Mahakama Yahukumu Wafanyabiashara Wawili Kifungo cha Miaka 20 kwa Biashara Haramu ya Meno ya Tembo
Dar es Salaam – Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu wafanyabiashara wawili Mohamed Mbotoni (47) na Abdallah Pazi (54) kutumikia kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na kumiliki meno ya tembo yenye thamani ya Sh103 milioni, Mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia, Mahakama hiyo imetoa amri ya vipande hivyo nane vitaifishwa na kuwa mali ya Serikali, ambapo vitapelekwa Maliasili.
Washtakiwa hao wakazi wa Temeke Wiles, wanakabiliwa na shtaka moja la kusafirisha nyara hizo bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini.
Walitenda kosa hilo Mei 23, 2022 katika maeneo ya Uwanja wa Taifa, wilaya ya Temeke ambapo walikamatwa na vipande vinane vya meno ya tembo, vyenye thamani ya Sh103,099,000.05 (zaidi ya Sh103 milioni) bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini.
Hukumu Yatolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi
Hukumu hiyo imetolewa Ijumaa Januari 2, 2026 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, ambaye alisema kuwa mahakama imewatia hatiani washtakiwa kama walivyoshtakiwa.
Hakimu Mhini alisema upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi wanane na vielelezo kadhaa ambavyo vimeweza kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.
"Upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha mashtaka pasina kuacha shaka dhidi ya washtakiwa wote," alisema Hakimu Mhini.
Ushahidi Uliotolewa Mahakamani
Akipitia baadhi ya ushahidi, Hakimu Mhini alisema vipande hivyo vilikutwa nyumbani kwa Mbotoni vikiwa vimefichwa kwenye banda la kuku na wote walikuwa wanafahamiana.
Alisema Mbotoni alimualika Pazi nyumbani kwake ili waweze kujadiliana na kupanga mipango ya kufanya biashara ya meno ya tembo na kwamba hata Serikali ya mtaa inajua kuwa Mbotoni alikuwa anafanya biashara ya meno ya tembo.
Hata hivyo, Mei 23, 2022 kikosi kazi cha Kuzuia na Kupambana na Ujangili kilipata taarifa kuwa kuna watu wanafanya biashara ya meno ya tembo.
"Kikosi kazi kiliunda timu na mmoja wao alijifanya ni mnunuzi wa meno ya tembo na hivyo, siku hiyo mchana alimpigia simu Mbotoni na kukubaliana kuonana mchana maeneo ya Uwanja wa Taifa kwa ajili ya kuuziana meno ya tembo," alisema Hakimu.
Jinsi Washtakiwa Walivyokamatwa
Kikosi hicho kabla ya kwenda Uwanja wa Taifa kwa ajili ya kukutana na Mbotoni, walipita kituo cha Polisi Chang’ombe kwa ajili ya kutoa taarifa na kupewa hati ya ukamataji.
Baada ya hapo walienda Uwanja wa Taifa na kukutana na Mbotoni, walimkamata na kumuweka chini ya ulinzi, huku wakisubiri mjumbe wa Serikali za Mtaa wa eneo hilo.
"Baada ya hapo, walienda nyumbani kwa Mbotoni na kuanza upekuzi, ambapo mshtakiwa huyo alidai kuwa vipande nane vya meno ya tembo ameviweka katika banda ya kuku, hivyo waliongozana na maofisa hao na kuvichukua," alisema Hakimu, wakati akipitia baadhi ya mashahidi.
Mshtakiwa baada ya kuhojiwa alikiri kufanya biashara hiyo yeye na mwenzake Pazi na kisha hati ya ukamataji mali ilisainiiwa na washtakiwa walipelekwa kituo cha Polisi Chang’ombe kwa ajili ya mahojiano na baadae walifikishwa mahakamani.
Thamani ya Meno ya Tembo
Vipande hivyo ya meno, vilithibitishwa na ofisa wa wanyamapori kuwa vina thamani ya dola za Kimarekani 45,000 ambazo ni sawa na fedha ya Kitanzania Sh103 milioni.
Washtakiwa baada ya kusomewa maelezo hayo, walikubali majina yao, umri wao, dini zao, mahali wanaoishi na siku walipofikishwa mahakamani na wamekana mashtaka yanayowakabili.
Novemba 26, 2024 washtakiwa walisome shauri na kesi hiyo ilianza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka Januari 16, 2025.
Maombi ya Adhabu
Awali, kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Christopher Olembille, aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mujibu wa sheria kwa sababu utalii ni moja kati ya chanzo cha mapato kwa Serikali hivyo kuua wanyama kunahatarisha sekta hiyo.
Hata hivyo Mahakama iliwapa nafasi Mbotoni na Pazi kujitetea, ambapo washtakiwa hao waliomba wapunguziwe adhabu kwa kuwa wanayegemewa na familia zao.
Hakimu Mhini alisema kulingana na shauri alizotoa washtakiwa na upande wa mashtaka, mahakama hiyo inawapa adhabu ya kila mmoja kutumikia kifungo cha miaka 20 gerezani.
"Mahakama imewatia hatiani kama mlivyoshtakiwa na kwa kesi hii adhabu ya chini ni kifungo cha miaka 20 jela, hivyo Mahakama inawahukumu kila mshtakiwa kutumikia kifungo cha miaka 20 jela, ili iwe fundisho na haki ya kukata rufaa ipo wazi endapo hamjaridhika na uamuzi uliotolewa na mahakama hii," alisema Hakimu Mhini.