Wizara ya Kilimo Zanzibar Yakabiliwa na Upungufu wa Wataalamu Pemba
Unguja – Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar imekabiliwa na changamoto kubwa ya upungufu wa wataalamu wa kilimo na vitendeakazi wakati wa ziara yake Pemba.
Kutokana na hali hiyo, wizara imejitolea kutafuta njia bunifu za kutumia wataalamu na vitendeakazi vilivyopo kwa ufanisi zaidi bila kuongeza gharama za ziada.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk Salum Soud Hamed, amelitoa taarifa hilo Jumanne Desemba 9, 2025 wakati akitembelea taasisi na vituo mbalimbali vya wizara katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Dk Salum ameeleza kuwa kutokana na upungufu wa wataalamu, kuna haja ya kupanga upya maeneo ya kilimo kwa kuanzisha mpangilio maalumu wa upandaji miti ya matunda na kuimarisha vitalu vya uzalishaji miche ili kuzuia wadudu wasiharibu mbegu.
"Naipongeza menejimenti ya wizara kwa kuandaa ziara ambayo imetoa mwanga juu ya mafanikio na maeneo yanayohitaji kuimarishwa. Serikali itatafuta njia bunifu za kutumia wataalamu waliopo kwenye idara tofauti ili kuongeza ufanisi," amesema.
Wizara Yadhamiria Mageuzi ya Sekta ya Kilimo
Waziri wa wizara hiyo, Suleiman Masoud Makame, amethibitisha azma ya kufanya mageuzi makubwa ya sekta ya kilimo kwa kuimarisha maeneo ya uzalishaji ili kuhakikisha uhakika wa chakula nchini.
Ameeleza kuwa ziara hiyo imelenga kutambua maeneo yanayomilikiwa na wizara, kuyapima kimafanikio, kubaini changamoto zilizopo na kuhakikisha utekelezaji wa majukumu unakwenda sambamba na malengo ya Serikali.
"Katika maeneo yote tuliyotembelea yapo mafanikio lakini tunahitaji kufanya kazi kubwa ya kuimarisha sekta hizi. Serikali haiwezi kuwa na ardhi ambayo haitumiki wakati ina mahitaji makubwa," alisema Waziri.
Ameongeza kuwa changamoto nyingi zinahitaji hatua za haraka kwani maeneo mengi yanayomilikiwa na wizara hayatumiki ipasavyo, jambo linalochangia uvamizi na kurudisha nyuma juhudi za Serikali.
Watendaji Wapongezwa kwa Ziara
Msimamizi Idara ya Kilimo, Mbarouk Ali Mgau, amethibitisha changamoto za upungufu wa wafanyakazi na vitendea kazi, ambazo zinakwamisha kasi ya maendeleo katika sekta.
Hata hivyo, amesema hatua zimeshaanza kuchukuliwa ili kuleta mafanikio ndani ya sekta.
Amewapongeza viongozi kwa kutembelea maeneo ya kazi, akisema ni mara ya kwanza tangu walipoteuliwa kushika nyadhifa hizo.
Katibu Mkuu wa wizara, Saleh Mohamed Juma, amewataka watendaji kuimarisha nidhamu ya kazi, kuwahi kazini na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.