Mwenyekiti Mpya wa Halmashauri ya Karatu Aainisha Vipaumbele
Arusha – Mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya Karatu, Engelbert Aloyce Qorro ameainisha vipaumbele atakavyovitekeleza kwa kushirikiana na viongozi wenzake kufikia malengo waliyojiwekea ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Qorro alizungumza hayo Alhamisi Desemba 4, 2025 baada ya kuchaguliwa kwa kura zote 21 za madiwani wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Makamu Mwenyekiti wake, Cyril Placid James. Amesema anatarajia mahusiano mazuri kati ya madiwani na wataalamu wa halmashauri hiyo.
Mpango wa Utekelezaji wa Vipaumbele
Kuhusu utekelezaji wa vipaumbele vyake, Qorro alisema kwa kuzingatia Ilani ya CCM na Dira ya Taifa ya 2050, ataongoza wajumbe wa Kamati ya Fedha kuzunguka Kata zote 14 kuzungumza na wananchi juu ya vipaumbele vya mahitaji yao ili kuhakikisha kuna uwiano wa fedha za miradi ya maendeleo kwenye Kata zote.
"Jambo lingine nitakua daraja linalounganisha sauti na mahitaji ya wananchi na utekelezaji wa wataalamu wa halmashauri ili kuhakikisha maamuzi sahihi na maendeleo yenye tija yanayopimika kwa wananchi," alisema Qorro.
Uimarishaji wa Ukusanyaji Mapato
Mwenyekiti mpya alibainisha kuwa kwa kutumia mfumo thabiti ataimarisha ukusanyaji mapato ya ndani kwa kuhakikisha kila mapato yanayokusanywa kutokana na kodi, ada, leseni na huduma za halmashauri zinakusanywa kwa uwazi na kwa wakati kwa kufanya ufuatiliaji wa karibu na kutumia teknolojia ya kisasa ya malipo kidijitali.
Qorro aliongeza kuwa katika kuandaa bajeti, watalenga miradi yenye faida kwa wananchi na kutoa mafunzo kwa watumishi wa halmashauri ili kuongeza weledi na uwajibikaji katika ukusanyaji na utumiaji wa fedha za umma.
Mwenyekiti huyo alisema katika kufikia malengo hayo ataimarisha ujirani mwema na taasisi za umma zinazozunguka wilaya ya Karatu ambazo ni Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na Mamlaka ya Wanyapori nchini (TAWA).
Ahadi za Mbunge wa Viti Maalumu
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Arusha, Cecilia Paresso alisema atatumia uzoefu alionao kwa kushirikiana na viongozi wa wilaya na mkoa wa Arusha kwa ujumla kusukuma utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa asilimia 100.
"Uteuzi wangu ni kwa ajili ya wananchi wote wa Karatu, tushirikiane kwa pamoja Karatu yetu ing’ae kwa maendeleo. Mwenyekiti nipo tayari kuitumikia wilaya yangu na mkoa wa Arusha kwa ujumla na nitatoa ushirikiano wa kutosha kwenye baraza hili. Nitatumia uzoefu nilionao kuhakikisha Ilani inatekelezwa ipasavyo," alisema Paresso.
Alisema wajumbe wa baraza hilo wanayo kazi kuhakikisha ahadi zote walizoahidi wakati wa kampeni na yale ambayo wananchi wanataka kuyaona ambayo yamebebwa kwenye Ilani ya CCM yenye misingi ya Kazi na Utu inatekelezwa kikamilifu.
Mbunge wa Karatu Atoa Mwongozo
Naye Mbunge wa jimbo la Karatu, Daniel Awack amesema jukumu walionalo madiwani ni kuchochea miradi ya maendeleo na sio kuchochea migogoro kati ya madiwani na wataalamu wa halmashauri hiyo.
"Sisi wabunge na madiwani tuliochaguliwa tumekuja halmashauri kuleta maendeleo ya wananchi wetu, hatukuja halmashauri kupambana na Wakuu wa Idara. Tumekuja kupambania maendeleo na mapambano yetu makubwa tutayaelekeza kwenye ahadi tulizotoa kwenye vijiji vyote tulivyopita wakati wa kampeni," alisema Awack.
Aliongeza kuwa wataalamu wa halmashauri hiyo kwa kushirikiana na madiwani wataweza kujibu changamoto walizozianisha kwa sababu wananchi wanayo matumaini makubwa katika utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025-2030.