazazi na walezi kuzingatia usalama wao na familia kwa ujumla ili kuepuka matukio kama hayo.
Naye Judith Methew amelipongeza Jeshi la Zimamoto kwa uwahi wake kwenye matukio, akiomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano ili kulinda usalama pale inapotokea majanga yoyote.