Arusha – Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimewataka wanachama wake kuwa makini na matumizi ya teknolojia katika utendaji kazi, hususan Akili Mnemba (AI), ili kunufaika nayo bila kuhatarisha haki, utu na imani ya wananchi wanaohudumiwa.
Tahadhari hiyo imetolewa Desemba 5, 2025 jijini Arusha na Makamu Mwenyekiti wa TLS, Laetitia Ntagazwa, kwenye Mkutano wa Kawaida wa mawakili unaofanyika jijini Arusha.
Ntagazwa amesema pamoja na AI kuleta fursa pana katika sekta mbalimbali, pia inakuja na changamoto nyingi zinazoigusa moja kwa moja taaluma ya sheria, yakiwemo masuala ya faragha, uwajibikaji, usalama wa taarifa, maadili ya kitaaluma na upatikanaji wa haki.
"Tunaingia katika enzi ambayo akili bandia si dhana ya mbali tena, bali ni nyenzo halisi inayobadilisha mazingira ya kazi, mifumo ya kisheria na maisha yetu ya kila siku," amesema.
"Ni wajibu wetu kuelewa athari zake kimaadili na kisheria ili kuhakikisha ubunifu hauendi kasi kuliko uwajibikaji."
Akizungumzia mustakabali wa taaluma hiyo, Ntagazwa amesema ni muhimu kwa wanasheria, watunga sera na wadau wa teknolojia kujiandaa mapema kabla AI haijawa sehemu kuu ya utoaji huduma na maamuzi ya kitaasisi.
Amesema kuwa AI ikitumika kwa uangalifu na kwa kuzingatia misingi ya maadili, inaweza kuongeza ufanisi, kupanua upatikanaji wa huduma za kisheria na kuimarisha ubora wa taaluma katika sekta mbalimbali.
Hata hivyo, alionya kuwa matumizi yasiyodhibitiwa ya teknolojia hiyo yanaweza kuchochea upendeleo kwenye mifumo ya maamuzi, kudhoofisha uwajibikaji na kupunguza uadilifu wa kitaaluma.
Mkutano huo wenye kaulimbiu "Kujenga Madaraja: Utofauti kama Chachu ya Umahiri wa Kitaaluma," umeunganisha wataalamu kutoka sekta za sheria, fedha, elimu ya juu na teknolojia.
Akichangia katika mkutano huo, Wakili Elifuraha Laltaika amesema elimu juu ya matumizi ya teknolojia ni muhimu zaidi sasa, hususan katika usimamizi wa ushahidi.
"Ni muhimu kuepuka kupotoshwa na AI, hasa katika ushahidi wa picha, video na hata sauti, hivyo mafunzo haya yamekuja wakati mwafaka, tujiandae vema na mabadiliko hayo ya kiteknolojia" amesema.
Laltaika amewahimiza wajumbe kubadilishana maarifa ili kujenga mitandao itakayochochea ukuaji wa kiubora katika sekta ya sheria na maeneo mengine ya kitaaluma.
Aliongeza moja ya matarajio ya mkutano huo ni kuweka mikakati ya kuendeleza ubunifu unaozingatia maadili, ushirikishwaji na mifumo thabiti ya utendaji kazi isiyoathiriwa na teknolojia.