Mahakama Kuu Yatupilia Mbali Kesi ya Madai ya Sh15 Bilioni Dhidi ya Zitto Kabwe
Dar es Salaam – Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali kesi ya madai ya zaidi ya shilingi bilioni 15 iliyofunguliwa na mfanyabiashara Harbinder Sethi dhidi ya mwanasiasa Zitto Kabwe.
Katika shauri hilo, Sethi alidai kuwa ndiye mwenye hisa nyingi katika Kampuni ya Pan Africa Power Solution (PAP) iliyosajiliwa Tanzania na kwamba PAP inamiliki Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Zitto Kabwe, aliyewahi kuwa Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, alifunguliwa kesi ya madai ya kumkashifu Sethi kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii tarehe Aprili 4, 2025.
Hukumu ya Mahakama
Katika hukumu aliyoitoa Desemba 11, 2025 na kupakiwa kwenye mtandao wa mahakama Desemba 13, Jaji Arnold Kirekiano amesema mwombaji hajathibitisha kesi kwa kiwango kinachohitajika. Hivyo shauri hilo linatupiliwa mbali na mleta shauri atatakiwa kulipa gharama za kesi.
Maudhui Yaliyosababisha Shauri
Zitto aliandika kwenye ukurasa wake: "Kwanza naunga mkono msimamo wa uongozi wa Shirika la Tanesco kwamba imekwishamalizana na IPTL na hivyo haina madai yoyote kutoka kwa tapeli yeyote anayejiita mmiliki wa IPTL."
Aliendelea kusema: "Hivyo basi kitendo cha Bwana Singh Sethi kuendelea kudai kumiliki IPTL na kuisumbua Serikali na Tanesco ni utapeli wa wazi kwa kuwa hautokani na sheria wala amri yoyote ya mahakama."
Zitto pia aliandika: "Brela (Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni) wanapaswa kufuta usajili wa Kampuni ya IPTL na takataka zingine zote zinazohusiana na IPTL. Mzoga huu sasa uzikwe."
Madai ya Fidia
Kutokana na maandishi hayo, Sethi alifungua shauri la madai ya kashfa dhidi ya Zitto akidai matamshi yalitolewa kwa nia mbaya, bila sababu au uhalali wa kisheria. Pia yalimweka katika chuki, dharau na kejeli kutoka kwa umma, wawekezaji wengine na jamii yake.
Katika shauri namba 8810 la mwaka 2025, Sethi aliomba mahakama itamke kuwa Zitto alimkashifu na kwamba matamshi na chapisho lake ni la uongo na lenye madhara.
Aliomba mahakama imwamuru Zitto aombe radhi bila masharti na kuondoa uchapishaji kupitia jukwaa aliloolitumia. Vilevile aliomba Zitto achapishe tangazo la kuomba radhi katika magazeti kwa wiki nzima na kutoa matangazo kupitia televisheni na redio maarufu nchini.
Sethi aliomba mahakama imwamuru Zitto kumlipa shilingi bilioni 10 zikiwa ni fidia ya kashfa na uharibifu wa sifa, pamoja na shilingi bilioni 5 kwa hasara ya kashfa na madhara ya msongo wa mawazo.
Majibu ya Zitto Kabwe
Zitto aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC), alikana kufanya jambo lolote baya akieleza aliyochapisha ni ya kweli, aliyatoa kwa nia njema na ni maoni ya haki kuhusu masuala yenye masilahi makubwa ya umma.
Alihusisha maoni yake na haki ya uhuru wa kujieleza, akakana madai ya nafuu iliyoombwa, akiiomba mahakama kufuta shauri hilo.
Zitto alieleza katika kipindi cha ubunge alihudumu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na POAC kwa miaka minane mfululizo na zilipewa jukumu la kuchunguza kashfa iliyohusisha IPTL na PAP.
Alieleza machapisho yake katika mitandao ya kijamii aliyaandika kama sehemu ya mjadala wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo ilijadiliwa Bungeni.
Alieleza yeye kama mwananchi na mtu aliyefahamu vizuri suala hilo, alikuwa na haki na wajibu wa kutoa maoni kutokana na mjadala wa ripoti ya CAG.
Uamuzi wa Mahakama
Jaji Kirekiano amesema ni jambo la kawaida kwamba mzigo wa uthibitisho uko kwa mlalamikaji anayefungua kesi, anayepaswa kuthibitisha madai yake.
Jaji amesema amezingatia madai ya mleta maombi kuwa chapisho lilikuwa na nia mbaya na msimamo wa Zitto kwamba maoni yake hayakuwa na hasidi ndani yake bali aliyatoa kwa haki na alikuwa na wajibu huo.
"Katika hali hii ya ukweli, pamoja na ushahidi usiopingika kwamba suala la umiliki wa IPTL lilikuwa ni suala la uchunguzi wa Bunge, suala hili kwa kiasi kikubwa lilikuwa ni la masilahi ya umma," amesema Jaji.
Jaji amesema mleta maombi hajathibitisha katika kiwango kinachohitajika kuwa chapisho lilikuwa la uongo na hasidi, hivyo hakukuwa na nia ovu na chapisho halikuwa la uongo.
Jaji alieleza kuwa Sheria ya Huduma za Habari 2016 inasema chapisho linaweza lisiwe la kashfa kama suala lililoandikwa ni la kweli na lina masilahi ya umma.
Baada ya maelezo hayo, Jaji amesema mleta maombi ameshindwa kuthibitisha madai yake kwa kiwango kinachokubalika, hivyo kesi inatupwa na atawajibika kulipa gharama.