Vibarua Vinne Vinavyomkabili Meya Mpya wa Dar es Salaam Nurdin Shetta
Dar es Salaam. Wadau wa siasa wametaja mambo manne yanayomkabili meya mpya wa Jiji la Dar es Salaam, Nurdin Bilal maarufu Shetta, aliyechaguliwa Alhamisi, Desemba 4, 2025, kushika wadhifa huo kwa miaka mitano ijayo.
Mambo hayo ni pamoja na kurejesha mali na hadhi ya jiji hilo, kubadilisha muundo wa sasa wa jiji, ambalo mwaka 2021 lilivunjwa na Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli, na baadaye akaipandisha hadhi Manispaa ya Ilala kuwa Jiji la Dar es Salaam.
Kibarua kingine kinachomkabili Shetta ni kusimamia miradi ya jiji hilo na kuwaunganisha madiwani kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano.
Shetta, ambaye ni mwanamuziki wa kizazi kipya, amechukua nafasi hiyo baada ya kushinda kura za maoni za ndani za Chama cha Mapinduzi (CCM) zilizojumuisha wagombea mbalimbali, akiwemo Omar Kumbilamoto, meya wa jiji la Dar es Salaam aliyemaliza muda wake.
Changamoto za Muundo wa Jiji
Baada ya kuvunjwa kwa jiji la Dar es Salaam na Manispaa ya Ilala kupandishwa hadhi, baadhi ya wadau wa masuala ya utawala walisema suala hilo halikuwa sawa kwa sababu muundo uliowekwa ulipoteza hadhi ya jiji.
Oktoba 24, 2024, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Tamisemi, Mohamed Mchengerwa, alielekeza mchakato wa uanzishaji wa Mamlaka ya Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam uanze ili kuratibu maendeleo yote yanayofanyika kwenye halmashauri za mkoa wa Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Mchengerwa, Dar es Salaam ni mkoa unaotakiwa kuwa kioo cha nchi, na wageni wote wanapokuja wanaiona sura ya Tanzania.
"Mkoa huu unatakiwa kuwa na chombo kinachoratibu maendeleo ya mji huu na kuhakikisha mipango yote ya maendeleo inayofanyika hapa inakuwa na muunganiko ili kuleta ile sura tunayoitegemea," alisema Mchengerwa.
Ushauri wa Wadau
Akizungumza na TNC, mjumbe wa zamani wa Jiji la Dar es Salaam (kabla halijavunjwa), Saed Kubenea, amesema Shetta anatakiwa kuishauri Serikali kuangalia upya muundo wa jiji la Dar es Salaam, akisema kwa namna ulivyo si rafiki katika utoaji wa huduma za kiutawala.
"Huwezi kuwa na Jiji la Dar es Salaam, ukivuka Jangwani unaingia Manispaa ya Kinondoni, au huwezi kuwa na Jiji la Dar es Salaam lipo hadi Chanika, lakini ubalozi wa Marekani, Oystebay na Masaki, zote hazipo sehemu ya jiji hilo.
"Jambo la kwanza, meya anatakiwa kuishauri Serikali ibadilishe muundo wa jiji la Dar es Salaam ili kuleta ufanisi wa utendaji kazi kiutawala," amesema Kubenea.
Hata hivyo, Kubenea ametoa angalizo kuwa katika mabadiliko hayo ya muundo, wasijerejeshe muundo wa zamani, uliokuwa na kasoro ya kutokuwa na eneo la kiutawala, lakini kulikuwa na Jiji la Dar es Salaam.
Kubenea amesema wanaweza kuunda Jiji la Dar es Salaam lenye muundo kama jiji la Arusha au Manispaa ya Moshi, ambapo ndani kuna Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini, ndivyo wanavyopaswa kufanya hivi sasa.
"Wanaweza kuchukua baadhi ya kata zilizopo Kinondoni, Ilala na Ubungo ili kuunda Jiji la Dar es Salaam, kisha iwepo Halmashauri ya Wilaya ya Ilala ili kuwepo kwa maana zaidi. Ubalozi wa Marekani haupo Jiji la Dar es Salaam, lakini Kivule ipo katika jiji," amesema Kubenea.
Kurejesha Mali za Jiji
Mbali na hilo, Kubenea, ambaye ni mbunge wa zamani wa Ubungo, amesema kibarua kingine kinachomkabili Shetta ni kuhakikisha mali za jiji hilo, ikiwemo viwanja na Shirika la Maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam (DDC), vilivyopotea kabla ya kuvunjwa, zinarejeshwa.
"Jiji la Dar es Salaam lina mali nyingi zimechakaa, nyingine zimeibiwa huku watu wakizigeuza kuwa miradi yao binafsi. Kuna kazi kubwa kwa meya kuhakikisha mali za umma za jiji zinarudi," amesema Kubenea.
Mjumbe mwingine wa zamani wa jiji hilo, Patrick Assenga, ameungana na Kubenea akimtaka Shetta kuhakikisha anarejesha hadhi ya Jiji la Dar es Salaam tofauti na muundo ulivyo sasa.
"Zamani jiji la Dar es Salaam lilikuwa na hadhi kubwa kwa sababu lilijumuisha manispaa zote tano za mkoa. Sasa huwezi kuita jiji la Dar es Salaam kwa kuchukua manispaa moja. Hili la sasa si jiji la Dar es Salaam, bali ni halmashauri ya Ilala," amesema Assenga.
Umoja wa Madiwani
Wakati wajumbe hao wakieleza hayo, diwani wa Buyuni, Jesca Msola, amesema pamoja na mambo mengine, Shetta ana jukumu la kuwaunganisha madiwani ili kazi ifanyike kwa umoja na ushirikiano kwa manufaa ya wananchi wa jiji hilo.
"Pili, kuhakikisha miradi yote ya maendeleo ya jiji inasimamiwa vizuri na kukamilika kwa wakati," amesema diwani huyo.
Ahadi za Meya Mpya
Baada ya kuchaguliwa, Shetta, amewaahidi wananchi wa jiji hilo kuwa katika uongozi wake kila mtu atapata haki inayostahili, hakuna atakayekonewa wala kupendelewa.
Shetta, ambaye ni diwani wa Mchikichini, amesema yeye si meya bali ni Mwana Dar es Salaam.
"Tuwe watu wamoja, tusiwe na makundi, tunapopata kitu tunakwenda pamoja hakuna mtu kupendelewa, haya mambo katika uongozi wangu sitataka kuyaona.
"Ofisi yangu iko wazi, mnakaribishwa. Nasema hivi kwa sababu wapo watu wanaoweza kujimilikisha umeya. Mimi sio meya wa mtu," amesema Shetta.
Pia, Shetta ameahidi kuwaunganisha madiwani wote na watumishi, huku akiwashukuru kwa kumchagua kwa kishindo. Amesema umoja wao utawezesha kuongeza mapato zaidi kutoka Sh132 bilioni za sasa.
"Nakuomba Kumbilamoto uwe mwalimu wangu ili kufanikisha kazi kubwa iliyopo mbele yangu," amesema Shetta.
Kuhusu vijana, Shetta amesema kundi hilo ndilo lenye kujenga nchi, hivyo atahakikisha mkopo wa asilimia 10 unawafikia ili kujikwamua kiuchumi.
"Tuwape vipaumbele vijana wapate fedha hizi ili kujikwamua kiuchumi, tulinde amani yetu, tusishawishike vijana wenzangu," amesema Shetta.
Viongozi Wengine Waahidi Utendaji
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Halmashauri Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara, amewataka madiwani wenzake kwenda kuwatumikia wananchi ili kutatua kero zinazowakabili.
Naye, Meya wa Jiji la Arusha, Maxmillian Iranqhe, ambaye ametetea nafasi hiyo, amesema kazi kubwa iliyopo mbele yake ni kuwatumikia wananchi na kukamilisha miradi ya maendeleo katika jiji hilo.
Iranqhe, ambaye ni diwani wa Kaloleni, ameitaja miradi hiyo kuwa ni ukamilishaji wa jengo jipya la halmashauri ya jiji, ujenzi wa soko la Kilombero, Mrombo, kituo cha kisasa cha mabasi, uwanja wa michezo na masoko.
Mbali na hilo, amesema wataboresha miundombinu ya barabara ili zipitike wakati sambamba na ujenzi wa mitaro itakayopitisha maji wakati wa mvua.
Kwa upande wa mwenyekiti wa halmashauri ya Moshi, John Meela, ameahidi kuimarisha umoja na ushirikiano huku akisema kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa usawa.
"Naomba umoja na ushirikiano ili tuwatumikie wananchi waliotupa dhamana. Niwahakikishieni kila kata itapata mradi wa maendeleo bila ubaguzi," amesema Meela.