Shauri la Uchaguzi Lafunguliwa Kupinga Ushindi wa Zungu Ilala
Dar es Salaam. Aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Ilala katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Friday Yachitwi, amefungua shauri la uchaguzi akipinga ushindi wa Mussa Azan Zungu wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Baadhi ya malalamiko yake ni madai ya kukithiri kwa wizi wa kura na upigaji wa kura bandia, kiasi kwamba idadi ya kura zote imepita idadi ya wapiga kura waliojiandikisha katika jimbo la Ilala, mkoani Dar es Salaam.
Zungu mbali na ubunge, pia alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kupata kura 378 kati ya kura 383 zilizopigwa na wabunge.
Katika shauri hilo la uchaguzi namba 000030602 la mwaka 2025, Yachitwi anayewakilishwa na wakili Jasper Sabuni, amemshitaki Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ilala kama mlalamikiwa wa kwanza na Zungu mlalamikiwa wa pili.
Vilevile, amemuunganisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kama mlalamikiwa wa tatu. Shauri hilo limepangwa kutajwa Desemba 18, 2025 mbele ya Jaji Mary Moyo wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Yachitwi anaiomba mahakama itoe amri ikitamka kuwa uchaguzi uliompa Zungu ushindi ni batili kwa kuwa ulikiuka masharti ya Sheria ya Uchaguzi na Kanuni za Uchaguzi za 2025.
Pia anaiomba mahakama itoe agizo kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kuitisha uchaguzi mdogo wa mbunge Jimbo la Ilala ndani ya siku 30 tangu tarehe ya uamuzi wa shauri hilo na gharama za kesi zibebwe na walalamikiwa.
Mlalamikaji anasema yeye ni mmoja wa wagombea ubunge jimbo la Ilala na kwa kuwa hakuridhika na matokeo ya uchaguzi wenyewe na mwenendo mzima wa uchaguzi huo, anaiomba mahakama itamke kuwa uchaguzi huo ulikuwa batili.
Sababu za Kupinga Ushindi wa Zungu
Katika hati ya madai, mlalamikaji anaitaka mahakama isikitishe matokeo ya uchaguzi katika jimbo la Ilala yaliyoidhinishwa na mdaiwa wa kwanza kwa tarehe isiyojulikana kuwa Zungu amechaguliwa dhidi ya mlalamikaji.
Kulingana na mazingira tete ya kiusalama tangu siku ya uchaguzi, anadai msimamizi alimwidhinisha mgombea wa CCM kimyakimya bila ya yeye kushirikishwa, kuhusishwa wala kupewa taarifa yoyote kama sheria na kanuni za uchaguzi zinavyotamka.
Anadai kuwa, msimamizi wa uchaguzi ama watumishi wake, mawakala au wafanyakazi walio chini yake, walitoa matokeo yasiyozingatia mchakato wa uchaguzi unaolindwa na sheria, kukubalika, uliodhamiriwa na wa kuaminika.
Anadai hiyo ndiyo ilikuwa ahadi yake lakini badala yake alipitisha mchakato ambao ulishindwa kwa kiasi kikubwa, uliharibu chaguo na uamuzi wa watu wa Ilala au ambao ungeweza kuwa chaguo na uamuzi katika uchaguzi unaobishaniwa.
Yachitwi anadai kwa ujumla, vitendo vyote hivyo vya ukiukaji wa Katiba na sheria vilivyofanywa na msimamizi wa uchaguzi au walio chini yake, hakuna idadi ya kura halali zilizopigwa, hivyo Zungu hakupaswa kutangazwa kuwa mbunge.
"Pamoja na vitendo vingi visivyofaa vilivyotokea Oktoba 29, 2025, hapakuwapo idadi ya kura halali zilizopigwa na kwa hivyo (Zungu) hakupaswa kutangazwa kuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," analalamika Yachitwi.
Malalamiko ya Mawakala na Mchakato wa Kupiga Kura
Mlalamikaji anadai kutofuatwa sheria ya uchaguzi na kanuni zake za 2025 pamoja na mwongozo unaoelekeza mawakala walioidhinishwa kuwapo kwenye vituo vya kupigia kura, lakini msimamizi, aliwachelewesha bila sababu za msingi.
"Waliwachelewesha kuingia vituoni kwa saa kadhaa baadhi ya mawakala wa mlalamikaji, huku upigaji kura ukiendelea licha ya maombi ya mara kwa mara kuwa mawakala hao waingizwe vituoni," amedai.
Analalamika kuwa vitendo hivyo viliathiri masilahi yake ya kiuchaguzi na kwamba, vitendo hivyo vya mlalamikiwa wa kwanza (msimamizi) viliathiri haki ya mlalamikaji katika kulinda masilahi yake katika vituo vya kupigia kura.
Pia, analalamika kuwa mlalamikiwa wa kwanza ama mawakala wake au watumishi walio chini yake, waliruhusu upigaji holela wa kura usiozingatia sheria, taratibu na kanuni ikiwa ni pamoja na mtu mmoja kupiga kura zaidi ya moja.
Hayo kwa mujibu wa mlalamikaji, yalitokea katika kata za Kivukoni, Kisutu, Upanga Mashariki, kwenye ofisi ya mtendaji kata ambapo maofisa wa msimamizi walikuwa wakitumbukiza kura kiholela kwenye masanduku ya kupigia kura vituoni.
Anadai Kata ya Kisutu kituo cha Sekondari ya Jamhuri na Gerezani ni maeneo ambayo mlalamikaji pamoja na mashahidi wake walishuhudia kasoro hizo.
Mlalamikaji anadai hayo yalifanyika pia katika vituo vya shule za msingi Bunge na Uhuru.
Yachitwi anadai muda wa kupiga kura ni kuanzia saa moja asubuhi mpaka saa 10:00 jioni, lakini katika kata za Mchikichini, Jangwani, Ilala, Upanga Magharibi na Upanga Mashariki, uchaguzi ulivurugika saa 6:00 na 7:00 mchana na ulisitishwa.
Malalamiko ya Uthibitisho wa Matokeo
Analalamika kuwa, maofisa wasimamizi wa vituo vya kupigia kura vya kata za Gerezani, Kivukoni, Mchikichini, Jangwani, Ilala, Upanga Mashariki, Mchafukoge na Kisutu, hawakuthibitisha idadi ya kura zote zilizopigwa.
Mbali na hayo, anadai maofisa wasimamizi wa vituo hivyo hawakuthibitisha mbele ya wagombea au mawakala, kwamba kuna usawa kati ya karatasi za kura zilizopokelewa, idadi ya wapigakura na karatasi zilizotumika.
Pia, analalamika kuwa maofisa wasimamizi katika vituo hivyo hawakuhesabu kwa sauti kubwa, kuzirekodi wala kuoanisha na kura kwenye sanduku, ikilinganishwa na idadi ya wapigakura kama sheria inavyoelekeza.
Anadai maofisa hao katika vituo vingi vya jimbo la Ilala, hawakuwapa mawakala wake nakala ya fomu ya matokeo na wala hawakumpa wakala wake wa majumuisho taarifa ya majumuisho ya kata.
Madai ya Ukiukaji wa Katiba
Katika shauri hilo, mlalamikaji anadai msimamizi wa uchaguzi au watumishi walio chini yake walikiuka Katiba, walishindwa kusimamia mifumo ambayo ni sahihi, salama na inayoweza kuthibitishwa na kuwajibika na uwazi na ukweli.
Badala yake, anadai walitangaza matokeo ambayo katika hali nyingi hayakuwa na uhusiano na kura zilizopigwa kwenye vituo, walitengeneza mbinu ambazo hazina uwazi na kutengeneza matokeo kipindi ambacho mawakala wake walitengwa.
Anadai chini ya sheria iliyoanzisha INEC, msimamizi wa uchaguzi ana wajibu wa kuzingatia masharti ya Katiba, sheria, kanuni za kidemokrasia na utawala bora katika matendo na uamuzi wake ikiwa ni pamoja na kumtangaza aliyeshinda.
Mbali na hayo, anadai kuwa maofisa wa msimamizi wa uchaguzi, walikithiri wizi wa kura na upigaji wa kura bandia kiasi kwamba hesabu ya kura zote imepita idadi ya wapigakura waliojiandikisha katika jimbo hilo.
Kwamba makosa aliyoyaeleza, anadai hayakuwa chochote isipokuwa ni mchezo wa makusudi, ulioratibiwa vizuri na kutekelezwa na msimamizi kwa lengo kuu la kumsaidia Zungu kinyume cha Katiba na sheria.
"Mlalamikaji anawasilisha kwamba, makosa yaliyotajwa hapo juu, uharamu na kutofuata utaratibu kulikopitiliza viliathiri matokeo ya uchaguzi kwa upande wa mlalamikaji," anadai katika hati ya malalamiko ya shauri hilo.
Ameieleza mahakama kwa masilahi ya haki na ya wapigakura katika jimbo la Ilala, matokeo yaliyompa ushindi Zungu yatangazwe kuwa batili na msimamizi apewe amri ya kuitisha uchaguzi mdogo kutokana na makosa hayo.