Meya wa Mbeya Ataka Madiwani Kujenga Umoja na Kuheshimiana
Mbeya – Meya wa Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa, amewataka madiwani kujenga heshima kwa viongozi wa chama na Serikali kwa kuhepuka majungu, mifarakano na kuwa sehemu ya kuijenga halmashauri mpya.
Katika hatua nyingine, ametangaza msamaha kwa wale waliomkosea kwa kufungua ukurasa mpya wa safari ya miaka mitano na kuwahakikisha kutoa ushirikiano.
Issa amesema hayo Desemba 5, 2025, mara baada ya kutangazwa kushika nafasi hiyo kwa awamu ya pili na kuwa miongoni mwa madiwani walioapishwa kwenye kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa City Peack jijini Mbeya.
Kikao hicho kilihusisha madiwani 45 kati ya 55 wa Jimbo la Mbeya Mjini na Uyole sambamba na kufanya uchaguzi wa Meya, Naibu Meya na kamati maalumu za kudumu.
"Baraza hili linapaswa kuwa la mfano. Tulinde heshima za viongozi na wabunge kwa kutambua tuna majimbo mawili. Watatushangaa wakiona tunafarakana badala ya kuwa wamoja katika kuleta chachu ya kuibua miradi mipya yenye mchango kwa halmashauri," amesema.
Katika hatua nyingine, ametumia fursa hiyo kutangaza msamaha kwa wale waliomkosea na wanahisi aliwakosea kumsamehe huku akisisitiza hataki majungu na kwamba anamtegemea Mungu.
"Madiwani wenzangu ambao mmechaguliwa kwenye kamati msiwe chanzo cha kutugawa au kugawanyika. Kama ujapata leo, kesho utapata ni suala la muda. Cha msingi ni kushirikiana ili kuwa na baraza la madiwani la mfano," amesema.
Kufunga Milango ya Majungu
Issa amesema anafunga milango ya kupokea majungu na kuhitaji madiwani kujenga hoja za kuleta maendeleo katika Jimbo la Mbeya Mjini na Uyole.
"Ndugu zangu, kwangu milango ya majungu naifunga. Sitataka kuona diwani mmoja ananiletea hadithi za diwani mwingine, lakini atakayenisema aseme. Mimi namtegemea Mungu," amesema.
Meya amesema umefika wakati madiwani kuheshimiana kwa kuondoa makundi na kutozitwisha mzigo kamati za Chama cha Mapinduzi (CCM), kuwa sehemu ya kukaa kusuluhisha kesi mara kwa mara.
Onyo kwa Madiwani
Katibu Tawala Wilaya ya Mbeya, Mohamed Aziz, amewaonya madiwani kuondoa tofauti zao na kuwataka kwenda kwa wananchi kusikiliza na kutatua kero zao.
Amesema hatua ya kula kiapo ni kujidhihilisha wanakwenda kushirikiana na halmashauri katika kuleta maendeleo sambamba na kuhakikisha wanawafikia wananchi.
"Madiwani ondoeni tofauti zenu. Nendeni mkaunge mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan. Tumeona na kusikia hotuba yake siku akiongea na wazee, ameonyesha wapi tumetoka na tuendako kwa masuala mapana ya nchi," amesema.
Diwani wa Kata ya Nsalaga, Clement Mwandemba, amesema ni wakati wa kuwatumikia wananchi kwa kuwafikia kuona changamoto hususani kwa kundi la vijana.
"Tumefika hapa kwa kuaminiwa na wananchi. Jukumu letu ni kurejea tena kukaa chini kuzungumza na kujua wapi panahitaji kuwekwa sawa," amesema.