Mahakama Kuu Yawaachia Huru Waliohukumiwa Miaka 30 Jela Tabora
Arusha – Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Tabora imewaachia huru wanne waliokuwa wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya wizi wa kutumia silaha.
Walioachiwa ni Adamu Seleli, Juma Ramadhani, Ramadhani Juma na Hamisi Emmanuel ambao kwa pamoja walihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na Mahakama ya Wilaya ya Nzega.
Warufani hao na mwenzao wa tano (ambaye si mrufani) walishtakiwa kwa kosa la wizi wa kutumia silaha ambapo walidaiwa kumvamia dereva bodaboda, Amani Clement, kumpora Sh20,000 kisha kumjeruhi kwa panga kichwani na mkononi.
Jaji Frank Mirindo, aliyekuwa akisikiliza rufaa hiyo ya jinai alitoa hukumu hiyo Desemba 4, 2024 na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Maelezo ya Tukio
Awali Aprili 9, 2024, dereva bodaboda huyo ambaye pia ni mkulima katika eneo la Kashishi wilayani Nzega, usiku akiwa anaongea na simu nyuma ya nyumba yake alivamiwa na watu watano akiwemo Hamisi ambao walimpekua na kumpora Sh20,000 alizokuwa nazo mfukoni na kumjeruhi kwa panga kichwani na mkononi.
Amani alidai kumtambua Hamisi kupitia taa zilizokuwa zinazomulika eneo hilo ila hakuweza kutambua wengine aliokuwa nao na kuwa baada ya kupiga kelele watu hao walikimbia.
Rekodi za hukumu hiyo zinaonyesha kuwa Amani alipelekwa katika Hospitali ya Nzega na baadaye Hospitali ya Rufaa ya Shinyanga kwa ajili ya matibabu.
Hukumu ya Mahakama ya Chini
Katika mahakama ya chini washtakiwa hao walitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela huku aliyekuwa mshtakiwa mwenzao, Ramadhan Mohamed akihukumiwa kuchapwa viboko.
Katika rufaa ya sasa warufani hao walikuwa na sababu mbili ikiwemo kutokutambulika vya kutosha eneo la tukio na kuwa mtu pekee aliyetambuliwa eneo hilo kwa mujibu wa ushahidi wa jamhuri ni Hamisi ambaye pia wakati wa usikilizwaji wa kesi ya msingi alikana maelezo aliyodaiwa kuandika polisi ambayo alidaiwa kukiri kosa.
Maamuzi ya Mahakama Kuu
Katika rufaa hiyo upande wa Jamhuri uliunga mkono rufaa hiyo na kueleza kuwa warufani hawakutambulika ipasavyo katika eneo la tukio wala kutajwa na watu walioenda kumuokoa Amani.
Jaji amesema mtu pekee aliyetambuliwa eneo la tukio ni Hamisi ambaye wakati wa usikilizwaji wa kesi ya msingi alikana maelezo ya awali aliyodaiwa kukiri kutenda kosa hilo.
Jaji Mirindo amesema baada ya kuchunguza maelezo hayo ya onyo haikujulikana kama ni sawa Hamisi alikiri kosa kwani yeye alirejelea makosa ya ujumla aliyofanya wilayani Nzega.
Baada ya kupitia mwenendo na hoja za pande zote mbili katika rufaa hiyo, Mahakama ilikubaliana na hoja za warufani na kuruhusu rufaa hiyo ambapo ilibatilisha na kuweka kando hukumu na adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela iliyokuwa imetolewa na Mahakama ya Wilaya ya Nzega na kuamuru warufani waachiwe huru.