Ajali ya Lori Dodoma: Miili Yote Mitano Imetambuliwa na Kuchukuliwa na Jamaa
Dodoma – Miili yote mitano ya madereva wa bodaboda waliofariki dunia kwa ajali ya kugongwa na lori lililofeli breki eneo la Dodoma Makulu imetambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao kwa ajili ya mazishi.
Ajali mbaya hiyo ilitokea saa 2:30 usiku wa Desemba 11, 2025 wakati madereva wa pikipiki walikuwa kwenye kijiwe chao cha Amani, wakisubiri wateja.
Waliofariki wametambuliwa kuwa ni Ishadi Jaa (25), Hafidhi Selemani (30), Adam Juma (27), Ijumaa Ndafu (27) na Michael Mkande (26).
Ndafu alizikwa Desemba 12 kwenye makaburi yaliyopo Dodoma Makulu, huku mwili wa Ishadi Jaa ukisafirishwa kwa maziko mkoani Arusha.
Renatha Mzanje, Ofisa Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma, amesema marehemu wote watano waliopokewa hospitalini wametambuliwa na miili yao imechukuliwa na jamaa zao.
"Miili yote mitano imetambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao kwa ajili ya mazishi. Suala la wanazikwa wapi hatujui maana hiyo ni mipango ya familia. Tunaweza kusema wanazikwa Dodoma lakini wanafamilia wakaamua kusafirisha," amesema Mzanje.
Dereva Anaendelea Kutafutwa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera, amesema dereva aliyesababisha ajali hiyo bado anaendelea kutafutwa baada ya kukimbia kutoka eneo la ajali.
Hyera amesema mbali ya watu watano waliofariki dunia, utingo wa lori lililosababisha ajali alijeruhiwa na kuwa anapata matibabu. Mzanje ameeleza kuwa hali ya utingo huyo inaendelea vizuri.
Athari nyingine zilizotokana na ajali hiyo ni pamoja na uharibifu wa pikipiki na uzio wa nyumba iliyo jirani na barabara ambao uligongwa na lori hilo.
"Eneo hilo la barabara lina mteremko mkali, hivyo madereva ni lazima waendeshe mwendo wa tahadhari ili inapotokea changamoto yoyote waweze kuepusha maafa yanayoweza kuzuilika, tofauti na wanavyokuwa kwenye mwendo mkali," amesema Kamanda Hyera.
Hyera amesema kutokana na eneo hilo kuwa la hatari kwa waendesha vyombo vya moto na watembea kwa miguu, Jeshi la Polisi litaimarisha usalama, wakati mamlaka nyingine ikiwamo Tanroads zikifanya jitihada za kuepusha ajali.