Vijana Wajipatia Ajira za Muda Wakati wa Sikukuu za Mwisho wa Mwaka
Dar es Salaam – Kadri shamrashamra za mwisho wa mwaka zinavyozidi kushika kasi, picha halisi ya namna vijana wanavyojitafutia kipato katika msimu wa sikukuu inaendelea kujitokeza, hususani maeneo ya mijini.
Kutoka masoko yenye msongamano hadi matamasha makubwa ya burudani, vijana wamekuwa wakijipatia ajira za muda mfupi zinazoibuka Desemba kila mwaka.
Kwa ujumla, ajira hizi za muda mfupi huwaingizia vipato vijana, hasa ambao hawapo kwenye ajira rasmi.
Licha ya kutokuwa na mikataba ya kazi, ajira hizi za muda huwasaidia kujiongezea kipato, kujenga mtandao wa wateja na kuongeza maarifa ya kazi kwa vitendo.
Ufuatiliaji uliofanywa na TNC katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam unaonesha ajira hizo za muda zimegawanyika katika makundi tisa, kila moja likiwa na nafasi ya kipekee katika kuongeza kipato cha vijana katika kipindi hiki ambacho matumizi ya kaya huongezeka.
Biashara Bidhaa za Sikukuu
Kariakoo, Ilala, Mwenge na Mbagala ni miongoni mwa maeneo ambayo ni kitovu cha ajira za muda mfupi.
Wauzaji wa nguo, viatu, mapambo na bidhaa za elektroniki wameongezeka katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwishoni mwa mwaka.
Baadhi ya wafanyabiashara wenye maduka hutoa bidhaa kwa mali kauli kwa vijana ambao hukabidhi fedha baada ya mauzo.
Hili linafanyika zaidi katika eneo la Kariakoo ambako watu wengi hufurika kwa ajili ya kufanya ununuzi, zikiwamo bidhaa za mavazi.
Katika msimu huu wa sikukuu, nguo na viatu vya watoto ndivyo huuzwa zaidi, wachuuzi wamewarahisishia wateja, badala ya kuingia dukani, baadhi huishia nje ambako bidhaa huuzwa mikononi.
"Ni uamuzi wako kama unataka kwenda dukani sawa, lakini nguo ni zilezile. Unaponunua kwangu unanisaidia kupata chochote kutoka kwa mwenye duka," anasema Seleman Kidunga, anayeuza nguo katika Mtaa wa Congo, Kariakoo.
Kidunga anasema kwa kufanya hivyo ana uhakika wa kupata Sh25,000 kwa siku, kwa kuwa kila nguo anayouza anapata kati ya Sh1,000 hadi Sh2,000.
Huduma za Upishi na Uchomaji Nyama
Huduma za upishi na uchomaji nyama ni eneo lingine linalotoa ajira za muda kwa vijana wengi wa mijini msimu wa sikukuu.
Kampuni za upishi huajiri wafanyakazi wa muda, kuanzia wapishi, wahudumu wa kusambaza chakula hadi waosha vyombo.
Kwa kiasi kikubwa, kampuni hizi hupata tenda za kuhudumu kwenye matamasha na mikusanyiko, huku wapishi binafsi wakipata ujira kwa kupika kwenye familia zenye uhitaji.
"Tenda huwa zinatokea, mtu anakwambia nina wageni wengi nahitaji chakula, mnakubaliana unampikia, unapeleka au unaenda kupika nyumbani kwake, mnalipana kulingana na makubaliano," anasema Ummy Kassim, mmiliki wa mgahawa eneo la Mbagala.
Clara John, mkazi wa Kimara, anasema sikukuu za mwishoni mwa mwaka humwingizia kipato kwa kuwa hupata ajira ya muda kwa mjasiriamali anayefanya kazi ya upishi kwenye sherehe na kwenye familia zinazohitaji huduma.
"Kazi yangu ni kupakua chakula na kuosha vyombo. Nashukuru Mungu hadi Januari baada ya sikukuu kwisha huwa sikosi Sh200,000, zinanisaidia kwa mahitaji ya shule ya watoto," anasema.
Matamasha na Michezo
Matamasha yanayofanyika hutoa ajira za muda kwa vijana, zikiwamo za ulinzi, uuzaji tiketi, kusimamia jukwaa na ubebaji vifaa.
Miongoni mwa matamasha hayo ni lile litakalofanyika mkoani Kilimanjaro kuanzia Desemba 22, 2025, linalofahamika kama Rombo Marathon na Ndafu Festival.
Tukio hilo huwakutanisha watu kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kwa takribani siku nne, likitengeneza fursa za biashara na ajira za muda kwa vijana, huku wengine wakiendeleza kukuza mitaji ya biashara zao.
"Hili siyo tamasha pekee, ni fursa ya watu kufanya utalii. Tutakuwa na mahema ya viwango tofauti, zitapatikana nyama zilizotengenezwa kwa viwango vya hali ya juu, na watoa huduma wamejipanga kuhakikisha watu wanafurahia shughuli hii," anasema Profesa Adolf Mkenda, mbunge wa jimbo la Rombo.
Si hilo pekee, yamekuwapo matamasha ya kidini ambayo hutoa ajira za muda kwa waandaaji, watengeneza tiketi kuna viingilio, wanaokodisha viti, mahema na hata wanaotoa huduma za chakula na vinywaji.
Usafi na Ukarabati wa Nyumba
Kwa baadhi ya watu, kuelekea sikukuu za mwishoni mwa mwaka hufanyika maandalizi ya kupokea wageni, hivyo kazi za kupaka rangi, kufagia, kupiga deki na kusafisha nyumba na mazingira yake huongezeka.
Wengine hufanya kazi za ujenzi na matengenezo ya nyumba kwa kuzipa mwonekano mpya.
Jeni Kondo, mkazi wa Tabata anayefanya kazi kwenye kampuni ya usafi, anasema nje ya zabuni ambazo kampuni yao hupata, binafsi kipindi hiki hupata kazi za usafi kwenye nyumba za watu binafsi.
"Baadhi ya wafanyakazi kwenye kampuni ambayo tumepata tenda ya kufanya usafi huwa wananipa kazi za majumbani kwao. Mtu anakwambia nina wageni nahitaji usafi wa nguvu, mnakubaliana mtakavyolipana kulingana na uzito wa kazi," anasema.
Huduma za Usafiri
Ongezeko la safari kuelekea mikoani linaakisi mahitaji ya nguvu kazi katika vituo vya mabasi na huduma za bodaboda na bajaji.
Baadhi ya vijana hujiajiri kwa kazi ya kupiga debe kuvutia abiria kupanda mabasi na kisha kulipwa ujira, huku wengine wakifanya kazi ya ukuli, kubeba mizigo ya abiria.
Fursa zaidi hupatikana kwa wenye magari ya kukodisha kwani, kutokana na ongezeko la abiria, Serikali imetoa vibali maalumu kwa magari hayo kubeba abiria kuwapeleka mikoani.
"Hivi sasa vijana wengi wanapata ajira kwenye hizi Coaster. Gari ni lazima liwe na dereva na kondakta. Kuna waliopata ajira kwa mlango huo, ukiondoa hawa ambao wanafanya shughuli zao kwenye mabasi ya mikoani, mawakala na wapiga debe ambao idadi yao huongezeka katika msimu wa abiria wengi," anasema Shaban Kitinile, wakala anayefanya shughuli zake Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli.
Biashara Mtandaoni
Kwenye mitandao ya kijamii, vijana wanaojihusisha na utengenezaji wa video za matangazo, uuzaji wa bidhaa za sikukuu na usambazaji wa matangazo kupitia WhatsApp, TikTok na Instagram hujipatia ajira za muda.
"Katika msimu huu, habari kubwa ni matangazo ya bidhaa zinazoshushwa bei na ofa mbalimbali zinazotolewa na wafanyabiashara kupitia huduma zao, hata utengenezaji wa maudhui unazingatia hilo," anasema msanii wa vichekesho na mtengeneza maudhui mtandaoni.
Biashara ya Mazao ya Chakula
Mazao kama mpunga, mahindi, matunda na mbogamboga huongeza idadi ya vijana wanaofanya kazi za kupakia na kupakua, kupima mazao na uuzaji.
"Katika kipindi hiki chakula huhitajika kwa wingi kwa sababu familia zinakuwa pamoja na mara nyingi kunakuwa na mikusanyiko, hivyo mzunguko wa biashara za vyakula unakuwa mkubwa wakati huu," anasema Deus Liogope, mfanyabiashara katika Soko la Temeke Stereo.
Utalii
Shughuli za utalii hutoa ajira nyingi zaidi kwa vijana msimu huu, zikiwamo za waongoza watalii, wapokeaji wageni na wahudumu wa hoteli.
Katika kipindi cha sikukuu za mwishoni mwa mwaka, utalii wa ndani huongezeka kutokana na baadhi ya familia kuwa na utaratibu wa kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii.
Hii hufanya maeneo hayo kuwa na uhitaji wa huduma muhimu, ikiwemo malazi, chakula na uongozaji, hivyo ajira hutengenezwa katika sekta hiyo.
Mapambo ya Sikukuu
Uuzaji wa miti ya Krismasi, taa, mapambo na zawadi hutoa ajira za muda kwa vijana.
Katika masoko na barabara mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam, wachuuzi huuza bidhaa na mapambo yanayotumika katika msimu huu.
Rashid Kamadi, mfanyabiashara wa mapambo anayefanya shughuli zake Kariakoo, anasema licha ya kutokuwapo kwa wateja wengi kwa sasa, hali hubadilika kuanzia Desemba 20.
"Huwa tunaanza kuuza mapema maana kuna wale ambao hufanya maandalizi kabla mambo hayajawa mengi. Hivi sasa wateja ni wachache, ila ni kawaida, wataanza kuwa wengi kuanzia Desemba 20 na kuendelea," anasema.