Safari ya Utekelezaji wa Mpango wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto Mkoani Mbeya
Dar es Salaam – Safari ya utekelezaji wa Mpango wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) mkoani Mbeya inaendelea kuwa mfano bora wa namna takwimu, ushirikiano na ufuatiliaji wa karibu vinavyoweza kuleta mageuzi makubwa katika hatua za awali za maisha ya mtoto.
Desemba 2, 2025, hafla ya tathmini ya mkoa huo iliandaliwa kupitia mradi wa MMMAM (2023/2024–2025/2026), ambapo wadau walijadili mafanikio ya miaka mitatu na misingi iliyowekwa kwa ajili ya uendelevu wa huduma hizo.
Katika kipindi cha utekelezaji, mradi ulifikia halmashauri saba na kata 167 kati ya 172, ukinufaisha watoto 7,017 dhidi ya lengo la 4,433, sawa na asilimia 158 ya utekelezaji. Vilevile, walezi 6,327 walifikiwa kulinganisha na lengo la 4,066, sawa na asilimia 155.
Kupitia mafunzo kwa wasimamizi wa mashauri ngazi ya jamii 752, mfumo wa utoaji huduma umekuwa na uwiano na ubora zaidi. Uelewa wa wazazi kuhusu lishe bora, afya, malezi yenye mwitikio, usalama na ujifunzaji wa awali umeongezeka kwa kiwango kikubwa. Halmashauri pia zimejengewa uwezo wa kutumia takwimu kupanga na kutekeleza afua zinazoendana na mahitaji ya watoto na kaya.
Ushirikiano wa Pamoja Wazalisha Matokeo Mazuri
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Afisa Ustawi wa Jamii Mwandamizi kutoka TAMISEMI, Amina Mfaki, alisema mafanikio hayo "yanadhihirisha nguvu ya ushiriki wa pamoja na matumizi ya takwimu kuongoza maamuzi sahihi."
Alieleza kuwa usambazaji wa Bango Kitita la Mwongozo Jumuishi wa Huduma za MMMAM, pamoja na uimarishaji wa mafunzo na ufuatiliaji wa karibu, kumeongeza umahiri wa watoa huduma na kuweka msingi madhubuti wa kupata huduma bora kwa wakati.
TNC imebaini kuwa safari ya MMMAM imeonyesha namna ushirikiano wa serikali, wadau na jamii unavyoweza kutafsiri takwimu kuwa vitendo vinavyobadilisha maisha.
Mabadiliko Halisi katika Maisha ya Kaya
Mabadiliko katika maisha ya kaya yameonekana wazi. Wito Mwangomo, mlezi aliyefikiwa na mradi, alisema kabla ya mafunzo hakuelewa umuhimu wa michezo, lishe bora na malezi chanya. Kupitia wasimamizi wa jamii, familia yake imeweza kutengeneza vifaa vya michezo kwa kutumia rasilimali zilizopo, kuandaa milo kamili na kufuatilia huduma za afya.
"Tofauti ni kubwa sana kati ya watoto niliowalea awali na wale ninaowalea sasa," alisema Mwangomo.
Msingi Thabiti wa Uendelevu
Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa, Aika Temu, alibainisha kuwa mkoa sasa una msingi thabiti wa kuendeleza huduma za MMMAM. Alisisitiza matumizi ya Mwongozo wa CCSWOPG kupanga bajeti na vipaumbele kwa kutumia takwimu za ndani. Aliahidi kuendeleza uhamasishaji na kuimarisha huduma katika halmashauri zote.