Polisi Songwe Yakanusha Madai ya Kutekwa kwa Viongozi wa Chadema
Songwe – Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limekanusha madai ya kutekwa kwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani humo, Isakwisa Lupembe, pamoja na Meya mstaafu wa Tunduma, Ally Mwafongo, na kubainisha kuwa viongozi hao wako mikononi mwa polisi wakichunguzwa kwa tuhuma za vitendo vya kihalifu.
Mvutano ulizuka baada ya taarifa kusambaa mitandaoni zikidai kuwa Lupembe na Mwafongo walikamatwa usiku na watu waliodai kuwa askari polisi.
Taarifa hizo zilieleza kuwa viongozi hao walichukuliwa usiku na hadi alfajiri hawakuonekana katika vituo vya polisi, hali iliyosababisha taharuki miongoni mwa wanachama na wananchi.
Madai yalitolewa mitandaoni yakidai kuwa chama hakijafanikiwa kufahamu walikopelekwa viongozi hao, na wito ulitolewa kwa viongozi wa dini na wadau wa haki za binadamu kufuatilia suala hilo.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi, kupitia taarifa yake iliyotolewa leo Desemba 7, 2025, iliyosainiwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Songwe, Augostino Senga, limekanusha madai hayo na kueleza kuwa watuhumiwa hawakutekwa, bali walikamatwa na askari waliokuwa kwenye operesheni maalumu.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa viongozi hao wanashikiliwa kwa tuhuma za kushiriki katika makundi ya mtandaoni yanayodaiwa kuhamasisha uchochezi, kusambaza uzushi na uongo, na kuchonganisha jamii kwa kutumia kisingizio cha uhuru wa kujieleza.
Polisi imewataka wananchi kutoa taarifa sahihi na kuepuka kusambaza habari zinazoweza kutia hofu katika jamii, huku ikisisitiza kuwa uchunguzi unaendelea na hatua za kisheria zitachukuliwa mara upelelezi ukikamilika.