Sunday, December 7, 2025
  • Login
No Result
View All Result
Instagram
TNC
  • Home
  • Home
No Result
View All Result
TNC
No Result
View All Result

Ulinzi ulivyoimarishwa Dar

by TNC
December 6, 2025
in Swahili
0
0
SHARES
2
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Ulinzi Umeimarishwa Jijini Dar es Salaam Kuelekea Desemba 9

Dar es Salaam – Ulinzi umeimarishwa katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, hali inayoonekana wazi siku hizi.

Kwa kadri siku zinavyosonga, mabadiliko makubwa yamejitokeza kwenye baadhi ya mitaa hali ya ulinzi ikiimarishwa, kuelekea Desemba 9, siku iliyotajwa kutakuwa na maandamano.

Kila uchao idadi ya askari wa Jeshi la Polisi na wale wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wanaongezeka mitaani.

Awali, hali hiyo ilishuhudiwa wakati na baada ya vurugu zilizoambatana na maandamano yaliyofanyika Oktoba 29, 2025 siku ulipofanyika uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais.

Katika tukio hilo, baadhi ya watu walipoteza maisha, huku mali za wananchi na miundombinu ya umma vikiharibiwa na nyingine kuchomwa moto.

Kwa kadri siku zilivyosonga, askari kutoka majeshi hayo walianza kupungua mtaani polepole baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuagiza shughuli ziendelee kama kawaida, kabla ya kuanza kuonekana tena mwanzoni mwa wiki hii.

Vituo vya Ulinzi Vimeimarishwa

Kwenye Barabara ya Morogoro, askari wa Jeshi la Polisi na wale wa JWTZ wakiwamo wenye silaha wanaonekana kwenye vituo vya mwendokasi wakiimarisha doria. Baadhi ya vituo hivyo viliharibiwa kwa kuvunjwa au kuchomwa moto Oktoba 29.

Vilevile, wamekuwapo kwenye maeneo ya madaraja na miundombinu mingine ya umma, likiwamo Daraja la Juu la Kijazi, wilayani Ubungo, ambako yamekuwa yakionekana magari ya Polisi pamoja na JWTZ.

Hali ni vivyo hivyo kwenye barabara zingine za jiji ikiwamo Sam Nujoma, kutokea Ubungo hadi Mwenge; Buguruni, Tazara kwenye barabara ya Mandela.

JWTZ walikuwapo makao makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na maeneo jirani na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na maeneo ya barabara ya Bagamoyo.

Hali ya uimarishaji ulinzi imeshuhudiwa pia katika barabara za Kilwa na Nyerere hususan eneo la Uwanja wa Ndege pamoja na katikati ya Jiji.

Taarifa ya Jeshi la Polisi

Hayo yakiendelea, Jeshi la Polisi katika taarifa kwa umma iliyotolewa Desemba 5, 2025 limesema hali ya usalama wa nchi inaendelea kuimarika siku hadi siku, huku likiendelea kutimiza majukumu yake ya msingi, likiwamo la kuhakikisha linasimamia uwepo wa amani, utulivu na usalama.

"Katika hili, Jeshi la Polisi linatoa shukrani kwa wananchi na wadau mbalimbali wanaoendelea kutoa ushirikiano kwa kiwango kikubwa katika kulinda na kuimarisha amani nchini," imesema taarifa hiyo iliyotolewa na Msemaji wa jeshi hilo, David Misime.

Akirejea taarifa ya awali ya jeshi hilo iliyotolewa Desemba 3, 2025, Misime amesema upo uhalifu unaoendelea kupangwa na kuhamasishwa kwenye mitandao ya kijamii na kwenye makundi ya baadhi ya watu wakihamasisha alichosema wanachokiita maandamano ya amani na yasiyo na kikomo kuanzia Desemba 9, 2025.

"Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama linaendelea kuchukua hatua stahiki dhidi ya uhalifu huo unaopangwa, hivyo wananchi msiwe na hofu," amesema.

Masharti ya Kisheria ya Maandamano

Amesema sheria za nchi, ikiwemo Sheria ya Polisi na Polisi Wasaidizi Sura ya 322 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2023 inatoa maelekezo na masharti ya kisheria kuhusu mikusanyiko au maandamano ya hadhara.

Amesema jeshi hilo limebainisha mambo 12 linayodai yanaendelea kupangwa mitandaoni kuelekea Desemba 9, yanayoashiria uvunjifu wa amani, ikiwemo kuzuia shughuli za kiuchumi na kuvuruga miundombinu muhimu ya mawasiliano.

"Wameelekezana kwamba asiyejua kutumia silaha awaachie waliopata mafunzo ya matumizi ya silaha. Hii maana yake ni kwamba watu hawa wanazo silaha za kutimiza makusudio yao," alisema.

Alisema baadhi ya ujumbe unaohamasishwa unawahimiza watu kuchoma na kuharibu minara ya mawasiliano, ili nchi ikose huduma, kufunga barabara zinazotoka na kuingia bandarini na kuziba mipaka yote ya kuingia na kutoka nchini.

Vilevile, mpango wa kuvamia hospitali na kuzuia utoaji wa huduma, pamoja na kuwalenga watumishi wa Serikali kwa madhara binafsi.

"Wakati hayo yakiendelea kwenye mitandao ya kijamii tumesikia matamko mbalimbali na wanao yatoa wanasema, wanaohamasisha na wanaohamasishwa wakiandamana siku hiyo tutawakuta wamekatana vichwa huko mitaani," amesema.

Katika taarifa ya Desemba 5, Misime amesema: "Hivi sasa wameongeza lingine wakihamasishana siku hiyo wabebe petroli kwenye chupa."

Wito kwa Wananchi

Jeshi la polisi limesema kwa mujibu wa sheria, maandamano ya amani na yasiyo na kikomo yanayohamasishwa, yamekosa sifa za kisheria za kuyaruhusu kufanyika.

"Hivyo, Jeshi la Polisi linatoa wito kwa Watanzania na wasio Watanzania ambao wapo ndani ya nchi wayakatae yanayohamasishwa, waendelee kuyakemea na wasishiriki," amesema.

Jeshi la Polisi limetoa wito kwa Watanzania wote pale watakapoona jambo lolote lisilo la kawaida au lenye viashiria vya kiuhalifu au la kuhatarisha amani na usalama wa nchi, wasisite kutoa taarifa kupitia simu namba 111, 112, 0699 99 88 99, 0787 66 83 06 au kwa ujumbe kupitia kiunganishi cha mfumo wa kutoa taarifa https://taarifa.tpf.go.tz.

Wamiliki wa Mabasi Watahadhari

Licha ya Jeshi la Polisi kuwahakikishia usalama raia, baadhi ya wamiliki wa mabasi yanayofanya safari mikoani wameeleza hofu waliyonayo kuhusu usalama wa biashara zao, wakisita kutoa huduma kama tahadhari dhidi ya maandamano ya Desemba 9, pia kutokuwa na uhakika wa abiria kupatikana.

Baadhi wanaeleza wamesalia na kumbukumbu ya Oktoba 29, ambayo baadhi ya mabasi yalichomwa moto kwenye maandamano yaliyoambatana na vurugu.

Kwa mujibu wa watoa huduma hao, tukio hilo limekuwa funzo na linawafanya kuchukua tahadhari mapema ili kulinda usalama wa abiria, wafanyakazi wao na mali zao, huku wakihimiza mamlaka husika kuimarisha ulinzi katika vituo na barabara kuu za usafirishaji.

Baadhi ya wamiliki wa mabasi wamesema uchomaji wa mali za umma na binafsi uliofanyika Oktoba 29 unawaogofya.

"Tunapenda kufanya kazi, lakini basi lako likichomwa unapata hasara kubwa. Wengi wetu tumepambana kumiliki haya mabasi katika mazingira magumu, halafu yakichomwa inaumiza," amesema mmoja wa wamiliki hao.

"Kama waandamanaji waliweza kuchoma mabasi ya watu binafsi, magari mengine na miundombinu ya umma, wewe utakuwa nani usichukue tahadhari? Mimi mabasi yangu safari ya mwisho itakuwa Desemba 7, yatabaki mkoani kusikilizia hali ya hewa."

Huduma Zitaendelea Kama Kawaida

Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustapha Mwalongo amekiri kusikia tetesi zinazosambaa kuhusu baadhi ya kampuni za mabasi kusitisha huduma kuanzia Desemba 8, 9 na 10, mwaka huu.

Amesema ukweli ni kwamba, hakuna kampuni itakayositisha huduma, isipokuwa baadhi zitapunguza idadi ya mabasi kulingana na upatikanaji wa abiria.

"Ukweli uliopo ni kwamba, zipo kampuni ambazo zitapunguza idadi ya mabasi. Tutakuwa tunaruhusu mabasi kulingana na idadi halisi ya abiria waliokata tiketi," amesema.

Amesema utoaji huduma utaendelea kama kawaida na mabasi yataelekezwa kwenye mikoa yenye idadi ya kutosha ya wasafiri.

"Uhitaji wa abiria ndiyo utatufanya tutoe mabasi. Huwezi kutoa basi kama abiria ni watano," amesema.

Amesema kampuni nyingi za usafiri zinaendesha biashara kwa mikopo, hivyo zinawajibika kufanya marejesho ya kila mwezi. Hali hiyo inawapa changamoto kuendesha magari barabarani endapo hakuna abiria wa kutosha.

Baadhi ya abiria wanaendelea kulala na kuamka katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli jijini Dar es Salaam wakitafuta usafiri wa kuelekea mikoani.

Mbali ya hayo, kumekuwa na ulanguzi wa tiketi, huku baadhi ya mabasi yakibeba abiria kupita uwezo wake.

Tags: Darulinziulivyoimarishwa
TNC

TNC

Next Post

Telecom Company to Build 132 New Towers to Strengthen Tanzania's Digital Network

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Popular News

  • Zanzibar’s Leadership Advocates for Streamlined Tax System to Enhance Economic Growth

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanaohujumu miundombinu watachukuliwa hatua kali

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanaohujumu miundombinu watachukuliwa hatua kali

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wasiwasi juu ya Uchochezi wa Makada katika Jimbo la Katavi

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • Wanawake Wanaonyonyesha Washauriwa Kula Milo Mitano Siku

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Category

  • English
  • Swahili

Socials

Instagram TikTok YouTube Facebook

About Us

TNC (Tanzania News Company) is the primary Source of News in English & Swahili in Tanzania

© 2025 TNC - Tanzania News Company

Welcome Back!

Login to your account below

Forgotten Password?

Retrieve your password

Please enter your username or email address to reset your password.

Log In
No Result
View All Result
  • Home

© 2025 TNC - Tanzania News Company