Matokeo ya Darasa la Saba 2025: Ufaulu Wafikia Asilimia 96.94 Zanzibar
Unguja – Watahiniwa 50,769 sawa na asilimia 96.94 wamefaulu katika mtihani wa darasa la saba mwaka 2025, ukionesha uimarishaji wa ubora wa elimu Zanzibar.
Ufaulu umepanda kwa asilimia 0.28 ikilinganishwa na mwaka 2024, ambao asilimia ya ufaulu ilikuwa 96.66.
Vilevile, ufaulu wa chini umepungua kwa asilimia 0.28 ikilinganishwa na asilimia 3.34 mwaka 2024, huku ufaulu wa watahiniwa wa jinsi kike ukiwa juu kwa asilimia 52.36 kulinganishwa na watahiniwa wa kiume, ambao ni asilimia 47.64.
Taarifa Rasmi ya Matokeo
Taarifa ya matokeo hayo imetolewa leo Jumamosi Desemba 6, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Mitihani Zanzibar, Rashid Abdul-aziz Mukki katika ukumbi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Mazizini, Unguja.
Amesema watahiniwa 53,456 walisajiliwa kufanya mtihani huo, wanawake walikuwa 27,144 sawa na asilimia 50.78 na wanaume walikuwa 26,312 sawa na asilimia 49.22.
Ongezeko la Watahiniwa
Rashid amesema watahiniwa 6,508 sawa na asilimia 12.17 wameongezeka ikilinganishwa na watahiniwa 46,948 waliosajiliwa mwaka 2024. Ameeleza watahiniwa 46,896 walisajiliwa kutoka shule za Serikali na 6,560 za binafsi.
"Watahiniwa 52,374 walifanya mtihani, kati yao wanawake 26,862 sawa na asilimia 51.29 na wanaume 25,512 sawa na 48.71. Watahiniwa 6,353 (asilimia 13.81) wameongezeka ikilinganishwa na mwaka 2024," amesema.
Amesema watahiniwa 45,845 wametoka shule za Serikali na 6,529 kutoka za binafsi.
Suala la Watahiniwa Watoro
Rashid amesema watahiniwa 1,082 hawakuhudhuria kufanya mitihani, asilimia 73.94 ya watoro ni wanaume na asilimia 26.06 wanawake. Idadi ya watahiniwa watoro imeongezeka kwa asilimia 16.72 ikilinganishwa na watahiniwa 927 ambao hawakufanya mitihani mwaka 2024.
Amesema Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi inaongoza kwa kuwa na watahiniwa 212 watoro.
Vituo vya Mitihani
Rashid amesema vituo 514 vya mitihani vilisajiliwa, kati ya hivyo 299 ni vya Serikali na binafsi 215, ikiwa ni ongezeko la vituo 36 kulinganisha na vituo 478 vilivyosajiliwa mwaka 2024.
Mkurugenzi huyo amesema, wakati wa usahihishaji mitihani lilijitokeza tukio la kuandikwa kwa lugha za matusi, akieleza hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya wahusika.
Uchambuzi wa Madaraja
Ameeleza kuwa, ufaulu wa madaraja ya A, B na C umeimarika kwani watahiniwa 314 sawa na asilimia 0.60 wamefaulu kwa wastani wa daraja la A, ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.1.
Vilevile, watahiniwa 5,975 sawa na asilimia 11.41 wamefaulu kwa wastani wa daraja B ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.95 na watahiniwa 21,839 sawa na asilimia 41.70 wamefaulu kwa wastani wa daraja C.
Watahiniwa 22,641 sawa na asilimia 43.23 wamefaulu kwa wastani wa chini ya daraja D na wanafunzi 1,605 sawa na asilimia 3.06 wamepata wastani usioridhisha wa daraja F.
Ufaulu kwa Masomo
Akizungumzia ufaulu kwa masomo, amesema somo la sanaa za ubunifu na michezo lina ufaulu wa juu wa asilimia 99.02 na hisabati lina ufaulu wa asilimia 59.69, ukiwa umepanda kwa asilimia 4.17 kulinganisha na mwaka 2024 ulipokuwa asilimia 55.52.
Watahiniwa Wenye Mahitaji Maalumu
Ameeleza watahiniwa 296 walisajiliwa wakiwamo watano wasioona, wenye ulemavu wa viungo 22, ulemavu mchanganyiko wanne, viziwi 38, ulemavu wa akili 85 na uoni hafifu 142.
Amesema wanafunzi wenye uoni hafifu wameongezeka kwa asilimia 94.52.
Ufaulu unaonyesha kati ya watahiniwa 294 wenye mahitaji maalumu 280, wakiwemo watano wasioona, ulemavu wa viungo 19, viziwi 36, uoni hafifu 136, ulemavu mchanganyiko watatu na ulemavu wa akili 85 wamefaulu mitihani yao.
Shukrani kwa Wadau
Ameupongeza uongozi wa Wizara ya Elimu kwa kuendelea kuimarisha na kusimamia upatikanaji wa huduma ya elimu kwa wananchi wa Zanzibar.
"Shukrani za dhati kwa wazazi na walimu kwa kuhakikisha watahiniwa wanafika vituoni kufanya mitihani yao kwa ukamilifu," amesema.